NA BASHIR YAKUB -
Mara kadhaa nimeliona
hili. Hata we
pia ni imani
umeliona. Tunaliona hili katika
vyombo vyetu mbalimbali
vya usafiri .Tunashuhudia askari
wetu wakikataa kutoa
nauli. Na hii ni kwa
jeshi, polisi , magereza na hata
wale wa barabarani. Hata hivyo sio wote wapo
wanaotoa . Na zaidi hawatoi wakiwa wamevaa
sare.
Lakini mbona hawatoi
kwenye magari tu na si kwenye Fast jet au Emirates. Sijui ni kwanini.
Tunahitaji ufafanuzi
wa kisheria kulijua
hili. Tunahitaji maelezo ikiwa
inaruhusiwa kwao kufanya
hivyo au hapana.
1.SHERIA INAYOONGOZA
JESHI LA POLISI.
Jeshi la polisi
hutekeleza kila jukumu
lake kwa mujibu
wa sheria. Sheria
kuu inayoongoza majukumu yao
ya kila siku hujulikana
kama Sheria ya
Jeshi la Polisi
sura ya 322.
Humu umeelezwa wajibu na
haki zao. Imeelezwa
nini wafanye , nini wasifanye na nini wafanyiwe.
Sambamba na sheria
hiyo pia zipo sheria nyingine
ambazo hueleza wajibu
wao katika majukumu yao.
Ipo sheria ya
kanuni za adhabu
sura ya 16,
ipo sheria ya
mwenendo wa makosa
ya jinai pamoja
na sheria ya
ushahidi. Hii ni kwakuwa hawa hushughulika na
makosa ya jinai .
Kwa hiyo kama
kuna jambo lolote
tunahitaji kujua kuhusu
hawa basi tunataraji
kulipata katika sheria
hizi. Na kama
halipo humu basi
itabidi watueleze walikolipata.
2. SHERIA
YA JESHI LA
WANANCHI.
Jeshi la wananchi nao wanayo
majukumu na haki zao za kisheria. Kubwa kwao ni kulinda
mipaka. Wao nao
wanazo kanuni na sheria
zinazowaongoza. Moja ya sheria
inayawaongoza ni ile
ijulikanayo kama The National Defence
Act 1966.
Kwa hiyo ikiwa
kuna lolote tunahitaji kujua kama
ni haki yao basi tunataraji
kulipata katika sheria zinazowaongoza pamoja
na sheria nyinginezo.Kama
halimo tutahitaji maelezo
walikolipata.
3. SHERIA YA
MAGEREZA.
Magereza nao ni sehemu
ya majeshi ya usalama. Kazi yao kubwa
ni kiusimamia shugughuli
zote zinazohusu wafungwa. Sheria
inayotumika katika majukumu yao
huitwa The Prison Act, 1967.
Kwa hiyo ikiwa kuna lolote tunahitaji kujua
kama ni haki
yao basi tunataraji kulipata katika sheria
zinazowaongoza pamoja na sheria nyinginezo.Kama halimo nao
tutahitaji watueleze walikolipata.
4. JE KATIKA
SHERIA HIZI KUNA
SEHEMU WAMEZUIWA KULIPA
NAULI.
Hapana, hakuna kifungu
chochote katika sheria hizo kinachokataza
askari polisi, jeshi, au
magereza kutolipa nauli. Yapo
mambo yanayokatazwa katika
sheria hizo lakini
suala la nauli
si sehemu ya hayo mambo.
Wakati mwingine ni
vigumu kujua jambo
hili lilitoka wapi katika nchi
inayofuata utawala wa sheria.
5. SHERIA YA SUMATRA.
Mamlaka ya usafiri
wa nchi kavu
na majini huitwa
SUMATRA. Hawa kazi yao
pamoja na mambo mengine
ni kuratibu taratibu
za usafiri wa
nchi kavu na
majini .
Usimamizi na uratibu wa nauli ni sehemu ya majukumu yao. Sheria
kuu inayowaongoza huitwa
The Surface and Marine Transport Regulatory Authority Act. Ni sheria namba
9 ya 2001.
Sheria hii husomwa
na kanuni za SUMATRA.
Si ndani ya kanuni hizo
wala hiyo sheria kunamoelezwa
askari jeshi na
polisi wasilipe nauli. Jambo
hilo halipatikani kabisa.
6. BASI KUTOLIPA NAULI
IWE HISANI.
Sisemi ni vibaya
kutolipa nauli kwa
makundi haya. Ninachosema ni kuwa
iwe hisani. Ikiwa
hisani maana yake
ni kuwa anayetaka
atawatoza na asiyetaka
hatawatoza. Ni kosa kwao
kulifanya jambo hili la lazima na la kisheria. Na hapo
ndipo lilipo tatizo. Kumlazimisha
mwenye chombo cha usafiri asikutoze nauli hakukubaliki.
Kutolipa nauli si haki
ya yeyote kwa mujibu wa sheria.Hata
amiri jeshi mkuu rais Magufuli akipanda gari lazima alipe nauli. Hakuna aliye
juu ya sheria. Wao
ni watumishi kama
walivyo watumishi wengine
wote. Na kila
mtumishi ana umuhimu wake.
Lakini pia
kila mtumishi fulani anategemea kazi inayofanywa na mtumishi mwingine
ili aishi. Kitu hiki
hufanya kila idara
kuwa na umuhimu
wake wa pekee.Kwa hiyo kila idara
ni muhimu tena sana.
Ni kwa mantiki hii hatuwezi kusema
idara fulani ilipe
nauli na idara
nyingine isilipe kwakuwa ni
ya muhimu zaidi, hapana.Na kama
hilo litakuwepo litakuwa ni
kwa makubaliano na mipaka
maalum kama lilivyo lile
la waalimu wa Dar
es salaam.
Kutokana na haya
yafaa wenye vyombo
vya usafiri wawatoze
nauli hawa. Ikiwa hawatawatoza
iwe ni kwa hiari
lakini isiwe lazima au kwa shinikizo.
Makondakta na wenye
magari hawapaswi hata kidogo
kuogopa kudai nauli
kutoka kwa makundi
haya kwani hiyo
ni haki yao ya
msingi kama ilivyo
kwa abiria wengine wote. Inakera sana
kuona jambo hili linafanywa la
lazima na baadhi ya askari na wanajeshi.
Hatua unazoweza kumchukulia
abiria ambaye hajalipa nauli
ndizo unazoweza kuyachukulia makundi haya yasipolipa nauli.
MWANDISHI WA MAKALA
HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA
GAZETI LA SERIKALI LA HABARI
LEO KILA JUMANNE , GAZETI JAMHURI
KILA JUMANNE NA GAZETI NIPASHE KILA
JUMATANO. 0784482959,
0714047241
bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment