Wednesday 8 March 2017

JE BABA ANATAKIWA KUTOA SHILINGI NGAPI ZA MATUNZO YA MTOTO ?.


Image result for MATUNZO YA MTOTO

NA  BASHIR   YAKUB -

Wazazi  wanapokuwa  wametengana  matunzo  ya mtoto  ni  jambo  jingine  linaloleta    faraka  kubwa. Nani  anawajibu  wa  kutoa  matunzo  ya mtoto,  na  matunzo  yenyewe  ni  kiasi  gani  hubaki  kuwa  kiini  cha  ugomvi.

Wapo  wanaotoa  lakini  anayepewa  anasema  anapewa  kidogo.  Anayetoa  naye  anasema  natoa  kidogo  kwasababu  sina. Huyu  naye  anauliza  kama  huna  kwanini  ulizaa. Mambo  kama  hayo  na mengine  mengi  yanayofanana  na  hayo.

Basi  katika  kupitia  Sheria  namba  21, Sheria  ya  mtoto  ya  mwaka  2009   tutatizama   nani  anatakiwa  kutoa matunzo  ya  mtoto  halikadhalika  ni  kiasi  gani  kinatakiwa  kutolewa.

1.NANI  ANAWAJIBIKA    KUTOA  MATUNZO  YA  MTOTO.

Kifungu  cha  41  cha  Sheria  ya  Mtoto ya  2009   kinasema kuwa wajibu  wa  kutoa  matunzo  ya  mtoto  upo kwa  mtu   anayetambulika  kama  mzazi. Kifungu  hakikutaja  jinsia   ya  mzazi  bali kinamtaja  yule  ambaye  ni  mzazi. Hii  maana yake  ni kuwa  kila  mzazi   awe  baba au  mama  anao  wajibu  wa  kuwajibika katika  kutoa  matunzo  ya  mtoto.

Kifungu  kinasema  mzazi  atawajibika  kutoa  yale  mahitaji  yote  muhimu  kwa  mtoto( necessities).
Kifungu  cha  8( 1 )  cha  sheria  hiyohiyo  nacho   kinaeleza  kuwa  wajibu  wa  kutunza  mtoto  ni  wa  mzazi,   kwa  maana  ya  mzazi   yeyote  kati  ya  wawili.

Kifungu  hicho  kinakwenda  mbali  kwa  kueleza  maana  ya  matunzo ambapo kinataja  matunzo  kwa  kumaanisha, chakula  cha  mtoto, makazi  ya  mtoto, mavazi  ya  mtoto, huduma  za  matibabu  na  afya   kwa  mtoto, elimu  na  mwongozo  kwa  mtoto, uhuru  kwa  mtoto, na  kumpa  haki  ya  kucheza  na  kujumuika  kama  mwanajamii.

Kwahiyo  kila mzazi  baba  au mama anao  wajibu  wa kumtunza  mtoto  na  matunzo  yenyewe  ndiyo  haya.  

2.   BABA  KUTOA  MATUNZO.    

Hapo  juu  tumeona  kila  mzazi  anao  wajibu  wa  kutoa  matunzo  ya  mtoto. Hata  hivyo  matunzo  kati  ya  baba  na  mama  yanaweza  kutofautiana. Ikiwa  mtoto  anakaa  na  mama  pengine  ni  mdogo  na  mama  ndiye  mlezi  basi  kukaa  naye  huko  ni  matunzo kwa  upande  wa  mama.

Baba  ambaye  hakai  na  mtoto  kama  mlezi  wa  muda  wote naye  sasa anatakiwa  kutoa  mchango  wake  kwa  ajili  ya  chakula na  mengine  yaliyotajwa  hapo  juu.
Hapa  ndipo  linapokuja  suala  la  baba  kutakiwa  kutoa    hela. Na  hapo  ndipo  tutakapotizama  ikiwa  anatakiwa  kutoa  hela  basi  atoe  kiasi  gani.

3.  JE  BABA  ATOE  SHILINGI  NGAPI   ZA  MATUNZO ?.

Kifungu  cha  44( a )   cha  Sheria  ya  Mtoto  kinasema  kuwa  wakati  amri  ya  kutoa  matunzo  ya  mtoto  itakapokuwa  inatolewa   basi  kipato  cha  yule  anayetakiwa  kutoa  matunzo kitazingatiwa.  Hakuna  popote  kifungu  hiki  kimetaja  kiasi  cha  hela  kinachotakiwa  kutolewa . 

Kwahiyo  kwa  haraka  utaona  kuwa   kama  ni  baba  anatakiwa  kutoa  matumizi  basi  atatakiwa  kutoa  kulingana  na kipato  chake.  Haiwezekani  baba  mwenye  kipato  cha  laki  tatu  kwa  mwezi   akatakiwa  kutoa  matunzo  ya  laki  nane  kwa  mwezi.  Amri  ya  matunzo  ni  lazima  izingatie  kipato  cha  mtoaji.  

4.  JE  INAWEZEKANA  BABA  KUSEMA  SINA  KABISA  KIPATO ?.

Ndio  inawezekana, lakini  kusema  hivyo  hakutamwondoa katika  wajibu wa  kutoa  matunzo  ya  mtoto.  Hakuna  sina  itakayoua  haki  ya  mtoto  kupata  matumizi. Ni  lazima  baba  ahakikishe mtoto  anapata  matumizi .
MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI   LA  JAMHURI   KILA JUMANNE.  0784482959,  0714047241bashiryakub@ymail.com.


10 comments:

  • Uno says:
    12 March 2017 at 16:02

    Asante kwa mada

  • Unknown says:
    24 December 2018 at 12:33

    Asante sana kwa kutuelimisha kaka

  • Unknown says:
    9 August 2019 at 13:47

    Je kwamm ambae nachukua million moja na mwanamke analazimisha tuachane na tuna watt wawili na anaujauzito je ktk hyo million ntabaki na bei gani

  • Unknown says:
    30 August 2019 at 14:10

    Utatoa 50000 elf kwa kika mtoto

  • mgallason says:
    31 August 2019 at 01:50

    Asante kwa msaada huu na mimi ninayepata laki tatu je

  • Unknown says:
    19 October 2019 at 00:37

    Je mwisho wakutoa hizopesa mpaka umrigani

  • Unknown says:
    19 December 2019 at 07:15

    Kama baba anapata mshahara wa laki 3 anatakiwa kutoa sh.ngap

  • Unknown says:
    10 February 2021 at 20:09

    Asanten mme nielimisha

  • Unknown says:
    4 May 2021 at 02:46

    Sorry..hicho kiasi wanakikokotoaje.kwa asilimia labda

  • Unknown says:
    6 June 2021 at 12:11

    Kama baba anapokea milion moja na laki 2kwa mwez anatakiwa mtoto wake 1 amtunze kwa shilingi ngap kwa kila mwezi

Post a Comment