Thursday 12 May 2016

JE WE NI MFANYAKAZI, UNAJUA STAHIKI ZAKO UNAPOUMIA KAZINI.

Image result for KUUMIA KAZINI

NA  BASHIR  YAKUB - 

1.NINI MAANA  YA  KUUMIA  KAZINI.

Kuumia  kazini  kunajumuisha  kila  jeraha  analolipata  mfanyakazi  wakati  akitekeleza  majukumu  yake  ya  kazi. Jeraha  laweza  kuwa  dogo  au  kubwa   lakini  litaitwa jeraha  tu. Katika maana  hii  yapo  mambo mawili  kwanza  jeraha  na  pili   wakati  ukiwa  kazini.  Ili  mfanyakazi  apate  stahiki  zake  ni  lazima  haya mawili  yatokee.

( a ) JERAHA  HUJUMUISHA  NINI.

Jeraha  ni  pamoja  na  kidonda, kukatika  kiungo iwe  mkono ,  mguu,  kidole  au  vinginevyo, kuathirika  akili, magonjwa yaliyotokana  na  kazi  kwa  mfano  kansa  inayotokana  na  kemikali  za  viwanda, magonjwa  ya  ngozi, na athari  nyingine  za  kimwili  au  kiakili  zilizotokea   wakati  mfanyakazi  akiwa  kazini au  zilizosababishwa na  kazi   ya  mfanyakazi.

( b ) NI  WAKATI  UPI  NI  WA  KAZI.

Wakati  wa  kazi  ni  wakati  wote  ambao  mfanyakazi  atakuwa  akitekeleza  majukumu  yake  ya  kazi kwa  mujibu  wa  ratiba  ya  ofisi. Kuumia  ukitekeleza  kazi  za  kiofisi  nyumbani  kwako  hakuwezi  kuhesabika   kama  kuumia  kazini /wakati  wa  kazi.

Lakini  kuumia  ukiwa  safarini  kuelekea  mkoa  au  nchi  fulani  kutekeleza  majukumu  ya  kazi  ni  kuumia  wakati  wa  kazi.  Hii  ndiyo  tafsiri  yake.

2.  AINA  ZA  MAJERAHA  ZINAZOTOLEWA  FIDIA.

Aina za  majeraha  zinazotolewa  fidia zimegawanyika katika  makundi  makuu  manne. Kwanza ni  kuumia  kunakomfanya  mtu  kupoteza  kabisa  uwezo  wa  kufanya  kazi(permanent  total incapacity. Hapa   moja  kwa  moja  ni kuwa  mtu  huyu  hataweza  abadan  asilan  kufanya  kazi  tena.

Hajafa  lakini   hawezi  tena  maishani  kutekeleza  kazi  aliyokuwa  akifanya.
Pili ni jeraha  la  kudumu  lakini  likiwa  ni  sehemu  tu  ya  kiungo( permanent partial incapacity). Kwa  mfano  kwenye  mkono  unaweza  kukatika  tu   vidole kadhaa.  Ni  jeraha  la  kudumu  kwani  huwezi  tena  kupata  vidole hivyo  lakini  ni  sehemu  ya mkono  na sio  mkono  mzima.

Tatu  ni  jeraha  la  muda  au  ulemavu  wa  muda ( temporary  incapacity). Kwa  mfano  kuvunjika  mguu  au  mkono  lakini  pengine  baada  ya  matibabu ya  miezi  kadhaa ukapona.

Nne, ni  jeraha  linalopelekea  kifo  cha  mfanyakazi.

3. JE  UNASTAHILI  NINI  KATIKA  HAYA.

Katika  kuumia  kunakomfanya  mtu  kupoteza  kabisa  uwezo  wa  kufanya  kazi(permanent  total incapacity  mfanyakazi  atatakiwa  kulipwa  asilimia  70  ya  wastani  wa  mshahara  wake  kwa  kipindi cha  miaka  saba.

Pili katika jeraha  la  kudumu  lakini  likiwa  ni  sehemu  tu  ya  kiungo( permanent partial incapacity)  inafanyika  tathmini  kuangalia  kiwango  cha  ulemavu  au  jeraha  kama  kiko  chini  ya  asilimia  30.

Kikiwa  chini  ya  30% basi  atalipwa  pesa  yake kwa  mkupuo  kutokana  na  asilimia  za  kiwango  cha  ulemavu  walizotathmini  wataalam. Hata  hivyo kiwango  cha  juu  kabisa  hakitazidi  mara  84  ya  mshahara   wa  mwezi  wa  mfanyakazi.

Tatu, katika  jeraha  la  muda  au  ulemavu  wa  muda ( temporary  incapacity) mfanyakazi  mwenye  bima baada  ya  kupata  cheti  cha  bodi  ya  madaktari  atalipwa  60% ya  mshahara  wake  wa  wastani  wa  siku  moja  hadi  26.

Nne, katika  jeraha  linalopelekea  kifo  cha  mfanyakazi   basi  wategemezi  wake  watapata  pensheni   hadi  60% ya wastani  wa  mshahara  wa marehemu  kwa  mwezi, na fidia  ya  kifo  inayofikia  hadi  Tshs 300,000/=.
MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA     SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.      0784482959,        0714047241              bashiryakub@ymail.com


0 comments:

Post a Comment