Monday, 9 January 2017

JE MPANGAJI ANAWEZA KUPANGISHAImage result for FREM  ZA  MADUKA

NA  BASHIR   YAKUB -  

Sheria  Na  4  sura  ya  113 Sheria  ya Ardhi  ndiyo  sheria  inayotawala  habari  nzima ya  upangaji  na  upangishaji. Mpangaji  ni  mpangaji  anajulikana  lakini  swali  ni  kama  baada  ya  kupangishwa  na  yeye  anaweza  kupangisha. Hata  hivyo  kabla  ya  hilo  tutizame  vipengele  muhimu  vinavyotakiwa  kuwa  katika mkataba  wa  upangaji.

Ni  muhimu  kuangalia  vipengele  hivi  kwasababu  suala  la uwezo  wa mpangaji  naye  kupangisha  ni  moja  kati  ya  migogoro   kati  ya  wenye  nyumba  na  wapangaji  ambayo  husababishwa  na  mikataba   isiyoshiba  kwa vipengele  muhimu.

1. VIPENGELE  MUHIMU  KATIKA  MKATABA  WA  UPANGAJI.

(  i   )   Kipengele kuhusu tarehe  ya  kuingia  katika  mkataba  husika.

( ii  ) Kipengele kinachochambua  wahusika  katika  mkataba mfano  majina  yote  matatu, eneo analokaa au  anuani kamili na  nafasi zao  zitajwe   kuwa  huyu  ndiye  mpangaji  na  huyu  ndiye  mpangishaji.

( iii )  Kipengele  kinachochambua vyema ardhi,  kama  ni  nyumba, shamba mfano  vyumba, stoo,jiko, ukubwa  ekari n.k  kama  ni  shamba.

( iv ) Kipengele  kuhusu kiasi  cha  kodi  kinachotakiwa  kulipwa  na  namna  ya  ulipaji  wake.

 (  v )  Kipengele  kuhusu lengo  la  pango  kama  ni  biashara, makazi  na  kama  ni  biashara  ya  aina  gani.

( vi ) Kipengele/vipengele kuhusu  haki  za  mpangaji   na mpangishaji katika  matumizi  ya  ardhi  husika.

( vii ) Kipengele kuhusu sharti  la  kupangisha  au  kutokupangisha  kwa  mtu mwingine.

( viii ). Kipengele kuhusu nani  anawajibika  kufanya  marekebisho .

( ix ) Kipengele kuhusu notisi  ya  kuvunja  mkataba  na  muda  wake  ielezwe  katika  mkataba.

( x ) Kipengele  kinachombana  mwenye  ardhi   kuwa  yote  aliyomwambia  mpangaji kuhusu  hadhi  na  hali  ya ardhi  husika kuwa ni  ya  ukweli, mfano  kuhusu  mvua  zikinyesha  eneo  halijai  maji, nyumba  haivuji na  kila  kitu  kinamchotaka  awe  mkweli.

( xi ) Kipengele  kinachonyima  au  kutoa  uhuru  wa  kuhuisha(renew)  mkataba.

( xii  ). Jambo  jingine  lolote  linaloweza  kuwa  muhimu. 

( xiii  ) Sehemu ya sahihi   na  shahidi, Ni  vyema  shahidi  awe  wakili.

2.  MPANGAJI  KUPANGISHA.

Ili  mpangaji  awe  na  uwezo  wa  kupangisha  itategemea  na  aina  ya  mkataba   alioingia  na  mwenye   ardhi. Ikiwa  mkataba  umeweka  bayana   kwa  kutoa  uwezo  kwa  mpangaji  kupangisha  basi  aweza  kufanya  hivyo.

Lakini  ikiwa  mkataba  hautoi  uwezo  huo  basi  mpangaji  hataweza  kupangisha  isipokuwa  apate  ridhaa  kutoka  kwa   mwenye  ardhi .

3.  MPANGAJI  KUBADILI  MATUMIZI  YA  ENEO.

Si  tu  mpangaji  haruhusiwi  kupangisha  bali  pia hata kubadili  matumizi  ya  eneo  au  kufanya  marekebisho   bila  taarifa  na  ridhaa  kwa  mwenye  ardhi  nalo  litakuwa kinyume  cha  sheria  ikiwa  mkataba  umekataza  kufanya  hivyo. 

Zaidi ya hilo kifungu  cha  93  cha  Sheria  ya ardhi  sura  ya 113  kinakataza  mwenye  ardhi kuchelewa  kutoa  majibu  ikiwa  mpangaji  ameomba  ridhaa  kati  ya yaliyoelezwa  hapa  juu.

4.  MASHARTI  KUBAKI  YALEYALE    IKIWA  MPANGAJI  ATAPANGISHA.

Ikiwa  mkataba utamruhusu  mpangaji  kupangisha  basi  hataweza  kupangisha  kwa  masharti  zaidi  ya  yale  aliyonayo  yeye  yaani  aliyopewa  na  mwenye  ardhi mwanzoni  wakati  akipanga.  Pia  muda  wa  kupangisha  hautakuwa mkubwa  kuliko  ule  uliopewa  yeye na  mwenye  ardhi.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MWANDISHI  WA MAKALA  YA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI   LA  JAMHURI   KILA   JUMANNE..   0784482959,  07I4047241bashiryakub@ymail.com

0 comments:

Post a Comment