NA BASHIR YAKUB -
Mikataba yoote ya kimataifa
huongozwa na wajibu wa aina mbili. Wajibu ulioandikwa(express obligation) na
wajibu ambao haukuandikwa(implied obligation).
Wajibu ulioandikwa ni masharti
yote ya mkataba yaliyo katika maandishi ambayo wahusika husoma na kuridhia,
wakati wajibu usioandikwa ni masharti ya mkataba ambayo hayakuandikwa katika
mkataba lakini yapo kwa asili au yapo kwakuwa tayari yalishasemwa na
sheria na hivyo si lazima kuyaandika ktk mkataba.
Mathalan, mfanyakazi wako
wa duka hawezi kukuibia halafu akasema kwenye mkataba wangu wa ajira hakuna
sharti la uaminifu. Laa hasha uaminifu ni sharti la asili
"implied obligation" kwa hiyo liandikwe au lisiandikwe bado
lipo tu.
Kwenye mikataba ya kimataifa
kama ile ya kwetu na makampuni ya madini masharti yafuatayo ni ya
asili na hayahitaji kuwa yameandikwa ili kuyatekeleza :
1. Wajibu wa kuanika taarifa zote muhimu kuhusu shughuli
inayotekelezwa katika mkataba( Implied covenant to disclose all necessary
information over the subject matter).
2. Wajibu wa kutekeleza na kutenda kwa nia njema(Implied
covenant to act in good faith and fair dealing).
3. Wajibu wa kila mhusika katika mkataba kuwa mkweli . Hili
huwa ni katazo la udanganyifu(Fraud).
Haya yawe yameandikwa kwenye
mkataba au hayakuandikwa yakikiukwa tafsiri yake ni kukiuka masharti ya
mkataba.
Matendo kama kulaghai kuhusu
uzito wa madini yanayochukuliwa, kulaghai kuwa unachukua dhahabu huku ukijua
unachukua zaidi ya dhahabu, kulaghai kuhusu bei , kutotoa taarifa sahihi za
kipi unapata na kipi hupati,nk ni kukiuka wajibu na masharti ya mkataba
jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Na ikiwa wamekiuka mkataba kwa
misingi hiyo basi Tanzania inaweza kufanya yafuatayo;
1. Kuendelea na mkataba lakini kwa sharti la kurudisha kile chote kilichopotea
kwa mda wote( specific performance).
2. Kutoendelea na mkataba na kudai fidia, hasara tuliyopata,pamoja
na riba zake kwa kipindi chote(breach of contract).
Ndugu zangu, wajibu wa
kutekeleza na kutenda kwa nia njema (implied covenant to act in good
faith and fair dealing), kuwa mwaminifu na kutoa taarifa sahihi katika
utekelezaji mikataba ni matakwa ya lazima duniani kote.
Sheria ya biashara ya Amerika
Uniform Commercial Code vifungu vya 1 - 12 habari hii imeelezwa kwa upana.
Sheria ya biashara ya Ufaransa
na Ujerumani The German Civil Code(BGB) na Civil Code of France zimeeleza vitu
hivi.
Pia mahakama kuu ya Uingereza
katika kesi ya Yam Seng PTE vs International Trade Co. Ltd (2013) EWHC 111 (
QB) iliamua kuwa masuala ya uaminifu na kutoa taarifa sahihi katika kutekeleza
mikataba ni wajibu ambao upo hata Kama haukuandikwa kwenye mkataba.
Halikadhalika sheria yetu ya
Mikataba, Sura ya 345 vifungu vya 18 na 13 vimeyafanya masuala ya
udanganyifu na kutoa taarifa zisizo sahihi kama mambo ambayo ni makosa
na yanayobatilisha mkataba.
Kamati ya Profesa Mruma
imebaini upotevu wa Bilioni 829.4 x Miezi 12 kwa miaka 18 =
Trilioni 829.4. Hizi ni pesa nyingi mno. Tunayo kesi nzuri ya madai
na uhakika wa kurejesha fedha tulizopoteza. Ni vema mda huu pamoja na
mambo mengine, nguvu nyingi ikatumika kuona ni namna gani tunapata hii fedha.
Makosa yapo na yametendwa na hilo halina Shaka. Iko wapi haja kukhofu,
hakika haipo.
Yumkini haitakuwa rahisi
kutokana na aina ya mabepari ambao tunashughulika nao. Ni mabepari
hatari wenye mtandao mkubwa wa kisiasa na nchi wafadhili pamoja na
taasisi kubwa kama IMF, WB, UN nk.
Hata hivyo tumeshasema hii ni
vita na vita sharti ipiganwe ili waliosiginwa wawe huru. Tunaweza kuumia
kwa mda ila mwisho wa maumivu hayo itakuwa ni neema kubwa na ya milele.
Mungu ibariki Tanzania na Mungu mbariki rais kwa
pamoja tushinde vita hii.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA JAMHURI
KILA JUMANNE.
0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment