Wednesday 17 January 2018

JE ALIYETEULIWA NA MAREHEMU KWENYE WOSIA KUSIMAMIA MIRATHI ANAHITAJI KUTHIBITISHWA NA MAHAKAMA ?.

Image result for MSIMAMIZI WA MIRATHI

NA  BASHIR   YAKUB -

Wako  wasimamizi  wa  mirathi  wa  aina  mbili. Kwanza ni  yule  ambaye  marehemu  mwenyewe  amemteua  kabla  ya  kufa  kwake  na  akaandika/kusema  kwenye  wosia  kuwa  fulani  ndiye  atasimamia  mirathi  yangu  baada  ya  kuondoka.

Pili,  ni  yule  ambaye  hakuteuliwa  na  marehemu  mwenyewe  bali   ameteuliwa  na  wanafamilia  kwenye  kikao  cha  familia. Kwa  walio  wengi  huyu  ndiye  tunamjua  kuwa  ni  lazima  jina  lake  lipelekwe  mahakamani  kwa  ajili  ya  kuthibitishwa  ili  aweze kuwa  msimamizi  kamili.  Makala yatapitia Sheria  ya  Usimamizi  wa Mirathi, Sura ya 352  na kanuni zake.

1.      HAKI  NA  WAJIBU  WA  WASIMAMIZI  WA  MIRATHI.

Haki  na  wajibu  wa  msimamia  mirathi  aliyeteuliwa  na  marehemu kabla ya kifo na  ambaye  hakuteuliwa na marehemu ni  sawa. Awe  aliteuliwa  na  marehemu  mwenyewe  au  aliteuliwa  na  wanafamilia  bado  haki  na wajibu  alionao  ni  uleule.  

Wajibu  mkuu  wa  msimamia  mirathi  ni  kuwa  mwadilifu, na  kuenenda  kwa  mujibu  wa  sheria  katika  kila  hatua  anayopiga katika  kusimamia  kwake  mirathi.

2. SIO LAZIMA MSIMAMIZI WA MIRATHI AWE  NDUGU/MWANAFAMILIA.

Hili ni  muhimu  zaidi  kulieleza.  Sio  kweli  kuwa  msimamizi  wa  mirathi  lazima awe  mtoto  wa  marehemu, shangazi, baba  mdogo/mkubwa,  mjomba kaka,dada nk.  Bali  msimamizi  wa  mirathi  anaweza  kuwa yeyote.  Suala  la  msingi  ni  atimize  sifa  za  kuwa  msimamizi  wa  mirathi. Na katika sifa hamna udugu.

Hakuna  haja  ya  kuwa  na  ugomvi  kuwa  msimamizi  wa  mirathi  lazima  atoke  katika  familia. Hakuna  ulazima  huo  ikiwa  mmeshindwa  kuaminiana  kwenye  familia. Mnaweza  kumteua  hata  kiongozi  wa  dini au  mtu  mwingine  yeyote  muadilifu  ambaye  mnadhani  ataweza  kutenda  haki  katika usimamizi.

Jambo  jingine  msimamizi  wa  mirathi  sio  lazima  awe  mmoja. Ikiwa  kuna  pande mbili  zinazozana  basi  sheria  inaruhusu  kila  upande  kutoa  msimamizi  wa  mirathi  ili  alinde  maslahi  ya  upande  wake.  Kwahiyo  wasimamizi  watakuwa  wawili   na  sheria  haikatazi.

Nyongeza ya  hapo ni kuwa hata kampuni  au taasisi  inaweza kuteuliwa kusimamia mirathi.

3. MSIMAMIZI  ALIYETEULIWA  KATIKA WOSIA  KUTHIBITISHWA NA MAHAKAMA.

Msimamizi  aliyeteuliwa  katika  wosia  naye  ni  lazima  kuthibitishwa  na  mahakama.  Sio  kwamba  kwakuwa  marehemu  kabla  ya kufa  alimteua  au kwasababu  ameandikwa  kwenye  wosia kama  msimamizi  wa  mirathi  basi  haina  haja  ya  kwenda  tena  mahakamani.

Ni  kweli  aliteuliwa  na  marehemu  kabla  ya  kifo   lakini  ni  lazima  athibitishwe  na  mahakama. Hivyo  ndivyo  sura ya 352 inavyosema
Ikiwa  hatathibitishwa  na  mahakama basi  hawezi  kusimamia mirathi. Lazima awe na fomu  ya  usimamizi  wa  mirathi  itolewayo  na  mahakama.

Fomu hii  ndiyo  inayoruhusu  kuuza  mali,  inaruhusu  kudai  madeni, unaweza  kuonesha  benki  na  akaunti  za  marehemu  zikafunguliwa  ili  mchukue  hela, inaoneshwa  kwenye makampuni  kama  kuna  hisa  ili kuweza  kupewa  hisa  za  marehemu nk, nk. Huwezi  kuonesha  wosia   ukaruhusiwa  kufanya  miamala  kama  hii.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI   LA  JAMHURI   KILA JUMANNE.  0784482959,  0714047241bashiryakub@ymail.com



0 comments:

Post a Comment