Monday 1 August 2016

MTU HATACHUKULIWA KUWA AMEUA BAADA YA MWAKA MMOJA NA SIKU MOJA.

Image result for KUSABABISHA  KIFO

NA  BASHIR  YAKUB - 

Mtu akimuumiza mwingine na  aliyeumizwa  akapata  jeraha  linalosababisha  alazwe  hospitali  au  asilazwe   lakini  aendelee  kuishi  na  jeraha  lake  hilo, Swali litakuwa  je  mtu  huyo  akifa  baada  ya  miezi  sita,  saba ,  kumi  au  zaidi   tokea  siku  alipoumizwa   kifo  chake  kitakuwa  kimesababishwa  na  yule  aliyemuumiza ?.

1.NINI  MAANA  YA  KUSABABISHA  KIFO.

Kusababisha  kifo   kunaweza  kuelezwa   katika  namna  nne  tofauti.  Na  hii  ni kwa  mujjibu  wa  Sura  ya 16, kifungu   cha  203, Kanuni  za  adhabu.

( I ) Mtu  amemtia  jeraha  mtu  mwingine.  Na  kutokana  na  jeraha  hilo  mtu  huyo  anakufa.  Haijalishi  amekufa  akiwa  anapata  matibabu  au  laah.  Na  haijalishi  kama  matibabu  hayo  yalikosewa  au  laah. La  msingi  ni  kuwa  matibabu  hayo  yalifanywa  kwa nia   njema na  hiyo  yatosha  kusema fulani  aliyesababisha  jeraha ndiye  huyohuyo  aliyesababisha kifo.

( ii ) Pengine  ni  pale ambapo  mtu  anamlazimisha  mtu  mwingine  kwa  kumtishia  akimtaka  atende  tendo   ambalo   linasababisha  kifo  cha  mtu  mwingine.  Mtu  huyo  aliyetishia  atahesabika  kusababisha  kifo.  

(iii) Zaidi,  kutotekeleza  wajibu  ambako  kunapelekea  kifo  nako  ni kusababisha  kifo.  Kwa  mfano   daktari  aliyetakiwa  kumpokea  mgonjwa  na  kumtibia akishindwa  kufanya  hivyo  na  mgonjwa  akafa  basi  atakuwa  amesababisha  kifo.

( iv) Pia  ikiwa  mtu  ana jeraha   au  ugonjwa  ambao  kwa  vyovyote  vile  ungemsababishia  kifo  lakini  akatokea  mtu  mwingine  akatenda  tendo  ambalo  linasababisha  mgonjwa  afe  haraka  basi    mtu  huyo  aliyetenda  anahesabika  kusababisha  kifo.

2.KUTOCHUKULIWA  KUUA  BAADA  YA  MWAKA  NA  SIKU.

Kifungu cha  205 ( 1 ) kanuni  za  adhabu  kinasema  kuwa  mtu  hatachukuliwa  kuwa  amemuua  mtu  mwingine  kama  kifo   hakitatokea  ndani  ya  mwaka mmoja  na  siku  moja  tangu  siku  ya  sababu  ya  kifo.

Maana  yake  ni  kuwa  iwapo  mtu  atamsababishia mtu  mwingine   jeraha  au  maumivu  yoyote , na  kutokana  na  jeraha  hilo  au  maumivu  hayo  mtu  akafa   ndani  ya  mwaka  mmoja  na  siku  moja   tangu  siku  aliposababishiwa  madhara  hayo,  basi  yule  aliyesababisha  madhara  atahesabika  kusababisha  kifo.

Ikiwa  atakufa  baada  ya  mwaka   na  siku  moja  basi   yule  aliyeumiza   au  kujeruhi  hawezi  kuhesabika    kama  amesababisha  kifo.

3. KUHESABIKA  KWA  MUDA.

Kawaida  muda  huanza  kuhesabika  mara   tu  tendo   lililosababisha  kifo  linapotendeka.   Kuna  siku tendo  lilipotendeka  halafu   kuna  siku  tendo  lilipoacha  kutendeka.  Siku  tendo  lilipotendeka  ni  kwa  mfano siku   mtu  alipopigwa  au  siku  aliyoumizwa. 

Wakati  siku  tendo  lilipoacha  kutendeka   ni  kwa mfano  siku  daktari  alipoacha  kumpa  matibabu  mgonjwa,  au  siku  fulani  alipoacha  kumpa  fulani  chakula   na  hivyo  kupelekea  kifo  chake.  Ni  kuanzia  siku  hiyo  ambapo  muda  huhesabika  hadi  mwaka  na  siku  moja.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MWANDISHI   WA  MAKALA  YA SHERIA  KUPITIA  GAZETI   LA  JAMHURI  KILA  JUMANNE..   0784482959,  0714047241  bshiryakub@ymail.com

0 comments:

Post a Comment