NA BASHIR YAKUB -
Kutoa ushahidi wa uongo ni kosa. Ni kosa lenye adhabu kisheria. Ushahidi wa uongo ni pamoja na kupanga au kupangiwa la kusema mahakamani wakati mkijua kuwa sio la kweli. Kosa hili ni moja ya makosa yanayotendwa mno tena kiholela. Ni kawaida watu kupanga waseme nini mahakamani huku wakijua wanachopanga sio cha kweli.
Suala la ushahidi wa uongo halijalishi kesi ni ya aina gani. Iwe jinai au madai shahidi anawajibika kuwa mkweli daima. Kisichotakiwa ni kusema uongo ambao hupotosha usimamizi bora wa haki.
1.NAMNA YA KUWACHUKULIA HATUA SHAHIDI WAONGO.
Ni wajibu wa mtu wa upande wa pili katika kesi kuchukua hatua dhidi ya shahidi msema uongo. Ikiwa uko upande wa pili wa kesi na shahidi wa upande mwingine anatoa ushahidi wa uongo dhidi yako ni wajibu kwako kuchukua hatua haraka sana.
Hatua inayofaa ni hii ya kutoa taarifa polisi au kwa hakimu/jaji husika ili kumfungulia mashtaka shahidi kwa kusema uongo.
2. KOSA LA KUTOA USHAHIDI WA UONGO KATIKA SHERIA.
Kifungu cha 102 cha Kanuni za adhabu kinasema kuwa mtu yeyote wakati wa kufungua shauri au wakati shauri likiendelea, kwa kujua akatoa ushahidi wa uongo kuhusu suala lolote katika kesi atakuwa ametenda kosa.
Hiki ndicho kifungu cha sheria kinacholitangaza tendo la kutoa ushahidi wa uongo kuwa kosa( perjury).
3. HAIJALISHI USHAHIDI ULITOLEWA KWA KIAPO AU BILA KIAPO.
Kawaida upo ushahidi unaotolewa kwa kiapo na upo usiotolewa kwa kiapo. Ushahidi kutolewa kwa kiapo ina maana shahidi ataapa kabla ya kusema lolote kama shahidi. Na bila kiapo shahidi hataapa.
Kwahiyo iwe ushahidi ulitolewa kwa kiapo au bila kiapo ikiwa ni wa uongo hakuna kinga isipokuwa litakuwa kosa tu. Wapo wanaodhani ukitoa ushahidi bila kiapo basi hata uwe wa uongo itakuwa haina shida. Si kweli kosa linabaki palepale.
4. USHAHIDI UWE WA MDOMO AU MAANDISHI BADO NI KOSA.
Ushahidi waweza kutolewa kwa namna mbili. Unaweza kutolewa kwa mdomo au kwa maandishi. Ushahidi kwa mdomo ni pale mtu anapohojiwa na akazungumza mbele ya mahakama.
Wakati ule wa maandishi ni ule unaotolewa kwa kuandika.Shahidi anaweza kuandika mwenyewe au wakili wake nje ya mahakama. Kisheria huu wote ni ushahidi na wajibu wa kusema kweli unabaki palepale.
5. KUSAIDIA AU KUSHAURI KUTOA USHAHIDI WA UONGO NALO NI KOSA.
Kifungu cha 102 ( 2 ) cha kanuni za adhabu kinasema kuwa mtu yeyote ambaye atasaidia , atashiriki, atashauri, atatuma au kushawishi mtu mwingine kutoa ushahidi wa uongo atakuwa ametenda kosa la kushawishi kutoa ushahidi wa uongo.
Huyu hatashitakiwa kwa kutoa ushahidi wa uongo bali kushawishi kutoa ushahidi wa uongo.
6. ADHABU YA KUTOA USHAHIDI WA UONGO.
Kifungu cha 104 cha kanuni za adhabu ndicho kinachotoa adhabu kwa yote mawili, yaani kutoa ushahidi wa uongo na kushawishi kutoa ushahidi wa uongo.
Kinasema kuwa mtu yeyote ambaye atatenda kosa la kutoa ushahidi wa uongo au kushawishi kutoa ushahidi wa uongo atawajibika kwa adhabu ya kifungo cha miaka saba.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA HABARI LEO KILA JUMANNE , GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI NIPASHE KILA JUMATANO. 0784482959, 0714047241 bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment