Sunday 2 April 2017

NAMNA YA KUIJUA HATI ORIGINAL KABLA HUJANUNUA NYUMBA/KIWANJA , KUEPUKA UTAPELI.

Image result for hati za viwanja

NA  BASHIR  YAKUB -

Ni  wangapi  wamefanyiwa  utapeli  katika  harakati  za  kununua  viwanja  au  nyumba.  Ni  wangapi  wamepata  hasara  kubwa  kutokana  na  michezo  ya  utapeli  iliyotamalaki  katika  ardhi  nchini.  Ni  kesi  ngapi  ziko  mahakamani  zinazohusisha  utapeli   katika  mauzo na  manunuzi  ya  ardhi.  Idadi  ni kubwa  mno  na huu  ndio  ukweli.

Siku  zote  huwa tunasema  ni  vigumu  kujua   ukubwa  na  hatari  ya  jambo   hili  mpaka  likukute  au  limkute  mtu  wako  wa  karibu. Lakini  swali  ni  ikiwa  watu   wamekuwa  wakijifunza  kupitia  wenzao  ambao  wamekutwa  na  haya. Kama  na wewe  bado  hujajifunza  basi ni  muhimu  sasa  kujifunza.

Mtu   anauza  ardhi  moja  kwa  watu hata   zaidi  ya  wanne tofauti, mtu  anauza  ardhi  asiyokuwa  yake  huku  akijua  kabisa  sio  ya kwake, mtu  anaghushi  hati  au  leseni  ya  makazi  kisha  anauza  kiwanja  au  nyumba ya  mtu, kiongozi  wa  serikali  ya  mtaa   anashiriki  kuuza  ardhi  ya mtu   huku akijua  kuwa  juzi  mtu  mwingine  alinunua  ardhi  hiyohiyo, kwa  ufupi  hali  ni  mbaya  na  ni  vema  kusema  ili  watu  wachukue  tahadhari.

Wizara  ya  ardhi  imeshasema mara  nyingi  kuwa  moja  ya  sababu  kubwa  inayopelekea  watu   kutapeliwa  katika  manunuzi  ya  ardhi  ni  wanunuzi  wenyewe  kutozingatia  taratibu  za  kisheria  za  manunuzi. Migogoro  mingi  imezalika  hapa.

Mara  kadhaa  tumewahi  kueleza  kwenye  makala mbalimbali  namna  salama  ya  kununua  ardhi  kwa  kuepuka  utapeli.  Zipo  makala nyingi  ambazo  zimeeleza  hatua  za  kufuata  ili  uwe  salama.  Hata  hivyo  leo  kitaelezwa  kitu  kingine  ambacho  hakikuwahi  kuelezwa.  Ni  namna  ya kuhakiki  hati  au  leseni  ya  makazi   ili  kujua  ikiwa ni  halisi (original)  au  feki kabla  ya  kununua  kiwanja  au  nyumba.

1.UHAKIKI  ULIOWAHI  KUSHAURIWA.

Kabla  ya  kueleza  njia  nyingine  ya uhakiki  inayotakiwa  kuelezwa  leo hebu  tujikumbushe  njia iliyowahi  kuelezwa  katika  makala  zilizopita. Ni  uhakiki  wa  hati  kwa  njia  ya   upekuzi  rasmi( official  search).  Tulisema  kuwa  kupitia  njia  hii  utaandaa  maombi  kwenda  kwa   msajili  wa  hati(Registrar of Title)   ukitaka  kujua  ikiwa  nyumba /kiwan ja  unachotaka  kununua  kama kina  mgogoro  au  ikiwa kuna  mtu  mwingine  mwenye  maslahi  juu  yake.

Mgogoro  ni  kama  kuna  zuio  la  kifamilia( caveat), zuio  kutoka  mahakamani  na  mengine  yanayofanana  na  hayo.  Na  kuwapo  mtu  mwingine  mwenye  maslahi  ni  kama  kiwanja  au  nyumba hiyo kuwa   imesimama  kama  dhamana   ya  mkopo n.k.  Majibu  ya  vitu  vyote  hivi  utayapata utakapojibiwa   maombi  yako  ya  upekuzi  rasmi ( official  search).

2.  UHAKIKI   WA  KUIJUA  HATI  ORIGINAL.                                           

Hili  ndilo  linaloshauriwa   leo.  Ni uhakiki  wa  kujua  ikiwa  hati  ni  halisi  au  feki.  Upekuzi  rasmi(official  search) ulioelezwa  hapo  juu  kazi  yake  sio  kuonesha  uhalisi  au  ubatili  wa  hati  bali  husaidia  katika kujua  taarifa/maudhui( contents)  za  hati.  Na hii  ni  kwasababu  unapopeleka  maombi  haya hairuhusiwi kuambatanishi  hati.

Ni  kupitia  njia  hii  ya  kuwasilisha hati  halisi  kwa  msajili  unapoweza  kujua  uhalisi  au  ubatili  wa  hati. Basi unachotakiwa  kufanya  ni  kuchukua  hati  ya  kiwanja  au  nyumba unayotaka  kununua  na  kuipeleka  kwa  msajili  wa  hati.  Kama  muuzaji  hatokubali  kukupa  hati  ili  ukaihakiki  basi  muombe  uongozane  naye  akiwa  ameishika  yeye  mpaka  kwa  msajili.

Lakini  hautaenda  hivyo  bali  utafanya  maombi  maalum  ambapo  siku  utakapokuwa  unapeleka  hiyo  hati  utakuwa  tayari  umepeleka  maombi  kwanza  au  iwe siku  hiyo  ndio   unapeleka  maombi  pamoja  na  hati kwa  uhakiki. Pia  unaweza  kuwatumia  wanasheria  katika  hili.

Msajili  wa  hati  anachokifanya  ni  kuchukua  hiyo  hati  mliyoileta  na kuikagua  kwa  kutumia  mfumo(system) ikiwa  ni  halali  na  ikiwa   kweli  ilitolewa na  ofisi  yake.  Ikiwa  iko  sawa  atathibitisha  na  kubariki  muamala  wenu  na  ikiwa  si  sawa  pia  atasema.  Hakuna  namna  ambavyo  unaweza  kupewa  hati  feki  ikiwa  ulipitia  utaratibu  huu. Hata  mabenki  yanayokopesha  kwa  kukubali  dhamana  za  hati  hujiridhisha  kwa  njia  hii ili  kukwepa  dhamana  feki.
MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI   LA  JAMHURI   KILA   JUMANNE.  0784482959,  0714047241bashiryakub@ymail.com



0 comments:

Post a Comment