Monday, 16 May 2016

JE NI HALALI KUMWACHISHA KAZI MFANYAKAZI KWA KOSA LA KWANZA.

Image result for WAfanyakazi MAANDamano

NA  BASHIR  YAKUB - 

Sheria  ya  Ajira  na  Mahusiano  Kazini  ya 2004 ndiyo  sheria  mama  katika  masuala  ya  ajira. Kwa  anayetaka  kujua  haki  na  wajibu  wa kazi  na  mfanyakazi,  mwajiri  na  mwajiriwa  basi  na  asome  sheria  hii.  Sheria  hii  ilianza kutumika  rasmi tarehe  5/ 1/  2007.

Misingi  mikuu  ya sheria  hii  ni  usawa  wa  ajira kwa  jinsia, ujira  unaolingana  na kazi  inayofanywa  na  mfanyakazi, haki  na  maslahi  bora  kwa  mfanyakazi, mazingira  bora  na  salama  ya  kazi  na  mengine  mengi  hasa  yanayoshabihiana  na  haki  za  binadamu.

Kumwachisha  kazi  mfanyakazi  ni  moja  ya  maeneo  muhimu  katika  sheria  hii. Wakati  gani  mfanyakazi  aachishwe  kazi,  kwa  kosa  gani, utaratibu wa  kumwachisha  kazi,  stahiki  zake  baada  ya  kuachishwa  kazi,  uachishwaji  kazi  haramu, utaratibu  wa  hatua  za  kuchukua  panapo  uharamu  katika  kuachishwa  kazi  ni  sehemu ya  mambo  muhimu  katika  sheria  hii.

Makala  haya  yataeleza  habari  hii  ya kuachishwa  kazi  lakini  yatalenga  kipengele  kimoja  tu  cha  uhalali wa  kumwachisha  mfanyakazi  kwa kosa  la  kwanza.

1.NI  IPI  TAFSIRI  YA  KUACHISHWA  KAZI.

Kuachishwa  kazi  ni  hatua  ambapo  muajiri  husitisha  mkataba  wa  ajira  kwa  notisi  au  bila  notisi  kwasababu  mbalimbali  zikiwemo  za  utovu  wa nidhamu.

2. MFANYAKAZI  APIMWE KATIKA  MAMBO HAYA  KABLA  YA  KUACHISHWA  KAZI.

( a ) Je  mfanyakazi  amekiuka  kanuni  za  nidhamu.Kanuni  za  nidhamu  zipo  kwa  mujibu  wa  sheria.  Hazitokani  na  masharti  ya  kazi  yaliyowekwa  na  mwajiri. Lipo  jambo  ambalo mwajiri  anaweza  kuliita  utovu  wa nidhamu  lakini  kwa  kulipima  na  kanuni  za  nidhamu  likawa  sio.  Kwahiyo  ili kuachishwa kazi ni  lazima mfanyakazi  awe amekiuka  kanuni  za  nidhamu  kwa  mujibu  wa  sheria.

( b ) Je  mfanyakazi  alikuwa  anafahamu  kanuni  iliyokiukwa. Hapa  kuna  makusudi  na  bahati  mbaya.  Ikiwa  ni makusudi  kwa  ushahidi  basi atawajibishwa  lakini  ikiwa kwa  ushahidi inaonesha  kuwa  si  makusudi  isipokuwa  ni  kutokujua  basi  hilo litazingatiwa na adhabu nje ya  kuachishwa kazi itachukuliwa.

( c ) Je  kwa  kosa  lililotendwa  adhabu  ya  kuachishwa  kazi  ndiyo  inayostahili. Hakuna  adhabu  nyingine  nje  ya  kuachishwa  kazi. Mwajiri  apime  kabla  ya  kuchukua  hatua.

( d ) Je  kanuni  iliyokiukwa  ni  kanuni  isiyokuwa  na  utata  wowote  kisheria. Zipo  kanuni  tata ambazo  hazina  majibu  ya  moja  kwa  moja. Mfanyakazi  anatakiwa  kuachishwa  kazi  katika  kanuni  za  kinidhamu  zisizo  na  utata.

3.JE  KOSA  LA  KWANZA  LINAHALALISHA  ADHABU  YA  KUACHISHWA  KAZI.

Jibu  ni  hapana  kosa  la  kwanza  la  mfanyakazi  halihalalishi  kuachishwa  kazi  labda  kosa  hilo  likiwa  kubwa.  Yapo  makosa makubwa  ya  utovu  wa nidhamu  katika  kazi  na  yapo  yale  yasiyokuwa  makubwa.

Makosa  makubwa  ambayo  mfanyakazi  akiyatenda  kama  kosa  la  kwanza  anaweza  kuachishwa  kazi  ni  kama  haya.

( a ) Kukosa  uaminifu  kwa  kiwango  cha  juu. Hapa  yanajumuishwa  makosa  ya  wizi, utapeli, ujambazi, kughushi,  na  mengine  yanayofanana  na  hayo.

( b ) Ukaidi. Huu  usiwe  ule  ukaidi  wa  kawaida  bali  ukaidi ulichupa  mipaka.  Ukaidi  ambao  humpelekea  mfanyakazi  kutosikiliza  kabisa  maagizo  halali ya   wakubwa  wake  wa  kazi .      

( c ) Uzembe  usio  wa  kawaida. Huu  ni  uzembe  wa  kiwango  cha  juu  ambao humpelekea  mfanyakazi  kutotekeleza  tena  majukumu ya  kazi  yake.

( d ) Kushambulia.

( e ) Kuharibu  mali  za  mwajiri  tena  kwa  makusudi. Mali  za  mwajiri  ni  pamoja  na  vitendea  kazi  ambavyo  mwajiriwa atakuwa   amekabidhiwa  ili  kutekeleza  majukumu  yake.

Kwahiyo  kuachishwa  kazi  kwa  kosa  la  kwanza   ambalo  sio  kubwa  ni kinyume  cha  sheria.
MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA     SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.      0784482959,        0714047241              bashiryakub@ymail.com

0 comments:

Post a Comment