NA BASHIR YAKUB -
1.UKOROFI WA
WASIMAMIZI WA MIRATHI.
Baadhi ya wasimamizi wa
mirathi ni wakorofi.
Baada ya kuteuliwa
kwa jukumu hilo
hawapendi kugawa mali
ili kila mtu
achukue chake. Inapaswa kufahamika
kuwa mali si za msimamizi
wa mirathi . Mali ni
za warithi halali
isipokuwa msimamizi ni
kiongozi tu. Kwa
maana hii anawajibika
kusikiliza warithi wanasema
nini ili mradi
kile wanachosema kisipingane na sheria.
Wakati mwingine warithi
wanataka wagawiwe mali
zao ili kila
mtu endelee na
maisha yake lakini msimamizi
hataki tena bila
sababu za msingi. Hili
linakuwa si sawa
isipokuwa kama kuna sababu
za msingi za kufanya
hivyo.
Sababu zaweza kuwa labda
anayetaka kugawiwa mali ni mtoto mdogo asiyeweza kumiliki
mali kwa wakati huo, ni mtu
asiye na akili timamu kwa
muda huo, kuna
shauri mahakamani kuhusu hiyo
mirathi linaendelea, mali hazijakusanywa zote, kuna
ugomvi kwa warithi
kuhusu mali ambao
utaathiri mgao nk.
2. WAJIBU MKUU WA
MSIMAMIZI WA MIRATHI.
Kifungu cha
108(1) cha Sheria
ya Usimamizi na
Uendeshaji wa Mirathi,
Sura ya 352 kinaeleza wajibu
wa jumla wa msimamia
mirathi. Kifungu kinasema kuwa
kazi kubwa ya
msimamizi wa mirathi
ni kukusanya, mali na
madeni ya marehemu,kutunza mali
hizo, kusimamia gharama za
mazishi na msiba, na
kugawa mali kwa wanaostahili. Na kazi
hii yote ifanyike kwa
uadilifu mkubwa.
Kwahiyo kumbe moja
ya kazi ya lazima
na ya kisheria ya
msimamizi wa mirathi ni
kugawa mali kwa warithi. Huu
ni wajibu ambao
msimamizi anawajibika kuutekeleza. Na atagawa
kwa mujibu wa
wosia au sheria husika kama
hakuna wosia. Hagawi anavyotaka
yeye. Nani apate nini
halipo katika hiari
yake.
3. MUDA
WA KUGAWA MALI
KWA WARITHI.
Kifungu cha 107 cha
Sheria ya Usimamizi na
Uendeshaji wa Mirathi kinasema kuwa
ndani ya miezi
sita tokea kuteuliwa
kwa msimamizi wa
mirathi, msimamizi huyo
anatakiwa kupeleka taarifa(inventory&account) mahakamani
akionesha ni namna
gani amekusanya mali
za marehemu, madeni, amelipa
gharama kama zipo
na kwa namna
gani amegawa kwa wahusika.
Kwahiyo kazi ya
kugawa yafaa ifanyike
ndani ya miezi
sita. Hii ina
maanisha inaweza kufanyika hata ndani
ya mwezi mmoja
tokea kuteuliwa ikiwa
atakuwa amekamilisha taratibu
zote.
Kifungu kinasema ikiwa
ndani ya miezi
sita hajapeleka taarifa (inventory&account) mahakamani na
kuna sababu za msingi na za kisheria
za kutofanya hivyo
basi iwe ndani
ya mwaka mmoja. Ikiwa ndani
ya mwaka mmoja
itashindikana kwasababu za msingi
na za kisheria
basi anaweza kuongezewa muda na
mahakama hadi miezi mingine
sita.
Pamoja na hayo sheria
hiyo imetoa uhuru
kwa mahakama kutoa amri
au agizo la
kugawa mirathi kwa
warithi halali katika
muda ambao itaona
unafaa na kupendeza.
Kuna muda mahakama
inaweza kuamrisha hata ndani
ya wiki tatu
mali iwe imegawiwa
na taarifa imerejeshwa
mahakamani.
Mara nyingi amri
za namna hii hutolewa
kutegemea na udharula
wa mazingira husika
na kinachohitajika.
4. NINI
UFANYE IKIWA MSIMAMIZI
HATAKI KUGAWA MALI.
Ikiwa msimamizi hataki
kugawa mali na hakuna
sababu za kisheria
zinazomzuia kugawa basi lipo jambo
moja unaweza kufanya.
Ni kutoa taarifa katika mahakama ambayo imemteua/kumthibitisha.Utapeleka malalamiko
yako hapo halafu
ataitwa kwa wito(summons) na atatakiwa
aoneshe sababu(show cause)
kwanini hagawi mali
kama sheria inavyotaka. Haufungui kesi
ila unapeleka tu taarifa.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA JAMHURI
KILA JUMANNE.
0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment