NA BASHIR YAKUB -
Mara nyingi nimeandika kuhusu ardhi hususan viwanja na nyumba. Katika kufanya hivyo mara kadhaa nimejaribu kuwatahadharisha watu namna mbalimbali ya kisheria ya kuepuka kuingia katika migogoro ya viwanja na nyumba hasa wakati wa kununua( wanunuzi).
Nimewahi kueleza namna au vitu vya msingi ambavyo hutakiwa kuwa katika mkataba wa ununuzi wa nyumba au kiwanja.
Nikaeleza umuhimu wa kila kimoja na nikasisitiza kuwa atayekuwa amenunua ardhi na mkataba wake ukajaaliwa kuwa na vitu hivyo basi si tu atakuwa amefanya manunuzi bora lakini pia atakuwa amefanya manunuzi yanayokubalika kisheria.
Ifike hatua watu waelewe kuwa migogoro mingi ya ardhi huanzia na kutokuwa makini kwenye manunuzi. Kutokupata ushauri wa kisheria ikiwa ni pamoja na kutopitia hatua za msingi za kisheria kabla ya manunuzi, kuandikiwa mikataba ya manunuzi isiyokidhi vigezo vya kisheria ikiwemo ile ya serikali za mitaa ambayo hairuhusiwi kabisa kisheria ni kati ya sababu chache kati ya nyingi zitakazokupelekea uingie katika mgogoro.
Leo nitaeleza hatua moja ya msingi sana ambayo hutakiwi ufanye manunuzi ya ardhi bila kuipitia.
1.HATUA TANO ZA KUFUATA UNUNUAPO NYUMBA/KIWANJA.
Ziko hatua tano muhimu za kupitia pale unapo kuwa katika mchakato wa kununua ardhi. Umuhimu wa hatua hizi ni kuwa kwanza kabisa si rahisi kujikuta katika mgogoro unapokuwa umezipitia.
Lakini pili hata bahati mbaya utokee mgogoro basi wewe uliyepitia hatua hizo utakuwa salama na kama ni kesi basi wewe upo katika mazingira mazuri ya kushinda.
Hatua ya kwanza huitwa hatua kabla ya mkataba( pre contractual stage).
Hatua hii inayo mambo yake ya msingi na ya kisheria ambayo kuyafuata kwako kwaweza kukuweka mbali na hatari ya kununua ardhi yenye mgogoro au itayokuingiza katika mgogoro .
Hatua hii ndiyo nitakayoeleza kama msingi wa makala ya leo kama tutakavyoona. Kabla ya kueleza hatua hiyo ni vema pia nikazitaja hatua nyingine japo kwa ufupi.
Hatua ya pili huitwa hatua ya mkataba( contractual stage). Hii ni hatua ya kupitia na kujiridhisha na mkataba wa manunuzi ikiwa ni pamoja na kuusaini.
Hatua ya tatu huitwa “pre completion stage”, hatua ya nne huitwa hatua ya kumalizia ( completion stage) na hatua ya tano na ya mwisho huitwa hatua baada ya kumalizia ( post completion stage).
2. USINUNUE NYUMBA/KIWANJA BILA KUPITIA HATUA HII.
Kama nilivyoeleza hapo juu hatua nitakayojadili hapa huitwa hatua kabla ya mkataba au “pre contractual stage”. Jambo kubwa ambalo huhusishwa katika hatua hii ni kufanya utafiti wa kitaalam uitwao “official search” .
Katika hatua hii mlengwa anayetaka kununua ardhi kupitia ofisi ya mwanasheria ataandika barua kwenda kwa msajili wa ardhi kumuuliza taarifa kamili za nyumba au kiwanja anachotaka kununua.
Msajili wa ardhi atapekua katika kumbukumbu zake rasmi na kutoa majibu sawa na kile kilicho katika kumbukumbu zake.
3. MAMBO MUHIMU UTAKAYOULIZA KWENYE BARUA YA MSAJILI.
Kwanza katika barua yako utahitaji kujua jina la mmiliki linalosomeka katika nyaraka za serikali. Hii itakusaidia kulinganisha jina la anayekuuzia na lile linasomeka katika kumbukumbu za serikali.
Kwa kujua jina tu utaepuka kununua ardhi kutoka kwa mtu ambaye si mmiliki halisi.
Pili utahitaji kujua iwapo ardhi hiyo imewekwa kama dhamana popote katika taasisi za fedha. Kama imewekwa dhamana basi taarifa zitaonesha. Hii ni kwasababu taasisi za fedha hutuma taarifa kwa msajili wa ardhi katika kila ardhi inayowekwa kwao kama dhamana.
Tatizo la kununua ardhi iliyowekwa dhamana bila kujua ni aidha ukubali kuingia hasara kulipa deni ili nyumba ubaki nayo au uwe mpole nyumba uliyonunua iuzwe upate hasara.
Tatu utaweza kujua iwapo ardhi hiyo ni ya wanandoa hasa iwapo wanandoa hao wana mgogoro. Hii ni kwasababu sheria humpa haki mwanandoa kuweka zuio katika ardhi ya familia iwapo mmoja wao ana wasiwasi mwenzake anaweza kuuza ardhi hiyo.
Kwahiyo ikiwa taarifa kama hizo tayari zimepelekwa ardhi basi utakapopitia hatua hii kabla ya kununua utaoneshwa taarifa hizo na hivyo kuepuka kununua mali ya familia kitu ambacho ni kama kupoteza.
Nisisitize kuwa hatua hii ni muhimu sana kwakuwa ni hatua pekee ya kujiridhisha na uhalali wa ardhi unayotaka kununua. Nathubutu kusema kuwa usinunue kiwanja/nyumba bila kupitia hatua hii.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MWANDISHI
WA MAKALA YA
SHERIA KUPITIA GAZETI LA JAMHURI
KILA JUMANNE.
”. 0784482959, 0714047241
bashiryakub@ymail.com
asante kwa ushauri na somo lenye manufaa. je nawezaje kupata kitabu cha sheria ya ardhi ?