Tuesday, 2 August 2016

UNAELEWA NINI KUHUSU KUUA BILA KUKUSUDIA ?.

Image result for manslaughter


NA  BASHIR  YAKUB -

Tumekuwa  tukisikia   fulani  amepatikana  na  hatia  ya  kuua  bila  kukusudia  au  fulani  ameua  bila  kukusudia,  je  unajua  nini  maana  ya  kuua  bila  kukusudia  kisheria. Mara  ya mwisho  neno  kuua  bila  kukusudia  limesemwa sana baada ya  hukumu katika kesi  iliyohusu kifo cha mwanahabari  Daudi  Mwangosi.  Yapo  mengi  ya  kujua  kuhusu  kuua  bila  kukusudia.

Kifungu  cha  195,sura ya 16, Kanuni  za  adhabu ndicho  huzungumzia  kuua  bila  kukusudia.

1.NINI  MAANA  YA  KUUA  BILA  KUKUSUDIA.

Katika  sheria  kuua  bila  kukusudia  (manslaughter)  kunatofautishwa  na  kuua  kwa  kukusudia(murder). Kuua  bila  kukusudia  ni  kuua ambako  muuaji   anatenda  kitendo  kinachopelekea  kifo  lakini hakuwa na  nia,dhamira au  lengo  la  kusababisha mtu afe.

Wakati  kuua  kwa  kukusudia  ni  pale  mtu  anapotenda  tendo   ambalo  linapelekea  mauaji  ya  mtu   lakini  amefanya  hivyo  akiwa  amedhamiria   kuua.  Kwahiyo  haraka  utaona  kuwa  tofauti  kubwa  ya  kuua kwa  kukusudia  na  ile  ya  kuua  bila  kukusudia  ni  dhamira, nia au  lengo.

Dhamira,nia au lengo  likiwa ni kuua,  basi huko  ndiko  kuua  kwa  kukusudia. Na dhamira,nia au lengo  likiwa sio kuua lakini  bahati  mbaya  mtu  akafa  basi  hiyo  itakuwa  ndio  kuua bila kukusudia.

2. UTAJUAJE   HUYU  ALIUA  KWA  KUKUSUDIA  NA  HUYU  HAKUKUSUDIA.

Yapo  mambo    ambayo  hutizamwa  na  mahakama ili kujua  iwapo  kulikuwa  na  dhamira  ya  kuua  au haikuwepo.  Moja  ya  jambo kubwa  ambalo  huangaliwa  ni   mazingira  kabla  ya  tukio, mazingira  wakati  wa  tukio  na  baada  ya  tukio.
Kwa  mfano  A alimkashifu B kwa matusi  mabaya .  B akakasirika  sana . Baadae  B  akaenda  kwake  akaja na panga  ambalo  alilitumia  kumuua  A .  Hapa  B  atakuwa  ameua  kwa  kukusudia  kwasababu   alisafiri  kutoka eneo la tukio , akatembea  mpaka  nyumbani  kwake, akatafuta  panga,  akaanza  safari  ya  kurudi,  akamtafuta  tena  A,  akampata  ndipo  akamuua.  Hatua  zote  hizi   za kwenda,kurudi nk. zinathibitisha  dhamira, nia  au  lengo. Hakuna  bahati  mbaya inayopitia  hatua  hizi  zote.

Lakini  ingekuwa  palepale  baada  ya  kukashifiwa  kwa  hasira   akampiga  na  kumuua,  ingekuwa  kuua  bila  kukusudia kulikotokana na  joto  la  hasira(heat  of  passion).

Kwahiyo  ushahidi wa mazingira ya tukio kama  hayo ndio utaifanya  mahakama  iamue  kama  mtuhumiwa  ameua  kwa  kukusudia   au  hakukusudia.

Upande  unaosema  aliua  bila  kukusudia  utaleta  ushahidi  kuonesha  mazingira  ya  tukio  na  upande unaosema  alikusudia  nao  utaleta  ushahidi  kuonesha mazingira  ya  kusudi, nia au  dhamira.

3.  AINA  MBILI  ZA  KUUA  BILA  KUKUSUDIA.

Kwanza  ni  kuua  bila  kukusudia  lakini  kwa  tendo  linalotokana  na hiari(voluntary manslaughter). Hii  ni  pale  ambapo  ni  kweli  kuwa  fulani  alidhamiria  kumpiga  fulani au  alimsukuma  lakini  hakutaka afe.  Kwa  mfano  mzazi   anamchapa  mwanae  kwa  kosa  fulani  lakini   katika  kumchapa mtoto  anakufa.  Au  askari  anapiga  bomu  la  machozi  ili  watu  wakimbie   lakini  katika  kufanya  hivyo  bomu  linampata  raia  na  kumuua.Hii ni aina  ya  kwanza  ya kuua  bila  kukusudia.

Aina ya pili ni kuua  bila  kukusudia  kwa  tendo  ambalo  si  la  hiari( involuntary  manslaughter). Kwa mfano  breki  za  gari  zinakatika  na  gari  inamuua  mtu. Au  bunduki  imeshikwa  vibaya  inajifyatua  na kuua  mtu. 

Ni  matendo  ya  uzembe  lakini  hayakutokana na hiari kama  ilivyo hiari kuamua kumchapa mwanao.
Aina hizi  zote  mbili  ni za kuua  bila  kukusudia.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MWANDISHI   WA  MAKALA  YA SHERIA  KUPITIA  GAZETI   LA  JAMHURI  KILA  JUMANNE..   0784482959,  0714047241  bashiryakub@ymail.com

0 comments:

Post a Comment