Monday 9 January 2017

NAMNA BORA YA KUEPUKA HASARA UNAPONUNUA ARDHI.

Image result for VIWANJA


NA  BASHIR  YAKUB - 

Wakati  mwingine  ununuzi  wa  ardhi   huweza  kuchukua  muda. Hii  ni  kutokana  na  mazingira ya ardhi  yenyewe  inayouzwa  au  kununuliwa  inavyokuwa.  Wakati  ununuzi  unachukua  muda  pia  huweza   kuchukua  gharama.  Gharama  hizi  zaweza  kuwa  zinatolewa na  mtu    anayetaka  kununua  au  anayetaka  kuuza.

Ifahamike  mapema kuwa  ardhi  hapa  tunazungumzia  viwanja, nyumba na  majengo.

Swali  letu  litakuwa ni je gharama  hizi  zinalindwaje na  sheria  ili  mtu  asiingize  gharama  halafu   kuuziwa  akauziwa  mtu  mwingine. Kabla  ya  hilo hapa  chini tuzijue  gharama  zinazoweza  kuingizwa  kabla  ya  kununua. 

1.  GHARAMA   KABLA  YA KUNUNUA  ARDHI.

( i )   Mnunuzi  katika  kutaka  kujiridhisha   kama  muuzaji  kweli  ni  mmliki   halali na  ikiwa ardhi  haina  mgogoro  hutakiwa  kufanya  upekuzi  maalum( official search).  Upekuzi  huu  hufanyika  ardhi  na  huwa  ni gharama . Ada  lazima  ilipwe  kabla  ya  upekuzi.

( ii )   Gharama  za  mwanasheria. Kwasababu  ununuzi  ni  mchakato  wa  kisheria  basi wanunuzi  huwaingiza  wanasheria katika  mchakato  huu   tangu  anapoiona  ardhi, kuipenda  na  kutangaza  kuinunua  kutoka  kwa  mmiliki. Kwasababu  mwanasheria  atampa  ushauri  wa  awali,  atamwandalia  maombi  ya  upekuzi,  atamsaidia  kukagua  hati  miliki na  mengine mengi, basi  gharama  za  awali  kabla  ya  mkataba  wa  ununuzi lazima  hutolewa.

( iii )  Wengine huwasaidia  wauzaji   katika  gharama  za mchakato  wa  kuteuliwa  kusimamia  mirathi  ili  waweze  kuwauzia ,  na  wengine  huwasaidia  wauzaji  kuwalipia  madeni  ili  ardhi  iwe  huru  na  iweze  kununulika.   

( iv )  Gharama  nyingine  huhusisha  upekuzi ( official  search)  BRELA  iwapo  mchakato  unahusisha  kampuni  mbili  au  hata  moja.  Hutakiwa  kulipia  ada  BRELA  ili  waweze  kukupatia  taarifa  za uhai,  ufu,   au  hadhi  ya  kampuni  kwa  muda  huo.

Gharama zote hizi  na  nyingine  nyingi  hutolewa  na mnunuzi  mtarajiwa  kwa  kutegemea ahadi   aliyopewa  na  muuzaji   kuwa  atamuuzia  yeye  na  si  vinginevyo.

2.  HATARI (RISKS)  YA  KUTOA  GHARAMA   KABLA.

Unaweza  kuwa  umetoa  gharama  hizi  ukiamini  kabisa   kuwa  baada  ya  kila  kitu  kwenda  vizuri   wewe  ndiye  utakayeuziwa  hiyo  ardhi.  Badala yake   muuzaji  akapata   mtu  mwingine  mwenye   ofa  kubwa   akakukwepa  na  kumuuzia  huyo  mtu.

Wakati  huu  hatajali  gharama  ulizokwisha  ingiza  katika  mchakato  wala  muda mwingi  uliopoteza  katika  kufuatilia  mchakato.  Ni  katika  mazingira haya   ambapo  mnunuzi  hutakiwa  kulindwa  na  mkataba  maalum  kabla  hajanunua  ardhi.

3.  MKATABA  MAALUM   KABLA  YA  KUNUNUA  ARDHI.

( i )   Mkataba huu  huitwa  “EXCLUSIVE  AGREEMENT”.  Ni  mkataba  ambao  muuzaji   hujifunga ( commit) kuwa  anampa  ruhusa  mnunuzi  aingize  gharama  katika  mchakato  wa  kuthibitisha  uhalali  wa  ardhi au vinginevyo, na  kuwa  yeye  hatomuuzia  mtu  mwingine yeyote.  Ni  mkataba  ambao  hufanywa  baada  ya   wahusika  kukubaliana  bei na  kila  kitu.

Athari  ya  nini   kitatokea  ikiwa  muuzaji  atakaidi  na  kuuza kwingine  hutanabaishwa ,  mfano  fidia na  kiasi  chake  hutajwa.

( ii )   Lakini  pia  ikiwa  mnunuzi  hatanunua  baada  ya  kuwa  amesubuliwa  sana  na   muuzaji  na  kuacha  kuwauzia  watu  wengine  nalo  huelezwa.  Kiasi  cha  fidia   hapa  napo  huainishwa  kwa  uzuri.

4.     UMUHIMU  WA  PEKEE  WA  MKATABA  HUU.

(  i  )   Humlinda   mnunuzi  asiingie  katika  hasara  kubwa   ya  fedha  na muda.

( ii )   Humlinda  muuzaji   na  hasara  ya muda  ikiwa  ni  pamoja  na  kuwaacha  wanunuzi  wengine  akitumai  kwa  mtu  ambaye  baadae  ameamua  kununua  kwingine  au kuacha  kabisa.

5.    HATUA  ZA  KUCHUKUA.

Ni  muhimu  ikiwa  unaona  ununuzi  unahitaji  kuingizwa  gharama  za  awali   kabla  ya  kununua   ufanye  hivi. Usiseme  namuamini  fulani  bali fanya  kwa   wote  unayemuamini  na  usiyemuamini.  Suala  la  kisheria  huwa  halina  anayeaminika  na  asiyeaminika.


MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MWANDISHI  WA MAKALA  YA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI   LA  JAMHURI KILA JUMANNE..0784482959,  0714047241bashiryakub@ymail.com

0 comments:

Post a Comment