Wednesday, 20 July 2016

JE UNAJUA KUTOFAUTISHA HATI NA OFA UNAPONUNUA NYUMBA/KIWANJA.


Image result for OFA  YA  KIWANJA

NA  BASHIR  YAKUB -

Mara  zote  muuzaji  hutoa  maelezo  yanayolenga  kuonesha   usahihi  wa  ubora  wa  kile  anachokiuza. Ni  muhali  sana muuzaji  kusema  lile  lililo  la  kweli  haswa.  Hali hii ndio  humlazimu  mnunuzi  kutafuta  utaalam  kwa  wanaojua  vizuri  kile  anachotaka  kununua.

Kumekuwa  na  malalamiko  yanayotokana  na  baadhi  ya  watu  kutojua  kutofautisha  hati  ya  nyumba/kiwanja  na  Ofa  ya  nyumba/kiwanja. Muuzaji  anamuuzia  mnunuzi  na  anamkabidhi  nyaraka za  ofa huku  akimwambia  kuwa  hii  ni  hati.
Wengine  husema  kweli kuwa  hii sio  hati  lakini hapohapo hulaghai  tena kuwa  ukishanunua  unapeleka  tu  hii  ofa  ardhi  basi  wanakubadilishia  na kukupa  hati. 

Mnunuzi  anaponunua  na  kuipeleka  ardhi  ili  apewe  hati  anakutana  na mambo tofauti  kabisa  na  alivyoelezwa na  hivyo  kulazimika  kuanza  upya mzunguko.
Hapa  tutajua  ukweli  ikiwa  anayekupa  nyaraka  ofa  ni  sawa  kama  kakupa  hati  au  laah.

1.OFA  NININI.

Ofa  ni  neno  la kiingereza “ offer” . Kiswahili  kizuri  kinachotumika   kumaanisha  Ofa  ni neno  “fomu  ya  ahadi”. Fomu  ya  ahadi(ofa)  ni  taarifa  ya  maandishi  inayotolewa  na  kamishna  wa  ardhi  kwenda  kwa  mwombaji  ikieleza  kuwa  ombi  lake  limekubaliwa  na  kumpa  masharti   yanayotakiwa.

Hapa  ni  mtu  anakuwa  akitafuta  hati  na  hivyo  anakuwa  ametuma  maombi  kwa  kamishna  wa ardhi.  Kamishna  anapokubali  maombi  yake  baada  ya  kuwa  yamepitia  idara  kadhaa  ndipo  kamishna  hutoa   fomu  ya ahadi  ( ofa) ambayo  kimsingi  huambatana  na masharti  kadhaa  yanayotakiwa   kutekelezwa.

2. KUWA  MAKINI  OFA  SIO  HATI.

Ofa  au  fomu  ya  ahadi  sio  hati  hata  kidogo.  Ofa  ni  hatua  ya  kuelekea  kupata  hati  lakini  mtu  anakuwa  hajapata  hati. Yafaa  unaponunua  ardhi  uwe  na  uwezo  wa  kutofautisha  vitu  hivi ili  usiwe mwenye kulaumu  baadaye. Na ni muhimu  kujua  kuwa  ofa  yaweza kufutwa  mda  wowote  na  kamishna  na  hivyo  ukajikuta  umekabidhiwa  ofa  ambayo   si  tu  haina  hadhi  ya  kuitwa hati  bali  pia   iliyokwishafutwa  na  kamishna  wa  ardhi.

3. IPI  TOFAUTI   YA  OFA NA  HATI .

Tofauti  ni  nyngi  ila  hapa  zitaelezwa  chache  tu.
a )Hati  ni  nyaraka  iliyokamilika  inayompa  mtu  umiliki  halali  na  kamili,  wakati  ofa  ni  hatua  tu  ya  kuelekea  kupata  hati  na  si  nyaraka  inayotoa  umiliki  kamili.

b ) Hati  ni  nyaraka  inayoweza  kutumika  kama  dhamana  kwenye taasisi  za fedha halikadhalika mahakamani,  wakati  ofa  haiwezi  kufanya  kazi  hizo.

c ) Umiliki  wa hati  hufutwa  na  rais  wakati  ofa  yaweza  kufutwa  na  kamishna  wa  ardhi.

4. JE  KUNA  TATIZO  KUNUNUA  ARDHI  YENYE  OFA.

Hapana,  hakuna  tatizo  isipokuwa  ni muhimu  ujue  tu  kuwa  nyaraka hizo  unazopewa  ni  za  ofa  wala  sio  hati.  Ujue  kuwa   bado  unayo  kazi  ya  kufanya kuelekea   kupatiwa  hati.

Ni  wajibu  wa  muuzaji  kutomlaghai  mnunuzi  asiyejua  tofauti  hizi  na  ni  wajibu  wa  mnunuzi  kuhakikisha  anachukua  hatua  mujarabu kujiridhisha ili  asiwe mwenye  kulaghaiwa na muuzaji.

5. USHAURI.

Ikiwa  unadhani  huna  uwezo  wa kutofautisha  vitu  hivi na  tayari  unahitaji  kununua  ardhi  basi  ni bora  kutafuta wataalam  wa  masuala  ya  ardhi  au  mwanasheria  wakusaidie  ili  kuepuka  usumbufu  na  gharama  zaidi.
MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MWANDISHI   WA  MAKALA  YA SHERIA  KUPITIA  GAZETI   LA  JAMHURI  KILA  JUMANNE..   0784482959,  0714047241  bashiryakub@ymail.com


0 comments:

Post a Comment