NA BASHIR YAKUB -
Mara kadhaa linapoibuka suala la kugawana mali pale ndoa inapohesabika kushindikana masuala kadhaa ya msingi na yanayohitaji uelewa huwa yanaibuka.
Moja ya suala kati ya masuala ambayo huibuka ni hili la kutenganisha na kufafanua hadhi ya mali za wanandoa ili mgawanyo uweze kufanyika kwa haki. Yawezekana mwanandoa akadhani ana haki katika mali fulani lakini kumbe kisheria hana haki hiyo ni mtazamo wake ndio unamsukuma kuamini hivyo.
Halikadhalika yawezekana mwanandoa kudhani hana haki katika mali fulani kumbe anayo haki. Ili kujua una haki ipi katika mali ipi na huna haki katika mali ipi yahitajika kujua misingi ya kisheria inayotumika kugawanya mali za wanandoa.
1.KUGAWANA MALI ZA WANANDOA.
Ieleweke kuwa tunapoongelea wanandoa kugawana mali tunaongelea talaka. Hakuna kugawana mali bila talaka. Na kisheria talaka inapotoka tu swali linalofuata ni habari ya mali na watoto kama wapo. Mali si lazima magari na manyumba lakini pia hata vyombo vya ndani vikiwemo vitanda, makabati, sahani n,k nazo ni mali kwa mujibu wa sheria. Navyo huhitaji mgao.
2. JE KUGAWANA MALI NI NUSU KWA NUSU ?.
Linapokuja suala la kugawana mali wengi hudhani mtindo unaotumika kugawa ni ule wa nusu kwa nusu. Jambo hili si kweli kwakuwa sheria ya ndoa 1971 iliyofanyiwa marekebisho 2002 haisemi kuwa utaratibu wa kugawana mali ni nusu kwa nusu. Sheria hii imeweka msingi mkuu wa kugawana mali ambao ndio hutumika katika mahakama zetu katika kutoa maagizo ya kugawa mali za wanandoa.
Msingi uliowekwa na sheria ni msingi wa kiwango cha mchango wa mwanandoa katika kupatikana kwa mali husika. Kiwango alichochangia mwanandoa katika kupatikana kwa mali hiyo ndicho kitakachokadiriwa na kiwango hicho ndicho atakachopewa.
Kwa hiyo kama ni nyumba ya vyumba sita mmoja anaweza kupata chumba kimoja na mwingine akapata vitano kutegemea na mchango wake.
Na mchango hapa sio leta ni lete. Mchango sio hela tu hata kazi za nyumbani anazofanya mama wa nyumbani ambaye haleti hela nazo huitwa mchango ambapo hukadiriwa na kupata kile anachostahili.
3. MALI KABLA YA NDOA NA BAADA YA NDOA.
Katika kutenganisha mali za wanandoa huwa zinatenganishwa katika makundi makuu matatu. Kwanza kuna mali ambazo mtu alikuwa nazo kabla ya ndoa na wakati anaingia katika ndoa ameingia nazo. Kwa mfano mwanamke ameolewa akamkuta mwanaume tayari ana nyumba yake. Pili kuna mali ambazo zimepatikama wakati wawili wakiwa katika ndoa . Kwa mfano ndoa imefungwa wawili wakaanza kuishi pamoja na taratibu wakaanza kujenga na kukamilisha.
Na tatu ni mali ambazo zimepatikana katika ndoa lakini zikiwa hazina uhusiano wowote wa kindoa kwa mfano kurithi au kuzawadiwa mali. Tutaona hapa chini mazingatio ya sheria ya kila moja katika haya.
4. JE MALI ILIYOPATIKANA KABLA YA NDOA INAHESABIKA NI YA FAMILIA.
Mali iliyopatikana kabla ya ndoa na ikaendelea kuwepo kipindi cha ndoa inaendelea kuwa ya huyo mwenye nayo bila ushirika wa mwenza wake. Kama ni nyumba mwanamke alikuwa nayo kabla ya kuolewa au ni mwanaume alikuwa nayo kabla ya kuoa basi inaendelea kuwa ya kwake peke yake na haihusiki katika mgao suala la mgao linapojitokeza.
Hata hivyo inaweza kuingizwa katika mgao ikiwa kuna mchango wowote wa kuiendeleza uliotolewa na mwenza. Kwa mfano kabla ya ndoa ilikuwa na vyumba viwili lakini katika kipindi cha ndoa imepanuliwa na kufikia vyumba vitano, au ilikuwa haina uzio, au haina madirisha kabla ya ndoa lakini baadae vitu hivi vikawepo.
Katika hali kama hiyo itatakiwa iingizwe katika mgao na kutazama kiwango cha mchango wa kila mmoja katika uendelezaji huo. Ni hapo ambapo mchanganuo utafanyika ili kila mmoja apate haki kutokana na kiwango cha mchango wake.
Ikiwa hakuna uendelezaji wowote uliofanyika katika mali yaani labda nyumba ilivyokuwa kabla ya ndoa ndivyo hivyohivyo ilivyoendelea kubaki hata baada ya ndoa basi mali hiyo haitatakiwa kuingizwa katika mali za mgao bali itabaki mali ya mwanandoa mmoja pekee ambaye ndiye mmiliki wa tangu awali.
Hali ni hiyo hiyo hata kwa mali ambayo imepatikana katika ndoa lakini ikiwa haina uhusiano na kipato cha wanandoa, kwa mfano mali ya urithi au zawadi. Hii ina maana ikiwa mali hii itaendelezwa basi mchango wa uendelezaji utatathiminiwa na ikiwa haitaendelezwa basi itabaki mali ya mrithi au mpewa zawadi pekee na haitahusu mgao.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MWANDISHI
WA MAKALA YA
SHERIA KUPITIA GAZETI LA JAMHURI
KILA JUMANNE.
”. 0784482959, 0714047241
bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment