Sunday, 23 October 2016

NANI ANASTAHILI KIPAUMBELE KUSIMAMIA MIRATHI KATI YA WARITHI WA MAREHEMU.


Image result for MSIBANI
NA  BASHIR  YAKUB - 

Ni vema  kujua nani  anapaswa  kupewa  kipaumbele  cha  kusimamia  mirathi  pale   mwenye  mali  anapokuwa  ameaga  dunia. Mara  kadhaa  mjadala  huibuka   baina  ya  wanafamilia  hasa  pale  inapotokea  kuwa  marehemu  alikuwa  na  mke  zaidi  ya  mmoja  na  kila  upande  kuna  watoto.

Lakini  pia  hata  pale  marehemu  anapokuwa  na  mke  mmoja  mjadala  huu  napo  waweza  kuibuka  kati  ya  wanaotegemewa  kurithi  juu  ya  nani  awe  msimamia  mirathi. Hii  si  pale  tu  anapokufa  baba  lakini  pia  hata  panapo mswiba wa mama mjadala huu huibuka.

1.WOSIA  KUTAJA  MSIMAMIA  MIRATHI.

Ikiwa  marehemu  ameacha  wosia  na  katika  wosia  huo  imeelezwa  wazi  nani  atakuwa  msimamizi wa  mirathi  basi  huyo  aliyetajwa  ndiye  atakuwa  msimamizi  wa  mirathi . Wosia  unaweza kumtaja  mtu  mmoja kusimamia  mirathi  au  zaidi  ya  mtu  mmoja. Kwa  vyovyote  utakavyotaja   hao  waliotajwa  ndio  watasimamia  mirathi.

2.  WOSIA  KUTOTAJA  MSIMAMIA  MIRATHI.

Si  wakati  wote  wosia hutaja  msimamia  mirathi.  Hii  yaweza  kutokea  kwa  kutokujua  kwa  aliyeandika wosia   au  kujua  lakini  kuacha  makusudi  kwasababu  nzuri  anazozijua  mwenyewe.  Kwa  namna  yoyote  itakavyokuwa  wosia  usipotaja nani   asimamie  mirathi  basi   ni  wajibu  wa  wanafamilia  kuhakikisha  anapatikana    msimamizi ili  agawe  mali kutokana  na  wosia  unavyoeleza.

Muhimu  ni  kuwa  ni  lazima  apatikane  msimamizi   wa  mirathi.  Aweza  kuwa  mmoja  au  zaidi. Swali  kwetu  ni  ikiwa  kumetokea mgogoro  kuhusu  nani  asimamie  mirathi  je  nani  afaa zaidi  kuliko wenzake  kupewa  kipaumbele  kwa  mujibu  wa  sheria.

3.NANI APEWE KIPAUMBELE  CHA KUSIMAMIA  MIRATHI  KATI  YA  WARITHI   WA  MAREHEMU.

Sura  ya  352  ya  sheria  ya  usimamizi  mirathi  ndiyo  huongoza  jambo  hili.  Ikumbukwe  tumesema  hapo  juu  kuwa  suala  la  nani apewe  kipaumbele  cha  kusimamia  mirathi  linaibuka  pale  tu  ambapo  marehemu  hakuacha  wosia  kabisa  au  ameacha  wosia  lakini  ndani  mwake  hakumtaja  msimamizi  wa  mirathi.

4. KIPAUMBELE.
Kwanza  kabisa  anayestahili   kupewa  kipaumbele  ni  yule  ambaye  kwa  sheria itakayotumika  kugawa  mirathi  alistahili   kuchukua  mali  yote. Mirathi  hugawiwa  kwa  sheria  tatu  tofauti kutegemea  na  maisha  aliyoishi  marehemu.  Sheria  ya  kiislam  kama  aliishi  kiislamu, sheria  ya  kimila kama  aliishi  kimila  na sheria  ya  bunge  kwa  aliyeishi kikristo.

Kwahiyo  ikiwa  sheria  mojawapo  kati  ya  hizi  inatakiwa itumike  kugawa  mali  basi  itaangaliwa  nani  anastahili  kupata  mali  yote  kwa  mujibu  wa  sheria  hiyo  na  huyo   ndiye  atapewa  kipaumbele  kusimamia  mirathi. Habari  ya  kupewa  mali  yote  hujitokeza  hasa  pale  inapotokea  kuwa  mtu mmoja  tu  ndiye  mwenye  sifa  ya  kuwa  mrithi  halali.

Kipaumbele  cha  pili  atapewa  yule  ambaye  anastahili  kupata  mali  nyingi  zaidi  kuliko  wenzake  kutokana  na sheria  iliyotumika  kugawa  mirathi. Na  halikadhalika  vipaumbele  vitakwenda  hivyo  kwa  kutegemea  nani  anastahili  kupata  zaidi  kuliko  mwenzake.

Ikiwa  wanaogombea  wote  wanastahili  mgao  sawa  kwa  mujibu  wa  sheria  inayotumika kugawa  basi   hao wote wanaweza kuteuliwa  kusimamia  mirathi   isipokuwa  tu  wasizidi  wanne.

Ikiwa  warithi  halali  kama  walivyotajwa  hapo  juu  hawapo   basi  mdeni  anaweza  kuteuliwa  kusimamia  mirathi.  Na  kama  mdeni  hakuna  na  hakuna  mwingine  yoyote  mwenye  maslahi  katika  mali  za  marehemu  basi  mali  zaweza  kukabidhiwa  kwa  kabidhi  wasia  mkuu.

5. SIFA  YA  UADILIFU  KATIKA  KUSIMAMIA  MIRATHI.

Pamoja  na  kuwapo suala la  kipaumbele  katika  nani asimamie mirathi  ifahamike  kuwa mhusika  hatapewa  nafasi  hiyo  ikiwa tu  itathibika  kuwa hana  sifa  ya  uadilifu. Sifa  ya  uadilifu  ndio  kila  kitu  katika  kusimamia  mirathi. Haya  yote  ni  kwa  mujibu wa  sheria  ya  usimamizi  mirathi  sura  ya  352  kifungu  cha  33 (1), (2), (3), na (4).

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MWANDISHI  WA MAKALA YA SHERIA KUPITIA GAZETI  LA JAMHURI KILA JUMANNE..   0784482959,  0714047241bashiryakub@ymail.com0 comments:

Post a Comment