Monday, 3 April 2017

MAOMBI KWA KAMISHNA WA ARDHI KUZUIA KUFANYIKA KWA TRANSFER YA NYUMBA/KIWANJA .


Image result for WIZARA YA ARDHI

NA  BASHIR  YAKUB - 

Transfer  ni  kubadilisha  hati  au  leseni  ya  makazi  kutoka  jina  la  mmiliki  wa awali  kwenda  kwa  mmiliki  mpya.  Transfer  inaweza  kufanyika  kutokana na mauzo, kupewa  zawadi, fidia, n.k.  Kwahiyo  kuzuia  transfer  ni  kuzuia   kubadilishwa  kwa  hati  kutoka  mmiliki wa  awali  kwenda  mmiliki  mpya. Mara   nyingi  tumezoea   kuzuia   transfer  kwa  kutumia  mahakama ( court  injuction).

Sasa  yatupasa tufahamu kuwa  ipo  njia nyingine  nyepesi  ambayo  haihusishi  mahakama.  Ni  njia  ya  maombi  kwa  kamishna  wa  ardhi   kwa  mujibu  wa  Sura  ya  113 ,  sheria  ya ardhi ,namba  4, ya mwaka  1999  vifungu  vya  38, 39  na  41 . 

Kabla  ya kuona  ufanyeje  kutumia  njia  hii ni  vema  tuone    mazingira  ambayo   yakikutokea unaweza  kutumia  hiyo  njia.

1.HAYA  YAKITOKEA  UNAWEZA  KUPELEKA  MAOMBI  KWA  KAMISHNA.

( a ) Mme  wako  au  mke  wako  ameuza   kiwanja  au  nyumba  yenu  na  kuna  namna  ambavyo  mauzo  hayo   unadhani  sio  halali  kwasababu  yoyote  ile  ya  kisheria pengine ya  kutokushirikishwa,  au  kushirikishwa  lakini  baadae  kunyimwa  haki  yako  kwa  mujibu  wa  makubaliano au  vinginevyo. Lakini   wakati  huo   unadhani  huna  la  kufanya  kwakuwa  mauzo  tayari  yamefanyika  na  pengine  hata  wewe  ulishasaini.

( b ) Una  maslahi  na  haki  katika nyumba/kiwanja  cha  mirathi .  Mali  hiyo  imeuzwa  bila  wewe  kushirikishwa  au  umeshirikishwa  lakini  haki  zako  za  msingi  hazikuzingatiwa  au  namna  nyingine  yoyote  ambayo  kwayo  unahisi  mchakato  haukwenda  sawa.  Lakini   wakati  huo   unadhani  huna  la  kufanya kwakuwa  mauzo  tayari  yamefanyika  na  pengine  hata  wewe  ulishasaini.

( c ) Umemuuzia  mtu  nyumba/kiwanja  lakini  amekataa  kutekeleza  baadhi  ya  makubaliano  ya  msingi yaliyo  katika  mkataba  wenu  wa  mauziano  na  sasa  anafanya  mchakato  wa  kubadili  hati.

( d ) Na mazingira  mengine  yoyote ambayo  tayari  nyumba/kiwanja  kimeuzwa  lakini  ukaona  kuna  haja  ya  kuzuia  mchakato  wa  kubadilishwa jina  la  mmiliki  ili  baadhi  ya mambo yawekwe  sawa  kwanza.

2.   MAOMBI  KWA  KAMISHNA.

( a )Utaandaa  maombi  maalum  kwa  njia  ya  maandishi.  Maombi  utayaelekeza ( adress)  kwa  kamishna  wa  ardhi  Tanzania.

( b )Kichwa  cha  maombi  kitakuwa  kuzuia  kubadilishwa  kwa  umiliki  wa  nyumba/kiwanja  namba…,plot  namba….,  title  namba…… Utaweka  taarifa  zote  kama  zinavyoonekana  kwenye  hati.

( c ) Utaeleza  jina  lako  na  wewe  ni  nani  mpaka  utake  kuzuia  ubadilishaji  wa  umiliki.

( d ) Utaeleza  maslahi  yako  katika  nyumba/kiwanja  hicho  kwa  mfano  mke  halali, mkopeshaji, mrithi  halali,  mtia  sahihi  katika  mkataba  wa  mauziano,n.k.

( e ) Hakikisha  unaambatanisha  nyaraka  zote  muhimu  kama  kopi  ya  hati  kama  unayo, cheti  cha  ndoa, mkataba  wa  mkopo, mkataba  wa  mauziano  kama  unao, hati  ya  usimamizi  wa  mirathi n.k.

( f ) Utaeleza  ni  kwa  vipi  utaathirika  ikiwa  zuio  lako  halitakubalika  na  hivyo  transfer  kuendelea  na  hatimaye  kuhamia  jina  la  mmiliki  mpya.

( g ) Utaandika  jina  lako  na  utasaini,  kisha  utakwenda  ofisi  za  ardhi  na  kuuliza ofisi  ya  kamishna  wa  ardhi  ilipo  na  hapo  utaacha maombi  yako.

( h ) Pia wakati  mwingine kutokana  na  uharaka  wa  jambo   ni  muhimu  kuhakikisha unamuona  kamishna  wa ardhi na  kumueleza  tatizo  lako moja  kwa  moja.

3. FAIDA    ZA   NJIA   HII  DHIDI    YA  ILE  YA  MAHAKAMA.    

Haina  gharama  kubwa ,  ni  nyepesi,  haichukui  mda  mrefu, hatua  na  mchakato  wake  ni  za  kueleweka  zaidi, kwa  ufupi  njia  hii  ni  bora  zaidi  kuliko  ile  ya  mahakama.
MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI   LA  JAMHURI   KILA   JUMANNE.  0784482959,  0714047241bashiryakub@ymail.com
0 comments:

Post a Comment