Sunday 5 March 2017

NAMNA YA KUIOMBA MAHAKAMA IKUTAMBUE KAMA MZAZI WA MTOTO.


Image result for watoto

1.KUNYIMWA  MTOTO.

Wako  watu  ni  wazazi  na  wamezaa  lakini  wameyimwa  watoto.  Zipo  sababu  nyingi  zinazopelekea  hili. Matukio  ya  namna  hii  hayawatokei  sana  wanawake  na badala  yake  wanaume  ndio  waathirika  zaidi katika hili .  Ni  rahisi  na  kawaida  mno mwanaume  kuambiwa  na  mzazi  mwenzake   kuwa  huyu   mtoto  si  wako  hata  kama   anajua kabisa  huyo  mwanaume  ndiye  mzazi  halisi .  Leo haya  sio  maajabu  tena .

Upo  usemi  wao  kuwa mwanamke   ndiye anayejua  baba  wa  mtoto. Sitaki  kueleza  ukweli  au  upotoshi  wa  usemi huu bali  nawaza  iwapo  ni  sawa  kutumia usemi  huu   kupora  haki  ya  uzazi   wa mtu  ambaye  unajua  kabisa  ndiye  mzazi  halisi.

Na kwa  bahati  mbaya  wanaokutwa  na  kadhia  hii wamekuwa  hawajui  ni  hatua  zipi  wachukue. Wapo  wanaoamua kufanya  vurugu, wapo  wanaojiua, wapo  wanaoamua  kumuachia  mola, na  wengine  hukimbilia  serikali  za  mitaa  ikiwa  ni  pamoja  na  hatua  nyinginezo  zisizofaa.

Ukweli  ni  kuwa  hatua  hizo  haziwezi  kukusaidia  zaidi  utapoteza  muda  mwingi,  gharama  na  pengine  kuzua  matatizo  mengine  ambayo  hayakuwako.  Basi  sasa  yafaa   ujue  kuwa  sheria  imetambua  jambo  hili  na  imeweka  taratibu  nzuri  za  kufuata  ili  kuondoa  ujeuri  wa  aina  hii.

Sheria Namba  21, Sheria  ya  Mtoto  ya  mwaka  2009  imeeleza  nini  ufanye  kama  tutakavyoona   hapa  chini.  Lakini  kabla  ya  hilo  hebu  kwa  kutaja tu  tuone  sababu  kadhaa  zinazofanya  wazazi  hasa  wa  kike kuwanyima  wazazi  wenzao  haki  ya kutambulika  kama  wazazi  wenzao.

2.  SABABU .

( a ) Ukosefu  wa  kipato  ni  tatizo. Mtu  anajua  kabisa  fulani  ndiye  mzazi  wa  fulani  lakini  kwasababu  ya uchumi  mdogo  basi  anakataa  kumtambua mzazi  huyo  halisi  na  kumtambua  asiye  halisi.

( b ) Tofauti  za  kidini. Mtu  anasema  mtoto  wangu  hawezi  kutambulika  kwa  baba  fulani   sababu  ya  dini tofauti . Anasema  bora  akae  bila  baba  au  anamtafutia  baba  mwingine.

( c ) Kukomoa. Mtu  anamnyima  mtoto  mzazi  halisi  kisa  waligombana  na  hivyo  ni  nafasi  kwake  sasa  kumkomoa.

( d ) Familia  mbili  kutoelewana. Mtu  anasema  mtoto  wangu  hawezi  kuzaliwa  katika  familia  au  ukoo  wa  akina  fulani.

( e ) Ubaguzi  wa  rangi. Ndugu  wanamshawishi  mwanamke  amkatae  baba  wa  mtoto  kwakuwa   wao  ni  wahindi,  waaarabu  na  baba  ni  muafrika,  mzungu  au  kinyume  chake  n.k.

3.  NINI  UFANYE  KUTAMBULIKA  KAMA  MZAZI.

Sehemu  ya 5, kifungu  cha  34( 1 )( b )  cha  Sheria  ya  Mtoto ya 2009  kinasema  kuwa  mtu  yeyote  anayeamini  kuwa  ni  mzazi  wa  mtoto  fulani  anaweza  kuiomba  mahakama  itoe  amri  ya  kumtambua  rasmi  kama  mzazi.

Haraka  hapa  utaona  kuwa  kitu  kizuri  na  cha  kisheria  ni  kwenda  mahakamani  na  kuiomba  mahakama  ikutangaze  kama  mzazi  halali  wa  mtoto.  Itakuwa  ni njia  sahihi  kabisa  na isiyo  na  usumbufu.

( a ) NI  MAHAKAMA  IPI  UENDE  ?.

Kifungu  cha  3 ( a )  cha  sheria  hiyo  kinazitaja  mahakama  zinazoshughulikia  suala  hilo  kuwa  ni  mahakama  ya  mwanzo, ya  wilaya, ya  hakimu  mkazi  na  mahakama  kuu. 

Hata  hivyo  unashauriwa  kuitumia  mahakama  ya  mwanzo  iliyo  katika  eneo  lako au  ya  wilaya  iliyo  ndani  ya  wilaya  yako. Mahakama  ni  sehemu  salama  kabisa wala  huna   haja  ya  kuhofu.

( b ) NANI  ANAWEZA  KUOMBA  MAOMBI HAYA .

Maombi  haya  yanaweza  kuombwa  na  baba  ikiwa  mama  amedai  kutomtambua   kama  mzazi  halali  au  mama  ikiwa  baba  amemkataa  mtoto.

( c ) USHAHIDI  UPI  UJIANDAE  NAO.    

Kifungu  cha  35 cha  Sheria  ya  Mtoto kinajibu  swali  hilo na  hivyo  unatakiwa  kujiandaa  na  haya;

( i ) Kuthibitisha  ndoa  kama  mlikuwa au  mna   ndoa, ni  ushahidi.

( ii ) Kama  hakuna  ndoa  kutafanyika  kipimo  cha  DNA kama  ushahidi.

( iii ) Ushahidi  kuwa  baba  alifanya  taratibu  za  kiukoo/kimila  kumtambulisha  mtoto.

( iv ) Jina  la  ubini  au  la  baba  ambalo  mtoto  amesajiliwa/andikishwa  nalo,  ni  ushahidi.

( v ) Pia  nani  jamii  inamtambua  kama  mzazi  wa  mtoto  nao  ni  ushahidi  pia.
MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI   LA  JAMHURI   KILA   JUMANNE.  0784482959,  0714047241bashiryakub@ymail.com



0 comments:

Post a Comment