Wednesday 1 November 2017

JE WAJUA KUTELEKEZA ARDHI NI PAMOJA NA HAYA.


Image result for ARDHI YETU

NA  BASHIR  YAKUB -

Kuna  mambo ambayo  yafaa  tujihadhari  nayo  sana  hasa  kipindi  hiki. Wengi wamefutiwa  umiliki wa  ardhi. Takwimu  za kufutiwa ni kubwa sana kipindi hiki kama ulikuwa hujui. Kwa  watu  wanaonunua  ardhi  na  kwenda  kuishi  nje  ya  nchi  hili  lawahusu  sana kabla hamjapoteza ardhi zenu.  

Najua  unachojua kuhusu  kutelekeza ardhi  ni pengine  kutokujenga,  au  kutoitumia  kama ilivyopangiwa matumizi, nk. Ni kweli lakini  hiyo ni maana  finyu  ya kutelekeza ardhi. 

Maana  ni  zaidi ya hiyo,  na  hapa tutaona  ili  ujihadhari na  uwezekano wa  kupoteza  ardhi  yako.

1.MAMBO  AMBAYO  UKIFANYA  UTAHESABIKA  KUTELEKEZA  ARDHI.

Mambo  haya  yameelezwa   na  Sheria  Namba  4  ya  ardhi  ya  1999 kifungu  cha  51(1).

( a ) Kutokulipa  kodi, tozo  au  ushuru  wowote  ambao  upo  kisheria  kwa  ajili  ya  ardhi  ni  kutelekeza  ardhi  kwa  mujibu  wa  sheria hiyo.  Mnazijua  kodi  za  majengo,  kodi  za  ardhi  nk.  Hizi  ni  muhimu  sana  na  kimsingi  ndizo  zinazoeleza  uhai  wa  ardhi  yako.

Ikiwa hulipi  hizi  hata  kama  eneo  hilo  umejenga  kiwanda  kinachofanya  kazi  saa  24  siku  7  za  wiki  bado  mbele  ya  macho  ya  sheria  unahesabika  kutelekeza  ardhi.  Dawa  ya  kuepuka  hili  ni  ndogo.  Lipa  hizo  kodi  na  tozo  kwa  mujibu  wa  sheria. Yamkini  hizi  huwa si  pesa  nyingi  sana ya  kumshinda  mmiliki  kulipa.

( b ) Jengo  ndani  ya  ardhi  kuwa  gofu  ni  kutelekeza  ardhi  kwa  mujibu  wa  sheria.  Lakini  pia   katika eneo  hilo  sheria  imetumia  neno “disrepair”.  Maana   yake  kutokufanya  ukarabati.  Kwa  tafsiri  hii  ni  kuwa  kumbe  hata  kutokufanyia  majengo  yetu ukarabati  nako ni  kutelekeza  ardhi.

Utaona  katikati  ya  miji  yetu  majengo ya  zamani machafu,  yaliyopauka. Japo  ndani  mwake  watu  wanaishi  na  maofisi  yamo  bado kwa tafsiri  ya  neno  “disrepair”  ni  kuwa  jengo  hilo  limetelekezwa.  Na  sheria  imeeleza  zaidi  kuwa itakuwa  mbaya  zaidi  ikiwa  jengo  hilo  linahatarisha  afya  au maisha  ya  watumiaji  wake , majirani  au  hata  wapita  njia.

( c )  Sheria  inasema  ikiwa  mmiliki  ardhi  ameondoka  nchini  na  hakuacha  mtu  yeyote  hapa  nchini  wa  kuangalia  ardhi  ile  kwa  ajili  ya  kuilinda  na  kutekeleza  masharti  yote  yanayohitajika kisheria  kwa  ardhi  hiyo basi atakuwa ametelekeza ardhi hiyo.  Sheria  imetaja  kabisa  maneno  mtu  “aliyeondoka  nchini”.  Hii  maana  yake  ni  maalum  kwa  Watanzania  wanaoishi  nje  ya  nchi.

Unayemuachia  ardhi  kazi  yake  kubwa   si  kukaa  kama  mlinzi kwenye  ardhi  hiyo. Laa hasha,  bali  kazi  yake  kubwa ni  kuhakikisha  anatekeleza  masharti  ya  umiliki  wa  ardhi  kwa mujibu  wa  sheria  kwa  niaba  yako.  

Na kama  kuna  mambo  ambayo yatahitaji  sahihi  yako  basi  ni  kuhakikisha  yanakufikia  na  kuyatia  sahihi  kama  inavyohitajika.

Wengi  walio  nje  wamefutiwa  umiliki  wa  ardhi   kwa  kukosa hili. Usimamizi  wa  ardhi  zao. Hata hiyvo  kifungu  hicho kimeeleza utaratibu  wa  kumtaarifu  Kamishna  wa rdhi  kuhusu  ardhi  yako  kabla  hujaondoka kwenda nje. Hii  inaweza  sana  kukuweka  salama.

 ( d ) Pia   ardhi  kuacha  kutumika  kwa manufaa, au  ardhi  kuwa imeharibiwa  kwa maana  ya  uharibifu  wa  mazingira nako ni kutelekeza ardhi. Unaweza kuwa  uharibifu   uliosababisha  wewe  au  wa  asili.

2.  IPI  ADHABU  YA  KUTELEKEZA  ARDHI.

Adhabu  ya  kutelekeza ardhi  ni kufutiwa  umiliki   kwa  mujibu  wa  kifungu  cha  49  cha  sheria  hiyo.  Ukifutiwa  umiliki  ardhi yako  atapewa  mtu  mwingine  au  itaingia  kwenye hifadhi  ya  ardhi ya serikali  inayosubiri kugawiwa. Ni  kitu  kibaya  sana.

Makala  nyingine  nitaeleza  taratibu  zinazotakiwa kufuatwa  kabla hujafutiwa umiliki wa ardhi  ili  ujue  kama  umeonewa  iwapo  limekutokea hili  au  kama  halijakutokea   ujue  kuwa  kwa  dalili  hizi  sasa  naanza   kufutiwa  umiliki.
MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI   LA  JAMHURI   KILA   JUMANNE.  0784482959,  0714047241bashiryakub@ymail.com




0 comments:

Post a Comment