Wednesday 13 July 2016

HIZI NI HAKI ZAKO UNAPOHOJIWA NA POLISI.


Image result for AKIANDIKA MAELEZO POLISI
NA  BASHIR  YAKUB - 

Haki  hizi  zinatoka  katika  Sura  ya  20,  Sheria  ya  Mwenendo  wa  Makosa  ya  jinai   kifungu  cha  48  hadi  59. Ni  haki  ulizonazo  ikiwa utazuiliwa  na  kuhojiwa  na  polisi.

1. Ni  lazima  polisi  akutajie  jina  lake  pamoja  na  cheo  chake kabla  hajakuhoji.

2.  Lazima  uambiwe  tena kwa  lugha  inayoeleweka   kosa  ambalo  unatuhumiwa  nalo. Unaweza  kuambiwa  kwa  maandishi  au  kwa  mdomo.

3. Una  haki  ya  kutaka  kuitiwa  mwanasheria ,  ndugu, au  rafiki  ambaye  unaamini  atakusaidia  katika  kutoa  maelezo  au  kufanya  mahojiano.

4. Ni kosa  kulazimishwa  kukiri  kosa au  kuandika  kile askari  anachotaka.

5. Baada  ya  kutaja  jina  lako  na  anuani  yako  una  haki  ya  kutojibu  swali  jingine  ikiwa  utaona  inafaa  kufanya  hivyo.

6. Una  haki  ya  kukataa  kujibu  maswali  yasiyo  na  staha au  yanayolenga  kudhalilisha  au  kuondoa  utu  wako au  wa  familia  yako.

7. Hairuhusiwi   kupigwa, kudhalilishwa, kuteswa  unapohojiwa  au  unapokuwa  kizuizini.

8. Una  haki  ya  kupatiwa  au  kuwezeshwa  kupatiwa  matibabu  ikiwa u mgonjwa  au  una  jeraha  wakati  wa  mahojiano  au  kizuizini.

9. Ikiwa  aliyewekwa  kizuizini  ana  umri  chini  ya  miaka  16  basi  mara  tu  baada  ya  kukamatwa kwake  afisa  polisi  aliyemkamata au mwingine  ana  wajibu  wa  kuhakikisha  anawasiliana  na   mzazi  au  mlezi   na  kumweleza   kukamatwa , kituo  alipo, na  kosa  alilokamatiwa.

10. Askari  anayekuhoji  ana  wajibu  wa  kuweka  katika  rekodi/maandishi  mahojiano  yenu   ili  kusiwe  na  kuongezwa  au  kupunguzwa kwa  yale  uliyosema.

11. Baada  ya  mahojiano   utatakiwa  kupewa  yale  yaliyorekodiwa/kuandikwa  ili  nawe  uyapitie   kuona  kama  ulichosema  kimekosewa  au  kiko  sahihi.

12. Ikiwa  kilichorekodiwa  sicho  ulichosema  una  haki  ya  kumtaka  aliyekuwa  anarekodi/anaandika  kubadilisha  eneo  lilikosewa  na  kuandika  upya kile  unachoeleza.

13. Kama  hujui  kusoma  basi  unaweza  kumtaka  ndugu,  rafiki, au  mwanasheria  wako  akusomee  au  askari  polisi  akusomee   ili  uthibitishe usahihi wa  kilichoandikwa.

14. Iwapo  umekiri  kosa  na  umesoma  maelezo  yapo  sahihi   basi  mwishoni  utatakiwa  usaini  uthibitisho  maalum wa  kukiri  kosa.

15. Una  haki  ya  kuomba  kuandika  maelezo  badala  ya  kujibu  kwa  mdomo.

16. Ikiwa utaomba  kuandika  basi  ni  wajibu  wa polisi  kukuwezesha kwa vifaa  vinavyohitajika  ili  uandike.

17. Inaruhusiwa  kuhojiwa  masaa  manne tu,  isipokuwa  ikiwa  ya  kuhojiwa  bado  yapo  muda  huo  unaweza  kuongezwa  hadi  masaa nane .

18. Masaa  manne  ya  mahojiano yanapoisha  ni  lazima  ziwepo  sababu  za  msingi  za  kuongeza  masaa  mengine.  Si  hiari  ya  polisi  kuamua  bila  sababu  kuongeza  muda  wa  mahojiano.

19. Vitisho  na  kumlaghai  mtuhumiwa  wakati  wa  kuhoji  haviruhusiwi. Mtuhumiwa  atoe  maelezo  kwa  hiari  huru(free  consent).

20. Kabla  hujahojiwa  una  haki  ya  kuelezwa  haki  zako  ikiwemo  ile  ya  kukaa  kimya,  ile  ya  kuwa  maelezo  unayotoa  yanaweza  kutumika  mahakamani  kama  ushahidi  ili  uwe  makini, na  nyingine  zilizoelezwa  humu.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MWANDISHI   WA  MAKALA  YA SHERIA  KUPITIA  GAZETI   LA  JAMHURI  KILA  JUMANNE..   0784482959,  0714047241  bashiryakub@ymail.com



0 comments:

Post a Comment