Monday 11 December 2017

KUBADILI HATI KUTOKA JINA LA MAREHEMU KWENDA MSIMAMIZI WA MIRATHI.

Image result for NYUMBA

NA  BASHIR  YAKUB -

Mara  kadhaa nimezungumzia   kuhusu  namna  bora  na  ya  kisheria  ya  kuuza  na  kununua  nyumba  au  kiwanja    kutoka  kwa msimamizi  wa  mirathi  baada  ya   mmiliki  halisi  kufariki.

Leo  tena makala haya yataeleza  kubadili  jina kutoka  jina  la  marehemu  kwenda  kwa  msimamizi  wa  mirathi. Kubadili  huku  kunaweza  kuwa  na  lengo  la  kuuza, kupangisha  , kugawa  kwa  warithi  au  hata  kubadili tu  kwa maana  ya  kubadili  bila  malengo haya juu.

Maelezo  katika  makala  haya yatatoka Sheria  ya  Usajili  wa  Ardhi  sura  ya 334 na  kanuni zake  za  mwaka  1954, pamoja  na Sheria ya  usimamizi  wa  Mirathi sura ya 352 na  kanuni zake  za mwaka 1963.

UTARATIBU  NI  HUU.

1.Lazima  kwanza ufungue  mirathi na  apatikane  msimamizi  wa  mirathi.  Tumeeleza  mara  nyingi utaratibu  wa  kufungua  mirathi . Tulisema kuwa,  kwa  marehemu  aliyekuwa  mkristo  utafungua  mahakama  maalum ya  wilaya(district delegate)  au mahakama kuu  ,  na  kwa  marehemu  aliyekuwa  muislam  au  aliyeishi  kimila  bila  dini   utafungua  mahakama  ya  mwanzo  au  Mahakama  kuu.
Kwahiyo hoja  hapa  ni  kuwa  hatua  ya  kwanza   lazima  awepo  msimamizi wa mirathi.

2. Msimamizi wa  mirathi  atakapokuwa  amepatikana  basi  atapewa  fomu  namba 4 na 5 za  usimamizi  wa mirathi. Fomu  hizi  zinatolewa  na  mahakama  na  ni  uthibitisho  kuwa   fulani  ni  msimamizi  wa  mirathi halali.  Hoja hapa hakikisha  unazo hizo  fomu   mkononi.

3. Ukishakuwa  na  fomu  hizo  mkononi  basi  utatakiwa  kutafuta  na  kujaza  fomu  nyingine iitwayo  fomu  ya  uwakilishi  maalum  wa  marehemu kisheria( Lega personal representative). Fomu  hii  ni  namba 20  kwenye  kanuni  za  usajili wa ardhi.

Fomu  hii  ndiyo  inayowezesha jina  la marehemu  kutoka  na  kuingia  la  msimamizi  wa  mirathi  kwa  mujibu  wa kifungu  cha 67 cha  Sheria  ya  Usajili wa  ardhi.  Fomu  hii  inapatikana  mahakamani au kwa  wanasheria, au  ofisi  za  ardhi.  Hoja  hapa  ni  ipatikane  hiyo  fomu  na  ijazwe kwa ukamilifu.

4. Baada  ya  hapo, kwa  pamoja  yaani  utachukua fomu  ya  uwakilishi  maalum iambatanishwe na fomu  ya  usimamizi  wa  mirathi  na   kupelekwa  ofisi  ya  msajili   ofisi  za  ardhi.  Ofisi  hizi  zipo  kikanda  itategemea  uko  wapi  ili  uje  pa  kupeleka. Zipo  kanda  ya  ziwa, kaskazini, Dar es salaam makao  makuu  nk.

5. Panaweza  kuwepo  mahitaji  mengine  ya  ziada  kutegemea hali(status) ya  ardhi  yenyewe  kwa  wakati  huo  au kutegemea  maoni  ya  msajili  kuhusu  mazingira  halisi  ya ardhi  husika. Hata  hivyo  haya  yaliyoelezwa  ndiyo  ya  msingi na  kama  yatakuwepo hayo  ya  ziada basi ni  yale  madogo  madogo.

ANGALIZO.

Ni  muhimu  kuchukua  hatua  hizi  mapema  hasa  mara  tu  baada  ya  kupatikana  msimamizi  wa  mirathi.  Hii  itasaidia  kurahisisha  miamala  mingine  ambayo  warithi  na  msimamizi  wa  mirathi  wangependa  kuifanya kwa urahisi  ili  kunufaika  na  ardhi  husika,  kwa  mfano  kukopa, kugawa  kwa  warithi, kuuza, kupangisha nk.

Kama  hili  litakuwa halikufanyika  mapema  basi  miamala  mingine  itafanyika  lakini  si  kwa  urahisi  na  uharaka kama ambavyo lingekuwa limefanyika mapema.
Kwa  ufupi  machache haya  yanaweza  kukusaidia  ikiwa  ni  muhitaji  katika  hili.
MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI   LA  JAMHURI   KILA JUMANNE.  0784482959,  0714047241bashiryakub@ymail.com


0 comments:

Post a Comment