NA BASHIR YAKUB -
SHERIA ZILIZOPITIWA :
1. Sheria ya
Mwenendo wa Kesi za Jinai, Sura ya 20.
2. Sheria
ya Huduma za Mashtaka kwa Taifa, Na. 27/2008.
3. Kanuni
za Adhabu, Sura ya 16.
_______________
Tundu Lissu anasema anaamua
kumshitaki Makonda kwa kosa la kughushi nk. kwa kuwa Serikali imekataa na
haioneshi nia ya kumfikisha mahakamani Makonda.
Kama sababu ni kuwa serikali
imekataa kumpeleka Makonda mahakamani ndio maana Tundu Lissu na
wenzake wanaamua sasa kuchukua hatua basi nao hawatafanikiwa.
Kwa sheria ilivyo
hawatafanikiwa mpaka serikali wanayosema haitaki itake. Kwa mujibu
wa kifungu cha 97 cha Sheria ya Mwenendo wa Kesi za Jinai kazi ya
kufungua na kuendesha mashtaka yote ya jinai ni kazi ya serikali kupitia
ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Jinai (DPP).
Hata hivyo kwa mujibu wa
kifungu cha 99(1) cha sheria hiyohiyo ni kweli bila
ubishi kuwa mtu binafsi
au Wakili yeyote binafsi kama alivyo Tundu Lissu naye anaweza
kufungua na kuendesha mashtaka ya jinai dhidi ya mtu yeyote mkosaji kama
ilivyo kwa DPP wa serikali.
Pamoja na hayo kifungu cha
97 cha sheria hiyo ya Mwenendo wa Kesi za Jinai kinasema kuwa ikiwa
mashtaka yamefunguliwa na mtu binafsi au Wakili binafsi kama alivyo Tundu Lissu
basi mwendesha mashtaka wa serikali akiamua anaweza kuchukua kesi
hiyo.
Pia kifungu kinasema zaidi kuwa
Wakili huyo binafsi katika kesi hiyo aliyofungua atalazimika kufuata
maelekezo ya mwendesha mashtaka huyo wa serikali wakati wote
wa kesi.
Maana yake ni kuwa ikiwa
mwendesha mashtaka wa serikali atamwamuru Tundu Lissu kubadili jambo lolote
katika kesi aliyofungua basi atalazimika kulibadilisha. Lakini kubwa kuliko
yote ikiwa mwendesha mashtaka wa serikali atamwamuru Tundu Lissu kufuta kabisa
kesi ya Makonda basi atalazimika kuifuta. Hii ndio maana ya kifungu
hicho.
Lakini pia kifungu cha 91(1)
cha hiyo kinasema kuwa DPP anaweza kuifuta kesi YOYOTE ya jinai
wakati wowote kabla ya hukumu. Neno kesi YOYOTE maana yake ni iwe imefunguliwa
na mtu au Wakili binafsi, au taasisi yoyote ya serikali au binafsi mathalan
Chama cha Wanasheria, DPP wa serikali akiamua kuifuta
anaifuta mara moja.
Kwa msingi huu wa sheria ndio
maana nikasema kuwa Kama Tundu Lissu anasema anamshitaki Makonda kwasababu
serikali imekataa kumshitaki basi utaona wazi kuwa bado
hataweza kumshitaki mpaka serikali iamue na itake.
Awali kifungu cha 90 cha sheria
ya Mwenendo wa Kesi za Jinai kilikuwa kikilieleza hili kwa undani kabla
ya kufutwa na Sheria Namba 27/2008 ya Huduma za Mashtaka kwa Taifa
kifungu cha 31.
Mwisho yatupasa kujua
kuwa Tundu Lissu hawezi kumshitaki Makonda mpaka apate idhini ya hakimu.
Kifungu cha 99(1) Sheria ya Mwenendo wa Kesi za Jinai kinasema hivyo. Nimemsikia
Lissu akisema kuwa ati wanachotakiwa kufanya ni kutoa taarifa kwa hakim
basi. Hapana sio kweli , kifungu kinasema ni idhini na ndio maana hakimu
anaweza kukataa au kukubali. Limetumika neno "MAY" kuashiria uhiari
wa hakimu.
Kwa ufupi Tundu Lissu na
wenzake katu hawataweza kumshitaki Makonda na kufanikiwa mpaka
serikali iamue na itake. Hakuna namna ambavyo unaweza kuikwepa serikali
katika hili.
Tanbihi
ni kuwa makala
hayasemi kuwa Tundu
Lissu hatafungua kesi, bali
ni
kuwa kama atafungua
kesi na ikaendelea hadi
mwisho basi bila
shaka serikali itakuwa
imeamua iwe hivyo
kwa kuacha kutumia
mamlaka iliyopewa na
sheria na si
kwa ujanja wa yeyote.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA JAMHURI
KILA JUMANNE.
0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment