Thursday, 29 September 2016

NAMNA YA KURASIMISHA BIASHARA YAKO ILI UKOPESHEKE.NA  BASHIR  YAKUB -

Kurasimisha  biashara  kunazo  namna  nyingi.  Kufungua  kampuni   ni  moja  ya  namna  ya  kurasimisha  biashara. Kusajili  jina  la  biashara  nayo  ni  namna nyingine  ya  kurasimisha  biashara. Makala  yatazungumzia  hii  ya  pili  ya  kusajili  jina  la  biashara. Na  hii  ni  kwasababu  hii  ni  njia  nyepesi,  ya  haraka, na  ya gharama  ndogo  sana.

Mfano  wa jina  la biashara  ni kama,   HK  bazaar, kinondoni  investment, Congo traders, Karoli  LTD  na  mengine  yanayofanana  na  hayo.

1.NINI  MAANA YA  JINA  LA  BIASHARA.

Jina  la  biashara  ni  lile  jina  linalotumiwa  na  mtu  kama  jina  la  utambulisho  wa  biashara  yake  inayofanywa  katika  mfumo  ambao  sio  kampuni.  Makampuni  yana  majina  lakini  majina  hayo  hayawezi  kuitwa  majina  ya  biashara  bali  ni  majina  ya  kampuni.

Jina  la  biashara  ni  kwa  yule  ambaye  biashara  yake  imesajiliwa   lakini  sio  kampuni. 

Aidha mwenye  biashara  ambayo  haijasajiliwa  lakini  analo  jina  fulani  analotumia kisheria  huyo  hana  jina  la  biashara.Hilo  jina  sio  lake  na  mtu  mwingine  anaweza  kulisajili na  akamtaka  huyu  ambaye  hajalisajili  kuacha mara  moja  kulitumia .

Ili  sheria  ikutambue  kuwa  una  jina  la  biashara   ni  pale  tu  unapokuwa   umesajili  jina  hilo. 

2. WAPI  WAWEZA  KUSAJILI  JINA  LA  BIASHARA.

Jina  la  biashara  husajiliwa  kwa  msajili  wa  biashara  na  makampuni ( BRELA). Ukifika   hapo  utawaeleza  kuwa  unataka  kusajili  jina  la biashara  watakupa  fomu  maalum  utaijaza .  Lakini  kabla  ya  hapo  utatakiwa   utume  maombi  maalum  hapohapo BRELA ukitaka  kujua  iwapo  jina  ulilochagua  kuwa  la  biashara   yupo  mtu  mwingine  analitumia au  lah.

Hii  ni  kwasababu  jina  ni  moja  Tanzania  nzima.  Hakuwezi  kuwa  na  majina  mawili  au  zaidi   yanayofanana  huku  yote  yakiwa  yamesajiliwa.

3. ADA  YA  USAJILI  NI  KIASI  GANI.

Ada  ya  usajili  wa  jina  sio  kubwa.  Mara  ya  mwisho   mwaka  2015   ilikuwa   Tshs 6,000/= ( alfu  sita  tu).  Kwahiyo  ni  rahisi  sana na  hata  kama  imepanda  bila  shaka  haiwezi  kuzidi  alfu  ishirini.

4.  KUPATA  NAMBA  YA  MLIPA  KODI.

Katika  kurasimisha  biashara   kupata  namba  ya  mlipa  kodi  TIN  NUMBER  ni  hatua  ya  muhimu   sana.  Karibia  kila  ofisi  ya  TRA pote  hata  mikoani  hutoa namba  hizi. Wanazo  taratibu  ikiwa  ni  pamoja na  kuleta barua  kutoka  serikali  za  mitaa  kwa  anayehitaji  kupata  namba  hiyo. Kwahiyo  ni  lazima  pia  upate  namba  hii.

5. KUPATA  LESENI  YA  BIASHARA.

Ukiwa  tayari  umesajili  jina  na  umepata  nambari  ya  mlipa  kodi  basi  hatua  inayofuata  ni  kutafuta  leseni  ya  biashara.  Leseni  hizi  hupatikana  manispaa.  Kila  manispaa  ina  utaratibu  wa  kutoa  leseni . Viambatanisho  utakavyotakiwa  kuwa  navyo  ni pamoja  na  ushahidi  kuwa  unayo  namba  ya  mlipa  kodi.

6. FAIDA  ZA KURASIMISHA  BIASHARA.

Moja  ni  kuwa  unaweza  kukopesheka  katika  taasisi  za fedha. Lakini pia   hata  zile  fedha  zinazotolewa  na  serikali kwenye  halmashauri  kwa  ajili  ya  wajasiriamali unaweza  kuomba na  ukapewa. Si  rahisi  kupata  fedha  hizi  kama  hujarasimisha  biashara  kisheria.

Pili  ni kinga ya  biashara  zako  kwakuwa   unaweza  kupata  bima ya  majanga  kama  moto, nk pale tu unapokuwa  umerasimisha. Sio  rahisi  kupata  bima  ya  biashara ikiwa  hujarasimisha.

Tatu  unaondoka  katika  kufanya  biashara  kienyeji   na  kuanza  kufanya  biashara  kisasa na  katika  mfumo rasmi bila kujali udogo wa  biashara zako.  
Hizi  ni baadhi  tu  lakini  faida  ni  nyingi mno.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MWANDISHI  WA MAKALA YA SHERIA KUPITIA GAZETI  LA JAMHURI KILA JUMANNE..   0784482959,  0714047241bashiryakub@ymail.com


0 comments:

Post a Comment