Wednesday 15 November 2017

UFANYE NINI UKIGUNDUA UMENUNUA ARDHI ILIYOWEKWA REHANI BILA KUJUA ?.

Image result for NYUMBA NA KIWANJA

NA BASHIR   YAKUB - 

Umenunua  kiwanja  au  nyumba.  Aliyekuuzia  amekuhahakikishia  kuwa kiwanja/nyumba  hiyo iko  salama  na  haina  mgogoro  wowote. Mbali  na  mgogoro  pia  amekuhakikishia  kuwa  kiwanja/nyumba  hiyo  hajaiweka  rehani  popote  ili  kuchukua  mkopo.

Amekuhakikishia  kuwa  mpaka  wakati unanunua  kiwanja/nyumba hiyo, ni kuwa  iko  salama  na  haijashikiliwa  na  benki  au taasisi  yoyote  ya  fedha  kwa  ajili  ya  mkopo.

Au pengine  hukuuliza  kabisa  kama  kuna  deni lolote,  umejikuta tu  umenunua  bila  kuuliza  swali  kama hilo. Baadae  sasa  ndio  unagundua  kuwa  kiwanja/nyumba  uliyonunua kuna taasisi  moja  ya  fedha  ambapo  aliyekuuuzia  alichukua  mkopo  na  kuiweka   dhamana/rehani  na  bado  hajamalizia  mkopo huo.

Taasisi  hiyo inakuonesha  nyaraka  halali  za  kushikilia  kiwanja/nyumba  hiyo kama  dhamana  muda  mrefu  hata  kabla wewe  hujanunua. Na  kwa  bahati  mbaya  aliyekuuzia hujui  tena  alipo  au  bahati  nzuri  unajua  alipo.

 Lakini hata ukijua alipo, tayari  umeishanunua  na  hela  ulishampa  na  kila  kitu  kilikwishakamilika. Nini  kinakusaidia  kukutoa  katika  hali  hii  ambayo  sasa unaelekea  kuingia  katika mgogoro  mkubwa wenye  sura ya hasara.
Sheria  namba 4 ya 199, Sheria  ya  ardhi  itatupatia majibu   ya  jambo  hili.

1.UNUNUZI WA AINA HIYO UNAVYOTAMBULIKA KISHERIA.

Ununuzi  wa  aina hiyo  unatambulika  kama  aina  ya ununuzi ambao  unaingilia  haki  ya  mtoa  mkopo. Kifungu  cha  69(1) cha  sheria  hiyo  kinauita  ununuzi  huo  kama  ununuzi  unaolenga  kupora/kuharibu(defeat)  haki  ya  mtoa  mkopo.

Mtoa  mkopo  hapa  ni  benki  au  taasisi  nyingine  ya  fedha iliyotoa  mkopo.
Kwahiyo  kujikuta  umenunua  eneo  lenye  mazingira  ya namna hiyo hadhi  yake ni kama ilivyoelezwa hapa juu.

2. HAKI  ALIZONAZO MTOA  MKOPO DHIDI YAKO MNUNUZI.    

Kifungu  cha  7(1)( cha  sheria  tajwa   kinasema  kuwa  ikiwa mtoa  mkopo  atagundua  kuwa  rehani  aliyoshikilia  imeuzwa bila taarifa/kuhusishwa, basi  atakuwa  na  haki  ya  kwenda  mahakamani  na  kudai  kutenguliwa(set aside)  kwa  ununuzi  huo.  Ununuzi  wako  wa  eneo  husika  utatenguliwa  na  mahakama.

 Kwenda  mahakamani  ni  baada  ya  kukutaka  mnunuzi  uondoke  au  uachie hiyo  ardhi  kwakuwa  ilikuwa  rehani  na  pengine  ukakataa.  Ikiwa  utakubali kuachia  kirahisi na kukubali  hasara  basi  haitakuwepo  haja  ya  mtoa  mkopo  kwenda  mahakamani.

Lakini ikiwa  utakaidi  basi  ataiomba  mahakama  itengue  ununuzi  wako kwakuwa  umeuziwa  wakati  akiwa  ameshikilia eneo  hilo  kama  dhamana/rehani.

3.  JE  WEWE MNUNUZI  UNA  HAKI  GANI.      

Kifungu  cha  71 ( 1) kinaeleza jambo  moja  ambalo  linaweza  kukusaidia  kama mnunuzi  katika  mazingira  kama  haya.  Ni  kuwa  utatakiwa  kuthibitisha  kuwa  wakati  unanunua  haukujua  kabisa  kama  nyumba/kiwanja hicho  kiliwekwa  rehani  sehemu.  Ni  kazi  yako  kuhakikisha  unathibitisha  kutokufahamu kabisa  lolote  kuhusu  kuwekwa  kwake  rehani  wakati  ukinunua.

Ikiwa  utaweza  kulithibitisha  hilo  basi  kifungu hicho  kinaeleza  kuwa  mahakama  haitatoa  amri  ya  kutengua  ununuzi  wako. Hilo  ndilo  linaloweza  kukuokoa  na kadhia  hii.

Hata  hivyo  kuthibitisha  jambo hili kuwa  hukujua  kuna  misingi  yake. Kifungu  cha 71(2) kimetaja  msingi  mkuu  wa  kuthibitisha  kuwa   hukujua ni  kuonesha kwa ushahidi   kuwa  kabla  ya  kununua  ulifanya  utafiti  wa kutosha(due diligence/actual  and constructive notice),  na  unaokidhi  viwango  vya  kisheria ili  kujiridhisha  kuwa eneo  unalonunua halina  tatizo/mgogoro.

Moja ya  hatua  unayotakiwa  kuthibitisha  ni kuonesha  kuwa  ulifanya  “official  search”  na taratibu nyingine ambazo  zinakidhi  viwango vya kisheria katika  kujiridhisha  kabla  ya  kununua.

Basi  ukiweza  kuthibitisha  hayo  ununuzi  wako hautatenguliwa. Na hapo ndipo tunaposisitiza  sana kuhusu  kufuata taratibu za kisheria za manunuzi ya ardhi lengo likiwa  kukuweka  salama na hatari  kama hizi  mbeleni. Tujihadhari.
MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI   LA  JAMHURI   KILA   JUMANNE.  0784482959,  0714047241bashiryakub@ymail.com


0 comments:

Post a Comment