Monday 13 March 2017

JE MWISHO WA KUTOA MATUNZO YA MTOTO NI MIAKA MINGAPI ?.


Image result for BIDHAA ZA DUKANI MTOTO

NA  BASHIR  YAKUB - 

Matunzo  ya  mtoto  hasa  kwa  wazazi  waliotengana  ni  pamoja na  chakula,  makazi,  mavazi,  elimu,  pamoja  na  malezi  bora. Wazazi  wote  kwa  pamoja  yaani  baba  na  mama  wanao wajibu   kila  mmoja  kwa  nafasi  yake kuchangia  katika   matunzo  ya  mtoto.

Aidha  makala  haya  kupitia Sheria  ya  Mtoto ,Na. 21  ya  2009   yatajibu  ikiwa  suala  kutoa  matunzo  ya  mtoto  ni  la  milele  au  linao  muda  maalum.  Lakini  kabla ya  hayo  tutizame  nani  ana  mamlaka  ya kufungua  shauri  kudai  matunzo  ya  mtoto.

1. NANI  ANAWEZA  KUFUNGUA  SHAURI  LA  MATUNZO.

Wengi  wetu  twajua  kuwa  ni mama  wa  mtoto  pekee  ndiye  anayeweza kufungua  shauri  la  mtoto  kupatiwa  matunzo.  Dhana  hii  si  kweli.
Kifungu  cha  42( 1 )   cha  Sheria  ya  Mtoto  kinawataja  wafuatao  kuwa  na  mamlaka  ya  kuomba  mtoto apatiwe  matunzo :

( a ) Mzazi  wa mtoto.  Kifungu  hakikutaja  mama  wa mtoto  bali  mzazi  wa  mtoto. Kwahiyo  hata  baba  anaweza  kufungua  shauri  akimtaka  mama  kutoa  matunzo  ya  mtoto.  Mama  kumtelekeza  mwanae   nako ni kumnyima  mtoto  matunzo  .
Wako    mama  wanakimbia  nyumba  zao  na  kuwaacha  watoto. Unaweza  kutumia  kifungu  hiki  kumtaka  mama amchukue  mwanae  na  akae  nae  ikiwa  ni  sehemu  ya  matunzo.

( b ) Mlezi  wa  mtoto  naye  amepewa  mamlaka  ya  kufungua  shauri  kuomba  matunzo  ya  mtoto.  Wako  watu  wako  mjini  lakini  wamewaacha  watoto  vijijni  wakilelewa  na   ndugu au  rafiki.

Lakini  pia  yapo  mazingira  ambapo  kwa  amri  ya  mahakama    imeamriwa  mtoto  asikae  na  wazazi  bali  akae  na  mlezi  kutokana  na sababu  mbalimbali. Au  kwasababu  nyingine  yoyote mtoto  anakaa  na  mlezi .
Basi  ni  katika  hali  hiyo  mlezi  huyo  anayo  mamlaka  ya  kuomba  au  kufungua shauri  akishinikiza  mzazi/wazazi  kutoa  matunzo  ya  mtoto.

( c ) Mtoto  mwenyewe    kama  anao  uwezo  anaweza  kuomba.  Anaweza  kuomba  mwenyewe  au  kwa  kumtumia  ndugu  yake  au  rafiki  yake. Hii  haswaa  ni  pale  ambapo  mtoto  anakuwa  ametelekezwa  na mzazi  mmoja au  wote  wawili  lakini  akiwa  anajua  wazazi  walipo.

Wapo  watoto  wako  mitaani  hasa  wale  wanaoitwa  machokoraa   lakini  wazazi  wao  wapo  na  wanajulikana  na  watu  wanawajua  kabisa. Kwahiyo  mtoto  mwenyewe au  mwanajamii  kwa  kutumia  jina  la  mtoto  huyo  unaweza kufungua  shauri kuwalazimisha wazazi/mzazi  aliyepo  kumpatia  mtoto  huyo  mahitaji  akiwemo  elimu.

( d ) Wengine  ambao  wanaweza  kufungua  shauri  la  matunzo  ni  ustawi  wa  jamii  pamoja  na  ndugu  wa  mtoto  husika.

2.  JE  MWISHO  WA  KUTOA  MATUNZO  NI  MIAKA  MINGAPI  ?.

Kifungu  cha  47 cha  Sheria  ya  Mtoto  kinasema amri  ya  kutoa  matunzo  ya  mtoto  itakoma  mtoto  huyo  atakapofikisha  umri  wa  miaka  18.  Sheria  inamtambua  mtu  mwenye  umri  wa  miaka 18  kuwa  mtu  mzima.

Pia   atakupokuwa  amepata  ujira  wa  kumuingizia  kipato  au  amefariki  dunia  napo  amri  ya  matunzo  ya  mtoto  itakoma.
Hata  hivyo  kifungu  cha  48( 1 )  cha  sheria  hiyo  kinasema  kuwa  ikiwa  mtoto  amefikisha  miaka  18  lakini  bado anasoma shule au  chuo  cha  mafunzo  basi  kutoa  matumizi  hakutakoma  mpaka  hapo  atakapokuwa  amehitimu.

Kwahiyo    kwa  ujumla  mwisho  wa  kutoa  matumizi  ni miaka 18  lakini  ikiwa  mtoto  anaendelea  na  shule  au  chuo  cha  mafunzo  basi  matumizi yataendelea  kutolewa  mpaka  ahitimu.
MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI   LA  JAMHURI   KILA JUMANNE.  0784482959,  0714047241bashiryakub@ymail.com



0 comments:

Post a Comment