Wednesday, 20 April 2016

UNAPOPATA AJALI FANYA HAYA KUHUSU BIMA.

Image result for INSURANCE

NA  BASHIR  YAKUB - 

Yapo  mambo  mengi  ya  kufahamu  kuhusu  bima  za  magari.  Yako  mambo  ya sera  na  sheria. Lakini  kubwa  yapo  mambo  yanayohusu  hatua  za  kuchukua  pale panapo  ajali. Zipo  aina  nyingi  za  bima  lakini  makala  yataeleza  kuhusu  bima  za  magari.  Na  hasa  bima ya  mhusika wa tatu ( third party insurance).

Tunahitaji  kujua  kwanini  magari  yakigongana  hata  iwe  kidogo  tu  kwa  pasi  watu  wazozane.  Kwanini  ulazimike  kumlipa  mtu pesa  nyingi  eti  kisa  umempiga  pasi.

Kwanini  mtu  akushinikize  kumlipa hapohapo kwenye ajali. Kazi  ya bima  ninini  na  unachoogopa  ninini mpaka ulazimike  kumlipa  mtu hela  nyingi  tena  kwa  unyonge mkubwa. Haya  yote  tutaona.

1.USIMLIPE  MTU  HELA.

Inapotokea  ajali  iwe  zile  ajali  kubwa  au  ndogo maarufu  kama   pasi  awali  ya  yote  tunahitaji kujua nani  kati  ya  madereva  wawili  ana  wajibu  wa  kutoa  taarifa  kwa  kampuni  ya  bima  husika.  Kujua  nani  anapaswa  kutoa  taarifa  tunahitaji  kujua  nani  aliyemgonga  mwenzake.  

Kimsingi  yule  aliyemgonga  mwenzake  ndiye  anapaswa  kutoa  taarifa   kwa  kampuni  ya  bima  husika.  Kama  ni  wewe  umesababisha  ajali  basi  yafaa  utoe  taarifa  kwenye  kampuni yako  ya bima.

Hii  ni  kwasababu  ikiwa  wewe  ndio  uliyegonga   gari  jingine  basi  kampuni  yako  ndiyo itakayotakiwa  kulipia  ile  hasara  na  sio  wewe. Kwahiyo  kutoa  kwako  taarifa  ni  kujiondoa katika dhima(liability) ya kutakiwa kulipa.

2.   NINI  UFANYE  IKIWA  ULIYEMGONGA  AMELETA  UBABE.

Wengi  wanaopata  ajali  za  kawaida  hasa  hizi  zinazoitwa  pasi   hupenda  kumalizana  na  wakati  magari  yao  yanazo  bima. Wakati  mwingine  yule  aliyegongwa  huomba  kiwango  kikubwa  cha  pesa  kuliko  hata   uharibifu  ulio  kwenye  gari  lake.  Lakini  kwasababu   aliyesababisha  ajali  huhisi  hana  namna  hulazimika  kutoa  kiwango  hicho.  Na  wakati  mwingine  mzozo  mkubwa  waweza  kutokea  na  badae  mtu  akalazimika  kulipia uharibifu  .

Lakini  iweje  ulipe  gharama  kubwa  na  wakati unalipia  bima  kila  mwaka. Unachotakiwa  kufanya  ni  kitu  kidogo.  Kama  unaona  kweli   umesababisha  ajali  mwambie uliyemgonga  kuwa   unawasiliana  na  bima  yako  na  bima  ndio  watakaolipa.

Hii  ndio  haki ya sheria  na  hawezi  kufanya   lolote    isipokuwa  kusubiri  bima  kulipa kwakuwa  sheria   ya  bima  za  magari  kwa  mtu  wa  tatu  ndivyo  inavyosema.

Kumalizana  naye  si  jambo  baya  lakini  vipi ikiwa  atahitaji  kiwango  kikubwa  cha   kukukomoa. Vipi   ikiwa  ataleta  ubabe na kutoelewana baada ya  ajali. Basi  ni hapo  tunaposema kwamba huna  haja  ya  kubishana au kugombana.

Ni  kumweleza tu kuwa  ndio  nimekugonga  lakini  gari  langu  linayo  bima,  na  bima  hiyo  ndiyo utakayo kulipa. Utakuwa  umemaliza  mchezo  na  mzozo.

3.  JITAHIDI  UPATE  TAARIFA  ZA  BIMA  YA GARI  ULILOGONGA.

Ikiwa  umegonga  gari  la  mtu    tumesema  bima  yako  ndio  itamlipa  uliyemgonga.  Kwahiyo  yule  uliyemgonga ndiye anayetakiwa  kupata  taarifa  za  bima  ya  gari  lako ili  alipwe. 

Lakini  mbali  na  hilo  ni  muhimu  pia  na  wewe  kuhakikisha  unapata  taarifa  za  bima  yake. Bima  inabandikwa  kwenye  kioo  hivyo  ni  rahisi  kupata  taarifa  hizo.
Umuhimu  wa  kupata  taarifa  hizo  ni  kuwa  inawezekana ukadhani   we  ndo  ulisababiasha  ajali  kumbe  baadae  labda  baada  ya  askari  kufika ikaonekana  yeye  ndiye  aliyekusababishia  wewe  ajali.

Ikitokea  hivyo na tayari   ukiwa  na  taarifa  za  bima  yake  basi  itakuwa  rahisi  kwako  kufuatilia  ili  sasa  wewe  ndio  udai   malipo  ya  uharibifu  wa  gari  lako.  

4.  KUCHUKUA  PICHA  ZA  AJALI.

Kwakuwa  siku  hizi kuna  simu  za  kamera   ni  vizuri  kuchukua  picha  za  ajali. Hizi  husaidia  kujua  nani  alisababisha  ajali .

Ni  ushahidi  unaoweza  kusaidia  gari  lako   kutengenezwa  na  bima  katika  wakati  ambao  ulishakubali  bima  yako  itengeneze  gari  la  mwenzako  na wewe  ujitengenezee  gari  lako,  hasa  kwa  bima  ya  mtu  wa  tatu ( third party  insurance).  Mengine  yataelezwa  makala  zinazofuata.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA     SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.      0784482959,        0714047241              bashiryakub@ymail.com


0 comments:

Post a Comment