NA BASHIR YAKUB -
1.UKOMO WA HAKI.
Hakuna haki isiyo
na ukomo wa muda
unapokuwa unaidai. Huwezi kudai
haki muda wowote
unaotaka wewe. Ni lazima
udai haki ndani
ya muda.Na ni
ule muda tu uliowekwa na
sheria. Ipo sheria rasmi
inayoeleza muda wa
kudai haki mbalimbali.
Inaitwa Sheria ya Ukomo
wa Muda , Sura
ya 89. Katika
sheria hiyo hapajaelezwa tu ukomo
wa kudai haki
katika masuala ya ardhi bali
pia katika masuala
mengine yote ya
haki unazoweza kudai.
Ndani ya Sheria
ya Ukomo wa
Muda kumeelezwa ukomo wa
kudai haki iliyotokana
na masuala ya mikataba
na makubaliano, ukomo wa
kudai haki katika
masuala ya udhalilishaji, ukomo wa rufaa, ukomo wa
haki katika masuala
ya bima, madai ya fedha,
rehani za mikopo, na mambo mengine
mengi.
2. HUJAPITWA
NA MDA BADO UNAWEZA
KUIDAI ARDHI YAKO.
Wako watu huko
nyuma walidhulumiwa ardhi
muda mrefu na
sasa wamekata tamaa.
Wamekata tamaa kutokana na
kuona ni mda mrefu
umepita tangu haki
hiyo iporwe na
sasa wanadhani kuwa
hawawezi tena kudai
haki hiyo.
Wako watu wamedhulumiwa ardhi
katika masuala ya
mirathi, katika masuala
ya mikopo, katika
masuala ya mikataba
na makubaliano, katika
masuala ya ndoa na machumo
ya mali za ndoa, katika
masuala ya uvamizi, katika masuala
ya kuharibu mipaka
n.k. Na ardhi hapa
tunazungumzia mashamba, viwanja
na nyumba. Hivi kwa
pamoja ndivyo huitwa
ardhi.
Basi yafaa ujue
kuwa kama wewe ni
kati ya waathirika
wa jambo hili
basi bado unayo haki
ya kudai ardhi
yako madhali muda
huo haujakupita. Haki
yako inaishi mpaka
miaka 12 na
itakufa baada ya muda
huo. Kama imepita
miaka sita, mitano,
nane, kumi, n.k.
bado muda wako
wa kudai na
kurudishiwa ardhi upo.
3. KWA WANUNUZI WA ARDHI
ZENYE UTATA.
Kwa wale wanaonunua/ walionunua ardhi
zenye utata yafaa
nao wafahamu kuwa
hawapo salama mpaka
miaka 12 ipite
toka umenunua ardhi
hiyo. Muda wowote
kabla ya muda huo
kupita unaweza kupokea
wito wa mahakama
na kutakiwa kujibu
malalamiko kuhusu ardhi
uliyonunua au kupata kwa namna nyingine.
Ndio maana
mara kwa mara
tumekuwa tukiandika na
kusisitiza
kuhusu kufuata
utaratibu katika kununua/kupata ardhi
ili mwisho wa
siku uwe salama
na uwe na
amani na mali
uliyonunua/pata. Pata ardhi kwa kufuata
taratibu
za kisheria ili uishi bila
mashaka na ufurahie
mali yako.
4. ISEMAVYO
SHERIA KUHUSU MIAKA
12.
Schedule ya kwanza ,
Sehemu ya kwanza, 22,
ya Sheria Ya
Ukomo wa Muda ndiyo
iliyoeleza haki hii ambayo imeelezwa
hapa juu. Inasema kuwa
unatakiwa kudai ardhi
ndani ya miaka
12. Muda huu
unahesabika tangu siku
mgogoro ulipotokea. Ikiwa
tangu siku mgogoro
ulipotokea mpaka leo
haijapita miaka 12
basi bado uko ndani
ya muda , kwa
maana unaweza kudai
ardhi yako na
ikarudishwa.
Lakini ikiwa tokea
kutokea kwa mgogoro
na sasa unapotaka
kudai kurudisha ardhi
yako ni muda
umepita miaka 12 basi haki hiyo
umeiua mwenyewe na
muda tayari umekupita.
Mwisho niseme kuwa
katika haki zote za kudai
mali ni ardhi
pekee iliyopewa muda
mrefu wa kudai kuliko
nyingine. Hii ni kutokana
na umuhimu na
unyeti wa ardhi.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA JAMHURI KILA JUMANNE.
0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment