NA BASHIR YAKUB -
Wapo baadhi ya
askari hutumia nafasi
zao vibaya. Wapo wanaojua na
kutekeleza wajibu wao wa kisheria
na wapo wasiotekeleza
wajibu wao wa
kisheria. Raia hulalamika sana.
Moja ya maeneo makubwa yanayolalamikiwa ni
hili la kukamatwa
bila sababu za
msingi/kuwekwa ndani bila
sababu za msingi na
wakati mwingine kufunguliwa mashtaka bila
sababu za msingi.
Leo sio ajabu
askari kugombea mwanamke na
mwanaume mwenzake halafu
akamtafutia sababu na kumweka ndani
au akambambika shitaka bila
kosa lolote. Leo sio
ajabu kutupiana maneno mawili
matatu na askari
halafu ghafla ukaambiwa umekamatwa
na bunduki, leo sio
ajabu mwenye hela
kuamua amfunge nani kwa kutumia askari . Matukio ni mengi
yanayofanana na haya.
1.KUENDELEA KWA MATENDO
YA KUKAMATWA/KUWEKWA NDANI BILA
SABABU ZA MSINGI.
Hakuna shaka matendo
haya yameendelea kwasababu
wanaotendewa huwa hawachukui
hatua. Mtu anakamatwa
anawekwa ndani bila
sababu za msingi akiachiwa anashukuru
na kuondoka. Mwingine
anabambikiwa kesi inamtesa miaka na miaka ikiisha anashukuru na kuondoka. Namna
hii haiwezi kuwa suluhu. Kama hii
itakuwa suluhu basi wengi wajiandae kuumia.
Makala
yanazungumzia kukamata au kuweka
ndani bila sababu
za msingi( false
imprisonment/arrest). Hii isichanganywe na kumshitaki
mtu bila sababu
za msingi( malicious
prosecution). Japo kwa
namna fulani yanafanana
lakini makala haizungumzii
kushitaki bila sababu
za msingi.
2. NINI MAANA
YA KUMWEKA NDANI MTU
/KUMFUNGA BILA SABABU
ZA MSINGI.
Kumweka ndani mtu/kumfunga bila
sababu za msingi
ni kumzuia mtu bila hiari
yake na bila
sababu za msingi. Kuweka
ndani ndio kufunga. Na
kufunga kisheria sio
lazima mtu aingizwe
selo. Kuzuia uhuru wa
mtu kunatosha kuitwa
kufunga kisheria. Ndio
maana kufunga mtu inaweza kuwa
kwa maneno , kwa
matendo au vyote.
Kitendo
cha askari kumwambia
mtu uko chini
ya ulinzi hata
kama hajamgusa tayari
ni kumfunga. Ni kumfunga
kwasababu tayari mtu amepokonywa uhuru
wake na hivyo
hawezi kuendelea na shughuli zake.
Hivyo ni vema
kujua kuwa unaweza
kumshitaki askari hata
kwa kukwambia tu kuwa
uko chini ya ulinzi kama amefanya hivyo bila sababu
za msingi na kwa
hila( maliciously).
3. JE KUTOMPELEKA MTUHUMIWA
MAHAKAMANI NI KUFUNGA
BILA SABABU ZA MSINGI.
Mtuhumiwa aliyewekwa
ndani zaidi ya
masaa 24 bila
kupelekwa mahakamani naye
anahesabika katika wale
waliofungwa bila sababu
za msingi hivyo
anaweza kuwafungulia mashtaka askari wa
kituo kwa kufanya
hivyo.
Sheria iko wazi
kuwa ikiwa mtuhumiwa
alipokamatiwa ni karibu
na mahakama na hakuna umbali
wa kusababisha kucheleweshwa
kufikishwa mahakamani basi
ndani ya muda
mfupi inatakiwa mtuhumiwa
afikishwe mahakamani.
Ikiwa hilo halitafanyika
na
huku lilikuwa linawezekana
basi kuendelea kuzuiliwa
ni kosa ambalo
mtendewa anaweza kuwashitaki wahusika. Hii
ni kwasababu kutofikishwa
mahakamani kwa wakati
kumetafsiriwa kama kufungwa au
kuzuiliwa bila sababu
za msingi( false imprisonment).
4. NAMNA YA
KUSHITAKI.
Utafungua shauri la
madai ya fidia. Mshitakiwa wa kwanza
atakuwa askari aliyekukamata
au kukuweka chini
ya ulinzi. Hata wawe
sita wote kwa
pamoja watakuwa washitakiwa
wa kwanza. Wa
pili atakuwa mkuu wa
jeshi la polisi
na wa tatu atakuwa
mwanasheria mkuu wa
serikali.
Mkuu wa polisi na
mwanasheria mkuu wa
serikali wanaunganishwa kutokana
na matakwa ya
kisheria. Na moja ya
sababu inatokana na nafasi
yao ya uajiri wao kwa mlalamikiwa.
5. ILI USHINDE
UTATAKIWA KUTHIBITISHA MAMBO MAKUU MAWILI.
Kwanza uthibitishe
kuwa uliwekwa chini
ya ulinzi/kufungwa bila
hiari yako. Pili uthibitishe
kuwa kuwekwa kwako
chini ya ulinzi
au kufungwa kulifanyika
bila sababu za
msingi. Kwa maana ya kuwa
hakukuwa na sababu yoyote
ya msingi ya kukuweka chini
ya ulinzi/kukufunga.
6. ILI ULIPWE
KIASI CHA FIDIA
ULICHOOMBA UTATHIBITISHA HAYA.
Katika shauri hili
utakuwa ukiomba kulipwa fidia. Waweza
kuwa umeomba milioni
10,20, 50, 100 n,k. Na ili ulipwe utatakiwa kuonesha
kuwa uliathirika. Kuathirika kwaweza
kuwa kuathirika kiakili( mental suffering), kuaibishwa,
kushushiwa hadhi, kuumia kimwili, kupotezewa muda, kuharibiwa biashara
au/na shughuli nyingine, na
hasara nyingine yoyote
iliyotokana na kitendo
hicho.
Ikiwa utathibitisha haya utakuwa
umefanikiwa katika shauri
la namna hii.
MWANDISHI WA MAKALA
HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA
GAZETI LA SERIKALI LA HABARI
LEO KILA JUMANNE , GAZETI JAMHURI
KILA JUMANNE NA GAZETI NIPASHE KILA
JUMATANO. 0784482959,
0714047241
bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment