Monday, 9 May 2016

FAHAMU NAMNA YA KUFUNGUA MIRATHI


Image result for MALI ZA MIRATHI
NA  BASHIR  YAKUB - 

1.MIRATHI  NI NINI.

Mirathi  ni  mali  ya  marehemu  aliyoiacha  kwa  ajili  ya  kurithisha  warithi  wake  halali. Hakuna  mirathi   kabla  ya kifo  cha  mtu. Ni  lazima  mtu    afe  ndipo  ipatikane  mirathi.  Na  mirathi  kwa  ujumla  wake  huhusisha  mali  alizoacha  marehemu.

2.  NINI  LENGO  LA  UTARATIBU  WA  MIRATHI.

Lengo  kuu  la  kuwepo  utaratibu  maalum  wa  mirathi   ni  kukusanya, kuangalia, kusimamia, na kugawa mali  alizoacha  marehemu.  Kulipa  madeni  aliyoacha  marehemu   na  kujua  madeni  hayo  yalipo  nalo  ni lengo  la  kuanzishwa  utaratibu  huu  wa  mirathi. 

Lakini  jingine  katika  hili   ni  kusimamia  shughuli  za  mazishi  ikiwa  ni  pamoja  na  kufuata  maelekezo  ya  marehemu    kuhusu  namna  na  wapi  azikwe.  Hizi  zote  ni  shughuli  zilizopelekea  kuanzishwa  utaratibu  wa   mirathi.

Kama  utaratibu  huu  usingewekwa  na  sheria  basi  ingekuwa  rahisi   mali  za  marehemu  kupotea  hovyo,kuharibiwa,  kutumiwa  vibaya  na  kuhujumiwa. 

Lakini  ingekuwa    rahisi  kwa   wale  wote  wanaomdai  marehemu  kupoteza haki  zao  za  madai  baada  ya  kufa.  Lakini  kwa utaratibu  maalum wa  mirathi hawa nao hawawezi   kupoteza  haki  zao.

3.  NI  SHERIA  ZIPI  HUTUMIKA  KATIKA  MIRATHI.

Hapa  Tanzania  zipo  sheria  tofauti  tatu  zinazotumika  katika  mirathi.  Ipo  sheria  ya  serikali,  zipo  sheria  za  kimila  na   zipo  sheria  za  dini  ya  kiislamu.  Makala ya  leo hayataingia    ndani  zaidi  kueleza  sheria  hizi. Kwa  leo  itoshe  kujua  tu  kuwa  sheria zinazotumika  kwa  hapa  kwetu  ni  hizo  tatu.

4. NAMNA  YA  KUFUNGUA  MIRATHI.

(  a )  Hatua  ya  kwanza  kabisa  pale  tu  mtu  anapokufa  hakikisha  hazipiti  siku  thelathini  kabla ya  kupata  cheti  cha  kifo.  Makao  makuu  ya  wilaya   ndipo  vinapopatikana  hivi vyeti.  Na  wilaya  inayotumika  ni  ile   wiaya  alikofia  marehemu.  Cheti  hiki  ni  lazima    katika  shughuli  za  mirathi.

( b ) Hatua  ya pili  ni  kufanya  kikao  cha  familia  na  kumteua  msimamizi  wa  mirathi.  Wanafamilia  watakaa  watajadili  na  kwa  pamoja  watampata  msimamizi wa  mirathi. Mnapokaa  kikao  cha  familia  hakikisha  zile  ajenda  zote  mlizojadili  zinawekwa  katika  maandishi. Na ni  katika  kikao  hicho  ambapo  utatakiwa  kuandaliwa  mukhtasari. 

Mukhtasari  utaeleza  ajenda  za  kikao, waliohudhuria, aliyeteuliwa  kusimamia mirathi, hutaja  warithi na  mengine mengi.  Mukhtasari  hutakiwa  kuandikwa  kwa  mkono  na  sio  kuchapwa.  Na  kila  aliyehudhuria  atasaini.

( c ) Hatua  ya  tatu  ni kupata  barua  kutoka  serikali  za  mitaa.  Ukisema nataka  barua  ya  kufungua  mirathi  basi serikali  za  mitaa  wanajua  ni  barua ya  aina  gani  upewe.

( d ) Hatua  ya  nne  ni  kwenda  mahakamani  ili  kuthibitishwa  kuwa  msimamizi  wa  mirathi. Hapa  utatakiwa  kwenda na  cheti  cha  kifo, barua  ya  serikali  za  mitaa, mukhtasari  wa  kikao  cha  familia, na  picha  mbili  za  pasipoti.

Hata hivyo  ni  muhimu  kujua  kuwa  ikiwa  marehemu  aliacha  wosia  na  katika  wosia huo  msimamizi  wa  mirathi  ametajwa  basi  hakutakuwa  na  haja  ya  kukaaa  kikao  cha  familia  kumteua  msimamizi  wa  mirathi.

Hii ina  maana  hata   mtakapokwenda  mahakamani  ili  kumthibitisha  huyo  msimamizi  wa  mirathi basi  badala  ya  kuambatanisha  mukhtasari    mtaambatanisha  wosia.

Mahakamani  ndiyo  hatua  ya  mwisho.  Kwahiyo  baada  ya  taratibu  za kimahakama  ikiwamo  ile  ya  kutoa  tangazo  kwa  mwenye  kupinga kumalizika,  basi  msimamizi  atapitishwa  na  atapewa  fomu  maalum  ya  usimamizi  mirathi.
MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA     SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.      0784482959,        0714047241              bashiryakub@ymail.com



2 comments:

  • Unknown says:
    20 October 2020 at 21:40

    Kuna gharama zozote za malipo katika kufungua mirathi

  • Unknown says:
    10 April 2022 at 03:48

    Mfano wa barua ya kumthibitsha msimamizi wa mirathi

Post a Comment