Monday, 23 January 2017

KUTUMIA NYUMBA/KIWANJA CHA MTU KUKOPEA.


Image result for MKOPO

NA  BASHIR  YAKUB -

Sheria   inaruhusu  kutumia  ardhi  ya  mtu  kukopea.  Kwa  maana  mtu  ataomba  hati  yako   au  nyaraka   yako   yoyote  ile  ya  umiliki  halafu  ataitumia  kukopea. Inaitwa Rehani  ya  mtu  wa  tatu( third party mortgage).   Kifungu  cha  113 ( 2 ) cha  Sheria  ya  Ardhi  Na, 4 ya 1999  kimeeleza kitu  hiki. Hata  hivyo  yapo  mambo  tunayotakiwa  kujua  katika  mchakato  huu  wote.

Ili  mambo  yaende  vizuri  kutatakiwa kuwapo  mikataba  ya  aina  tatu  kama  tutakavyoona  hapa  chini.

1.MKATABA  WA  MKOPO.      

Mkataba  wa  mkopo  ( Loan  agreement)  ni  mkataba   kati  ya   mwomba  mkopo  na   na  taasisi  ya  fedha  inayotakiwa  kutoa  mkopo.  
Mkataba  huu  utakuwa  na  masharti   ya   mkopo  kuhusu  urejeshaji, muda  wa  kurejesha, viwango  vya  riba,  adhabu  za  kupitisha  muda  wa  rejesho, muda  ambao  mkopo  utadumu,  nini  kitafanyika  iwapo  mkopaji  atashindwa  kurejesha, haki  na  wajibu  wa  mkopaji  pamoja  na  mkopwaji.

Ifahamike kuwa  masharti  ya  mkopo    hayafanani.  Yanatofautiana  kutoka  taasisi  hadi  taasisi   na  pia yanatofautishwa  na  kiwango   cha  mkopo  pamoja  na  mazingira  yote  yanayouzunguka huo  mchakato. Huu  ni  mkataba  wa  kwanza.

2.   MKATABA  WA   REHANI.

Huu  ni  mkataba  wa  pili. Mkataba  wa  rehani ( mortgage deed ) utakuwa  ni  kati  ya  taasisi  ya  fedha  na  mtu  anayeweka  rehani. Kwahiyo  kama  wewe  unamdhamini  mtu  kwa  kumpa  nyumba  au  shamba  lako  ili  akakopee   basi  unatakiwa  kusaini  mkataba  huu. 

Yule  ambaye  jina lake  linaonekana  kwenye  nyaraka  ya  umiliki  ndiye  anayetakiwa  kusaini   mkataba  huu.   

3.   MKATABA  KATI  YA   ANAYEDHAMINI  NA  ANAYEDHAMINIWA.    

Aidha  usimkabidhi  mtu  hati  yako  akakopee  bila  kuwa  na  makubaliano  ya  kisheria na  huyo  mtu.  Ni  hatari  sana  kufanya  hivi   na   unaweza  kupoteza  na  wengi  wamekwishapoteza. 

Wengi  wanachojali  ni  mtu  achukue  hela  benki  na  wewe  akupe  asilimia  zako  mlizokubaliana  basi  muishie  hapo.  Ukifanya  hivi  utakuwa  umekosea  sana.
Wengine  huaminiana  tu  kwa  urafiki  au  undugu  na kufanya  mchakato  huu  bila  makubaliano  maalum.  Hii  si  sawa  na  ina  madhara  makubwa.

Hakikisha unamsainisha  mkataba  huu na  hakikisha  mkataba unakuwa  na  vipengele muhimu na  vya  kisheria  vya  kukulinda  wewe na  mali  yako.
Moja  ya  kipengele  muhimu  ni kueleza  wazi  ikiwa  atashindwa  kulipa  deni  huko  alikokopa  ni  kitu  gani   kitakulinda  ili  mali  yako  isiuzwe   au  hata  ikiuzwa  wewe  utapata  nini  kutoka  kwake  kufidia  hiyo  hasara.

4.   MADHARA.      

Madhara  makubwa  unayoweza  kupata  ni  pale   atakaposhindwa  kulipa  mkopo.  Hapa  bila  huruma nyumba/shamba  lako  litauzwa   na hautakuwa  na  chochote  cha  kukulinda  kama  mdhamini.  Wengi  imewatokea hii  na  aidha  wamekubali  mali  zao  ziuzwe  au  wamelazimika  kumlipia  mtu  deni  ili  kuokoa  mali  zao.

Pia  mara  nyingi  watu  wanaokopea  mali  za  watu   wana  tabia  ya kukimbia/kupotea au  kuwa  wajeuri  pale   wanaposhindwa   au  kuyumba  katika  marejesho.  Na wanakimbia  wakiwa  huru  kabisa   wakijua   kinachofuata  ni  kuuza  mali  ambayo  kimsingi  anajua sio  ya  kwake  na  hivyo  hana  la kupoteza.

Wewe  usiingie  katika  majaribu  haya  weka mpangilio  mzuri  wa  kisheria  ikiwa  utaamua  kumdhamini  mtu.

5.     UWEZO  WA  KUZUIA   MALI  YAKO  ISIUZWE.           

Ikiwa  ulimdhamini  mtu  na ameshindwa  kulipa  na  sasa   wakopeshaji  wanataka kuuza  mali   unaweza  kwenda  mahakamani  kuzuia uuzaji.   Lakini  utawezaje  na  hali  uliusaini   mkataba  wa  rehani( mortgage  deed).  Niseme  tu  utaweza  iwapo  tu  una  sababu  za  msingi   na  za  kisheria  na  sehemu  ya  kusimamia( Locus  stand).

Aidha  suala  la  msingi  kuliko  yote  ni kujihadhari  sana  na  mpango  huu  wa  kudhamini  kwa   kutumia  mali  yako  kukopea. Yawezekana  nawe  unataraji  kutengeneza  faida  kupitia  hilo,  ni  jambo  zuri  ila  hakikisha  unaweka  misingi  mizuri  ya  kukulinda wewe na  mali  yako.
MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MWANDISHI  WA MAKALA  YA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI   LA  JAMHURI   KILA   JUMANNE..   0784482959,  0714047241bashiryakub@ymail.com

  

1 comments:

  • Nsolo S. Stephen says:
    26 January 2017 at 20:06

    Ni kweli wengi wamepoteza mali zao hata hivyo mikataba 3 iliyotajwa haitumiki huko vijijini wala hatua zilizotajwa hazifuatwi.

Post a Comment