Tuesday 28 March 2017

JE NI MAKUBALIANO GANI YAITWE MKATABA ?.


Image result for MKATABA
NA  BASHIR  YAKUB - 

Yawezekana  katika  shughuli  zako  za  kila  siku unaingia  makubaliano  mbalimbali kama kuuza na  kununa  magari,  viwanja  na  nyumba, kutoa  huduma, kuajiri  na kuajiriwa, makubaliano  ya  vibarua, makubaliano  ya  kuagiza  mizigo  na  kupokea  mizigo, makubaliano  ya  kufanya  kazi   na  kulipwa  au  kulipwa baadae n.k. 

Makubaliano  yote  hayo  yaweza  kuwa  kwa  maandishi  au  kwa  mdomo.
Vyovyote  itakavyokuwa  swali  la kujiuliza  ni  kama  makubaliano  hayo  kwa  maandishi  au  kwa  mdomo  unaweza  kuyaita  mkataba.  Na  kama   yataitwa  mkataba  je  yanakubalika  kisheria.  Na je  sheria  inaweza  kukulinda  iwapo  limetokea  tatizo  lolote ?.

Tutahitaji  pia kujua  ikiwa  umedhulumiwa  katika  makubaliano   yawe  ya  maandishi  au  ya  mdomo   kama  inawezekana  kuchukua  hatua. Na je  ikiwa  makubaliano  hayo    sio  mkataba   ni  ipi  hadhi  yake  kisheria  na  yataitwaje.

1.AINA   ZA   MAKUBALIANO.      

Kuna  aina   kuu  mbili  za  makubaliano ambayo  yakikidhi  vigezo  yataitwa mkataba.  Kwanza  makubaliano  kwa  mdomo  na  pili  makubaliano  kwa  maandishi.
( a ) Makubaliano  kwa  mdomo   ni pale  unapokubaliana  na  mtu  katika  jambo  fulani  kwa  kuzungumza  tu.  Masharti,  vigezo  na  namna  ya  utekelezaji  wake  hufanyika  kwa  kuzungumza  tu.

Mpaka  makubaliano  yanakamilika  hakuna  popote  yanapokuwa  yameandikwa.  Jambo  la  msingi  hapa  ni  kuwa   aina  hii ya makubaliano  inakubalika  kabisa  kisheria . Ukweli  kuwa  hayakuandikwa  popote  katu  hauyabatilishi.

( b ) Makubaliano ya  maandishi  haya  ni  ya  kuandika.  Kila mlichokubaliana  kinawekwa  katika  maandishi  na  wahusika  wanasaini. Makubaliano  haya  nayo  yanakubalika  kisheria.

2.  JE  NI  MAKUBALIANO GANI  YANA  HADHI  YA   MKATABA ?.

Kifungu  cha  10 cha  Sheria   ya  mikataba ,  sura  ya  345  iliyofanyiwa  marekebisho  mwaka  2009  kinasema  kuwa makubaliano  yanaweza   kuwa  na  hadhi  ya  kuitwa mkataba  ikiwa  makubaliano  hayo  yamezingatia  mambo yafuatayo:

( a ) Hiari. Kuwe  na  hiari  kwa  wahusika  wote  waliongia  katika  mkataba.  Na  hiari  iwe  huru. Hiari  huru  ni  ile  inayotokana na  maamuzi  yasiyo  ya ushawishi  haramu.

( b ) Wahusika  wenye  hadhi.  Hapa  tunaongelea  wahusika ambao  hawako  chini  ya  umri  wa  miaka  18,  wahusika ambao  hawana  ugonjwa  wa  akili, wahusika  ambao  wakati  wanaingia  makubaliano  hawakuwa  wamelewa .  Pia  mhusika  anatakiwa  awe  mhusika halisi.

Asitokee  mtu  wa  kujifanya  ndiye fulani kumbe  sio.  Haya  yote yakikaa  vizuri  basi  makubaliano  yawe  ya  maandishi  au  ya  mdomo  yatakuwa   na  hadhi  ya  kuitwa  mkataba.

( c ) Malipo  halali.  Malipo  si lazima  pesa. Hata  kubadilishana  kitu  kwa  kitu,  huduma  kwa  huduma,  pesa  kwa  huduma    nayo  ni  malipo. Suala  la  msingi  hapa  ni  kuwa  kile  mnachobadilishana  kiwe  halali.

Ikiwa  mwanamke  atatoa  huduma  ya ngono  kwa  makubaliano  ya  malipo  tutasema  walichobadilishana  sio  halali  na  hivyo  makubaliano  sio  mkataba. Au  pesa  kwa  nyara  zilizopatikana  kinyume  cha  sheria,  au  pesa  kwa  dawa  za  kulevya  n.k .  Pande  zote  mbili  ni  lazima  ziwe  na vitu  halali  vya  kubadilishana.

Kwa ujumla  haya  matatu  yaliyotajwa  hapa  juu  yakitokea  basi  tutasema  makubaliano  yenu  sasa ni  Mkataba  halali. Likikosa  moja  au  likawepo  lakini  likawa  sio  halali  basi  hayo  makubaliano  hayatoitwa  Mkataba.  

Na makubaliano  yanapokuwa  na  hadhi  ya  mkataba  maana  yake  ni  kwamba  yanalindwa  na  sheria  na  kama  utadhulumiwa  au  kuvunjwa  bila  kufuata  taratibu   unakuwa  na haki   ya  kuchukua  hatua  za  kisheria ,kuomba  fidia   na  stahiki  nyinginezo.
MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI   LA  JAMHURI   KILA   JUMANNE.  0784482959,  0714047241bashiryakub@ymail.com




.

0 comments:

Post a Comment