NA BASHIR
YAKUB -
Kwa kutumia kigezo cha usajili,
Tanzania tunazo aina kuu mbili za kampuni. Kampuni za ndani(Local
companies) na kampuni za kigeni ( foreign companies).
Kampuni za ndani ni zile
zote zilizoanzishwa hapa nchini na kusajiliwa hapa nchini. Hata
kama wanahisa wake wote ni raia wa kigeni kwasababu tu ya kuanzishwa hapa na
kusajiliwa hapa zinakuwa ni kampuni za ndani.
Kampuni ya kigeni ni ile
iliyoanzishwa na kusajiliwa nje ya Tanzania lakini ikaanzisha
ofisi/biashara/tawi hapa Tanzania. Sheria Na. 12 Sheria ya Makampuni kifungu
cha 433 kinasema hivyo. Kampuni kama imeanzishwa nje hata kama wanahisa wake
wote ni Watanzania, hapa kwetu hiyo bado ni kampuni ya kigeni.
Kampuni ya ndani inaposajiliwa
hupatiwa cheti cha usajili kiitwacho "Certificate of Incorporation"
kwa mujibu wa kifungu cha 15(2) Sheria ya Makampuni. Kampuni ya ndani inapopata
cheti hiki basi usajili wake huwa umekamilika na inatambulika rasmi kama
kampuni ya ndani.
Kampuni ya kigeni inaposajiliwa
hapa Tanzania hupatiwa cheti kiitwacho "Certificate of
Compliance" kwa mujibu wa kifungu cha 435(1) Sheria ya Makampuni.
Kampuni ya kigeni inapopata cheti hiki basi usajili wake huwa umekamilika
na hutambulika rasmi kama kampuni ya kigeni.
Acacia ni kampuni ya kigeni.
Kwa maana kuwa ilianzishwa nje ya Tanzania na kufungua shughuli zake hapa
nchini. Kwa hiyo ili ihesabike imesajiliwa Tanzania ilitakiwa kuwa na cheti
kiitwacho"Certificate of Compliance". Kutokuwa na cheti hiki maana
yake ni kuwa haijasajiliwa Tanzania na haitambuliki.
Nimesikia mjadala BBC SWAHILI
leo wanaojadili wakijiuliza inawezekanaje kampuni kubwa kama hii ikafanya
biashara bila usajili. Watanzania wengi pia wanajiuliza swali hili.
Jibu lake ni hili. Acacia ni
kampuni tanzu(Subsidiary Company) ya Barrick. Kampuni inakuwa tanzu pale
ambapo zaidi ya nusu ya hisa zake zinamilikiwa na kampuni nyingine. Ile
inayomiliki huitwa "holding company" na inayomilikiwa huitwa
"subsidiary company". Kwahiyo Barick ni " holding"
wakati Acacia ni "subsidiary".
Barrick inamiliki hisa za Acacia
63.9%. Kwa kusema hivi maana yake Barrick ndiye mwenye Acacia. Hata hivyo kwa
mujibu wa sheria hizi zinahesabika kampuni mbili tofauti na kila moja inabeba
wajibu na hatia zake yenyewe(its own responsibility& liability).
Basi kumbe kilichotokea ni kuwa
Acacia walikuwa wakifanya biashara kwa jina la Acacia lakini wakibebwa na
mgongo wa Barrick. Walijificha hapa na wakaweza kuishi bila usajili wa
kwao kama wao. Walijibeba kwenye usajili wa Barrick.
Barrick wao wanao usajili na
wanayo " Certificate of Compliance" ya kwao ambayo tayari wameitoa
hadharani. Kwakuwa haya ni makampuni mawili tofauti kila moja inatakiwa kuwa na
cheti chake kwa mujibu wa kifungu cha 487 Sheria ya Makampuni na
kutokufanya hivyo ni kosa kabisa. Kwa hiyo hivi ndivyo ilivyowezekana kampuni
hii kufanya biashara bila usajili miaka hii yote.
Adhabu ya kosa kama hilo ni
kifungo jela. Sheria Na. 12 Sheria ya Makampuni iliyofanyiwa Marekebisho mwaka
2002, kifungu cha 472 kinasema hivyo.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA JAMHURI
KILA JUMANNE.
0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment