Tuesday 28 June 2016

NINI UFANYE IKIWA UMESHITAKIWA MARA YA PILI KWA KOSA LILELILE.


Image result for MAHAKAMA
NA  BASHIR  YAKUB -

Marejeo  ya  makala haya ni  katika  makosa ya  madai yaliyo katika mashauri  ya  madai.  Japo  jambo  hili lipo hata  katika  makosa  ya  jinai yumkini makala    hayatajielekeza  huko. 

Basi  yafaa  ifahamike kuwa mtu  aliyeshitakkiwa  kwa  kosa  fulani,  kesi  ikasikilizwa  na  hukumu  ikatolewa akashinda  au  akashindwa, ni kuwa  kesi  ya  namna  hiyo  haitakiwi  kufunguliwa tena.  Isifunguliwe  tena  katika mahakama  hiyohiyo  au  mahakama  nyingineyo  nchini.

Haiwezekani  kesi  iliyosikilizwa na  kutolewa maamuzi    kufunguliwa  tena.  Yapo  mambo  yanayoweza  kufuata  baada  ya  kesi  kuisha  kwa  mfano  rufaa,  marejeo,  na  mapitio  lakini  sio  kufungua  tena  upya.

1.MAMBO  YANAYOZINGATIWA.

Yapo  mambo  ya  kuzingatia  ili  kesi  iliyokwisha  isifunguliwe  tena. Kwanza  ni  lazima  wahusika  wawe  ni  walewale.  Haiwezekani Shaaban  alimfungulia  kesi  Maria  ikasikilizwa na kutolewa maamuzi  halafu  shaaban  huyohuyo  akamfungulia  tena  Maria kesi  ileile kwa  kosa lilelile.

Shaaban  anaweza  kumfungulia  Maria  kesi  nyingine  ikiwa  ni  kwa  kosa  tofauti  na  lile  la  awali  lililokwisha kuamuliwa . Utaona  hapa  kuwa   kinachozuiwa  ni  mtu  yuleyule  kumfungulia  mtu  yuleyule  kwa  kosa  lilelile.

2.  NINI  UFANYE  HILO  LIKITOKEA.

Iwapo  hili  litatokea   wenye  wajibu  wa  kulizuia  ni  watu  wawili.  Kwanza  ni  wajibu  wa  mshitakiwa  kuieleza  mahakama  kuwa  kesi  hii  ilishahukumiwa   sehemu  fulani  na  hapa imerudiwa.  Ni  wajibu  kwa  mshitakiwa  au  mwakilishi  wake awe  wakili  au  vinginevyo.

Pili  ni  wajibu  kwa  jaji  anayesikiliza au  hakimu  anayesikiliza  kesi  hiyo   kufanya utafiti  kupitia  kumbukumbu  za  mahakanma  na  kuliona  hilo  ili  kulizuia. Hata  hivyo   wajibu  mkubwa  ni  mshitakiwa  kwakuwa  jaji au  hakimu  wakati  mwingine  anaweza  asiligundue  hilo hasa  ikiwa   kesi hiyo  iliisha  mahakama  nyingine  na  sasa  imefunguliwa   upya  mahakama  nyingine.

Hivyo   tunaweza  kusisitiza  kuwa  wajibu   mkubwa  upo  kwa  mshitakiwa  mwenyewe  kwasababu  yuko  katika  nafasi  nzuri  ya  kujua  historia  ya  kesi  yake  kuliko  mwingine  awaye.

3.  NINI  ADHABU  YA MAHAKAMA  HILO  LIKITOKEA.

Ikiwa  mshitakiwa  ataielekeza  mahakama  kuwa  kesi  iliyo  mbele  yake  iliwahi  kuamuliwa  pahala  fulani  au   mahakama  yenyewe  ikaligundua  hilo   basi  adhabu  kubwa  ikayotolewa  ni  kulitupilia  mbali  shauri  hilo. Kulitupilia  mbali  ni  kulifuta  kabisa.

Na juu  ya  hilo  mahakama kama itapendezwa inaweza  kutoa  amri  ya  kulipa gharama. Mshitaki  atatakiwa  kumlipa  mshitakiwa  gharama  alizotumia  mpaka  hapo  kesi   ilipoishia.

4. SHERIA  INAYOKATAZA  KUFUNGUA  TENA KESI  ILIYOAMULIWA.

Kifungu  cha  9  cha  sheria  ya  mwenendo  wa  mashauri  ya madai  ndicho  kinachokataza  jambo hili.  Kitaalam  jambo  hili  limeitwa RES  JUDICATA.  Kifungu  kinasema  kuwa  hakuna  mahakama   itakayosikiliza na kuamua  shauri  ambalo  shauri  kama  hilohilo, linalohusu  watu  walewale,  na  madai  yaleyale, na  ambalo  lilishasikilizwa  na  kuamuliwa  na  mahakama   nyingine yenye mamlaka.

Lengo  kuu  la  kuzuia   jambo hili  ni  kuwa  hakuwezi  kuwa  na  hukumu  mbili  zinazohusu  suala  moja.  Hukumu  ni  moja, kwa shauri moja nchi nzima .
MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MWANDISHI   WA  MAKALA  YA SHERIA  KUPITIA  GAZETI   LA  JAMHURI  KILA  JUMANNE..   0784482959,  0714047241  bashiryakub@ymail.com


0 comments:

Post a Comment