NA BASHIR YAKUB -
1.NINI MAANA YA KUUMIA KAZINI.
Kuumia kazini kunajumuisha kila jeraha analolipata mfanyakazi wakati akitekeleza majukumu yake ya kazi. Jeraha laweza kuwa dogo au kubwa lakini litaitwa jeraha tu. Katika maana hii yapo mambo mawili kwanza jeraha na pili wakati ukiwa kazini. Ili mfanyakazi apate stahiki zake ni lazima haya mawili yatokee.
( a ) JERAHA HUJUMUISHA NINI.
Jeraha ni pamoja na kidonda, kukatika kiungo iwe mkono , mguu, kidole au vinginevyo, kuathirika akili, magonjwa yaliyotokana na kazi kwa mfano kansa inayotokana na kemikali za viwanda, magonjwa ya ngozi, na athari nyingine za kimwili au kiakili zilizotokea wakati mfanyakazi akiwa kazini au zilizosababishwa na kazi ya mfanyakazi.
( b ) NI WAKATI UPI NI WA KAZI.
Wakati wa kazi ni wakati wote ambao mfanyakazi atakuwa akitekeleza majukumu yake ya kazi kwa mujibu wa ratiba ya ofisi. Kuumia ukitekeleza kazi za kiofisi nyumbani kwako hakuwezi kuhesabika kama kuumia kazini /wakati wa kazi.
Lakini kuumia ukiwa safarini kuelekea mkoa au nchi fulani kutekeleza majukumu ya kazi ni kuumia wakati wa kazi. Hii ndiyo tafsiri yake.
2. AINA ZA MAJERAHA ZINAZOTOLEWA FIDIA.
Aina za majeraha zinazotolewa fidia zimegawanyika katika makundi makuu manne. Kwanza ni kuumia kunakomfanya mtu kupoteza kabisa uwezo wa kufanya kazi(permanent total incapacity. Hapa moja kwa moja ni kuwa mtu huyu hataweza abadan asilan kufanya kazi tena.
Hajafa lakini hawezi tena maishani kutekeleza kazi aliyokuwa akifanya.
Pili ni jeraha la kudumu lakini likiwa ni sehemu tu ya kiungo( permanent partial incapacity). Kwa mfano kwenye mkono unaweza kukatika tu vidole kadhaa. Ni jeraha la kudumu kwani huwezi tena kupata vidole hivyo lakini ni sehemu ya mkono na sio mkono mzima.
Tatu ni jeraha la muda au ulemavu wa muda ( temporary incapacity). Kwa mfano kuvunjika mguu au mkono lakini pengine baada ya matibabu ya miezi kadhaa ukapona.
Nne, ni jeraha linalopelekea kifo cha mfanyakazi.
3. JE UNASTAHILI NINI KATIKA HAYA.
Katika kuumia kunakomfanya mtu kupoteza kabisa uwezo wa kufanya kazi(permanent total incapacity mfanyakazi atatakiwa kulipwa asilimia 70 ya wastani wa mshahara wake kwa kipindi cha miaka saba.
Pili katika jeraha la kudumu lakini likiwa ni sehemu tu ya kiungo( permanent partial incapacity) inafanyika tathmini kuangalia kiwango cha ulemavu au jeraha kama kiko chini ya asilimia 30.
Kikiwa chini ya 30% basi atalipwa pesa yake kwa mkupuo kutokana na asilimia za kiwango cha ulemavu walizotathmini wataalam. Hata hivyo kiwango cha juu kabisa hakitazidi mara 84 ya mshahara wa mwezi wa mfanyakazi.
Tatu, katika jeraha la muda au ulemavu wa muda ( temporary incapacity) mfanyakazi mwenye bima baada ya kupata cheti cha bodi ya madaktari atalipwa 60% ya mshahara wake wa wastani wa siku moja hadi 26.
Nne, katika jeraha linalopelekea kifo cha mfanyakazi basi wategemezi wake watapata pensheni hadi 60% ya wastani wa mshahara wa marehemu kwa mwezi, na fidia ya kifo inayofikia hadi Tshs 300,000/=.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA HABARI LEO KILA JUMANNE , GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI NIPASHE KILA JUMATANO. 0784482959, 0714047241 bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment