Tuesday, 24 May 2016

NAMNA YA KUWEKA PINGAMIZI KUZUIA NDOA KUFUNGWA.

Image result for PINGAMIZI KANISANI NDOA

NA  BASHIR YAKUB -

Ndoa inayotarajiwa  kufungwa  inaweza kuzuiwa kwa pingamizi. Sheria ilishaweka  utaratibu maalum  wa  kuzuia  ndoa  kufungwa  kwa  wale  wenye malengo  ya  kufanya  hivyo. Badala  ya kutumia  fujo ,mabaunsa na hila zisizo  za kisheria  kuzuia ndoa  au harusi  waweza  kutumia njia halali ya kisheria  na  ukafanikiwa  kuzuia  ndoa  kufungwa.

Fujo  na hila zisizo  za  kisheria katika kuzuia  ndoa zaweza  kukuletea   madhara makubwa na  hata  jinai. Ya nini  basi ufanye  hivyo   wakati   ipo  namna halali na salama ya  kuzuia .Sababu  zipi  unaweza kutumia kuzuia na  mengine  tutaona  hapa chini.

1.SABABU  ZINAZOKUBALIKA  KATIKA  KUZUIA  NDOA  KUFUNGWA.

( a ) Sababu  ya  kwanza  unayoweza  kutumia  kuzuia  ndoa isifungwe  ni kuthibitisha kuwa  kuna  ndoa  nyingine  inayoendelea. Muoaji  au  muolewaji  wote  kwa  pamoja  hawatakiwi  kuwa  wapo  katika  ndoa  nyingine  tofauti  na  hii  inayofungwa  sasa.  

Maana  yake  ni  kuwa  mwanaume  asiwe  na  mke  mwingine wa ndoa  na  mwanamke  asiwe  na  mwanaume  mwingine wa  ndoa.
Isipokuwa tu kama  mwanaume  ni  muislam  na  katika  ndoa ya  awali  alifunga  ndoa  ya  kiislam  basi pingamizi  hili  halitasimana. Lakini  akiwa ni  mkristo  na  hapo  awali alifunga  ndoa  ya  kanisani  basi  pingamizi  litasimama.

Lakini  pia  mwanaume  akiwa  muislam  au  dini  nyingine  na  hapo  awali  alifunga  ndoa  ya  serikali ya  mke  mmoja  basi  naye ndoa  yake  mpya  itazuiwa kwa  pingamizi. Isipokuwa  tu  kama  ndoa  hiyo  ilishakufa  kwa  talaka. Hayo  ni  kutoka  kifungu  cha  15  cha  sheria  ya  ndoa.

( b )  Sababu  nyingine  ya  kuzuia  ndoa  ni  pale  panapo  ushahidi  kuwa  mtu  anayetarajiwa  kuoa  au  kuolewa  ana  magonjwa  ya  kuambukiza. Kama  ni  mume  anataka  kuongeza  mke  basi  mke  wake  wa  kwanza  anaweza  kuweka  pingamizi  ili  kuepuka  magonjwa  ya  kuambukiza.

Hapohapo ithibati ya tabia mbaya ya mke anayetarajiwa kuolewa nayo ni  sababu ya kuzuia ndoa.

( c ) Sababu  nyingine  ni  ile  iliyoelezwa  kifungu  cha  14  sheria  ya  ndoa. Kimesema kuwa pale  ambapo  watu  wenye  undugu   wa damu  watataka  kufunga  ndoa  basi  linaweza  kuwekwa  pingamizi  na  ndoa  hiyo ikasitishwa.  Undugu  wa  damu  uliotajwa  ni  mtu  na  kaka, dada, mzazi, mjukuu, mtoto wa  kuzaa, shangazi, mjomba, na mtoto  uliyemuasili( adopt),

( d ) Umri  mdogo  wa  muoaji  au  muolewaji  ni  sababu  ya  pingamizi.  Aidha nje  na  sababu  hizi   sheria  inakubali  sababu  nyingine  yoyote  ambayo  itaonekana  ni  ya  msingi  mbele  ya  macho  ya  sheria.

2. NAMNA  YA  KUWEKA  PINGAMIZI.

( a ) PINGAMIZI  LIWASILISHWE  WAPI.

Zipo  sehemu  tatu ambapo  waweza  kupeleka  pingamizi  lako. Kwanza  ni  mahakamani.  Mahakama  ya mwanzo  au ya  wilaya katika  eneo  lako  yaweza  kutumika  katika  kuweka  pingamizi. Pili ni  kwa  wakala  wa  usajili,ufilisi  na  udhamini( RITA).

Tatu  ni  katika  baraza  la  usuluhishi  wa  ndoa. Kwa  waislamu  baraza  hili  ni  BAKWATA  na  kwa  wengine ni  ustawi  wa   jamii. Ofisi  za  ustawi  wa  jamii  huwa katika  makao  makuu  ya kila wilaya.

Hata  hivyo  waislamu  nao  hawazuiwi  kutumia ustawi wa jamii katika kuweka  pingamizi . Katika ofisi nilizotaja ukifika hapo utaeleza  shida yako  halafu  utaelezwa  utaratibu.

( b ) KUSIKILIZWA PINGAMIZI NA UAMUZI.

Baada ya  kuwasilisha  pingamizi  haraka  iwezekanavyo  pingamizi  litasikilizwa na  uamuzi  utatolewa.  Kama  sababu  ni  za  msingi  ndoa  itazuiwa na  kama  si  za  msingi  pingamizi litatupiliwa mbali.

Na  katika kusikiliza  pande  zote  zitaitwa  kutoa  maelezo. Upande  unaopingwa  ukikaidi  kufika  basi  mlalamikaji  atasikilizwa  peke  yake  na  uamuzi  utatolewa.
MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA     SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.      0784482959,        0714047241              bashiryakub@ymail.com
0 comments:

Post a Comment