Tuesday, 26 July 2016

HAKI YA KUKATAA KUPOKEA MZIGO IKIWA HAUFANANI NA ULIOAGIZA.


NA  BASHIR  YAKUB - Image result for MELI YA MAKONTENA

Sheria  ya  uuzaji  wa  bidhaa sura ya 214  ni  sheria  inayoeleza  na  kuchanganua  miamala  ya  biashara  kwa  ujumla  wake.  Inaeleza  mikataba  ya  biashara, aina  zake,  watu  wanaostahili kuingia  mikataba  hiyo, biashara  halali  na  haramu, usafirishaji  wa  bidhaa  halikadhalika  kupokea,kuharibika na kupotea kwa bidhaa.

Kutokana  na  kukua  kwa  biashara  na  kuongezeka  kwa  uagizaji  wa  bidhaa  hasa  kutoka  nje ya  nchi  au  nje ya  mikoa  kupitia  mitandao  au  vinginevyo makala yataeleza   baadhi  ya  kanuni  za kisheria za kuagiza  na  kupokea  mizigo  ambazo zitamsaidia  mfanyabiashara na hata mlaji.

1.HASARA  NI  YA  NANI MZIGO  UKIPOTEA   AU  KUHARIBIWA   WAKATI  WA  KUSAFIRISHA.

Kifungu  cha  34( 2 )  kinasema  kuwa  ikiwa  jukumu  la  kusafirisha  mzigo/bidhaa  ni  la  muuzaji  basi  muuzaji  ndiye  atakayetakiwa  kuingia  mkataba  wa usafirishaji  mzigo   kati  yake  na  msafirishaji(transporter).  

Kifungu  kinaendelea  kusema  kuwa  ikiwa  mzigo  utapotea  wakati  ukiwa  njiani  au  kuharibika   kwa  namna  yoyote  basi  muuzaji   ndiye atakewajibika  na  upotevu  au  uharibifu  na  mnunuzi  anaweza  kukataaa  kupokea  mzigo  ulioharibika au  akakubali  kupokea lakini  akataka  kulipwa  fidia. Ikiwa  umepotea  kabisa atahitaji  kurudishiwa  hela  yake.

2.USIKUBALI KUPOKEA  MZIGO/ BIDHAA  AMBAYO HAIJATIMIA .

Kifungu  cha  32(1)  cha  Sheria  ya  uuzaji  bidhaa  kinasema  kuwa ikiwa muuzaji  atapeleka mzigo/bidhaa  ambayo  haijatimia  basi  mnunuzi  anaweza  kukataa  kupokea  mzigo huo.

Lakini  ikiwa  atakubali  kupokea  mzigo  huo  ambao  haujatimia  basi  atatakiwa  kulipa  pesa  ileile  iliyo  kwenye  mkataba  bila  kukata  au  kupunguza  hela  kufidia  bidhaa  ambayo  haijaletwa.

Kwahiyo  ukikubali tu  kupokea  mzigo  ambao  haujatimia  huwezi  tena  kusema  napunguza  na  hela.  Ukipokea  tu sheria  inasema unatakiwa kulipia  hela  yote  mliyokuwa  mmekubaliana. Hivyo basi kama  hauko  tayari  kulipa  hela  yote  basi  lililo  bora  kwako  ni  kutopokea  kabisa mzigo huo.

3. KUPOKEA BIDHAA/ MZIGO  ULIOZIDI  IDADI  MLIYOKUBALIANA.

Kifungu  cha  32(2)  kinasema  kuwa  pale  ambapo  muuzaji  atapeleka   kwa  mnunuzi  mzigo  ambao  umezidi  ile  idadi  waliyokubaliana  kwenye  mkataba   basi  mnunuzi  anaweza  kukataa  kupokea  mzigo   wote  au  sehemu  iliyozidi.  Lakini  pia  ikiwa  atakubali  kupokea  mzigo  wote  basi  atatakiwa  kulipa  pesa  kwa  kiwango  kile kile  walichokubaliana.

Hatakuwa  na wajibu  wa  kuongeza  pesa  ati  kwasababu  mzigo  nao  umeongezeka.  Hasara  itakuwa  kwa  muuzaji aliyezidisha.

4. MAKUBALIANO  YA KUPOKEA  MZIGO KWA  MAFUNGU(INSTALMENT).

Kifungu  cha  33  kinakubali   makubaliano  ya  kupokea  mzigo/bidhaa   kwa  mafungu(instalment).  Lakini  kimeweka  msisitizo  katika muda  na malipo  kufanyika  kama  makubaliano  yalivyo.  Ikiwa bidhaa  haitaletwa  kwa  muda  uliokubaliwa  basi  mnunuzi  anaweza  kudai  fidia  au  vinginevyo.

5. NI  MUHIMU  KUKUBALIANA  NANI  ATABEBA  HATIA( RISK).

Mara  zote  unapofanya  biashara   ambayo  inahusisha  kusafirisha  mzigo iwe kwa  barabara,garimoshi,ndege au meli ni  muhimu  sana  kukubaliana  katika  makubaliano  yenu  nani  atabeba  hatia  ikiwa  litatokea  tatizo.  

Hakikisha  mnaandika  kabisa  kwenye  makubaliano  yenu  kuwa  kwa  hatari  yoyote( risk) mhusika fulani  ndiye  atawajibika  kulipia.

Kama  ni  bidhaa  unaagiza kutoka nje  angalia  katika  maelezo  yao  kama  kuna  habari  ya  bima au  maelezo  yanayoeleza  nani  mbeba  hatia(risk) panapo  hatari. Kama  haipo  ni  wajibu  wako kuwezesha iwekwe.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MWANDISHI   WA  MAKALA  YA SHERIA  KUPITIA  GAZETI   LA  JAMHURI  KILA  JUMANNE..   0784482959,  0714047241  bashiryakub@ymail.com



0 comments:

Post a Comment