Monday 18 April 2016

FIDIA YA KUVUNJWA MKATABA.

Image result for mkataba wa kazi

NA   BASHIR  YAKUB- 

Kuvunjwa  kwa  mkataba  ni  kutotekeleza   kwa  matendo  yale  yaliyokubaliwa  ndani  ya  mkataba/makubaliano. Hatua  ya  kushindwa  kutekeleza  makubaliano  ndio  kuvunjwa  kwa  mkataba. Unapomuuzia  mtu  kitu  akalipa  kiasi  na  kiasi  akaahidi  kulipa  ndani  ya  siku  saba  na  zikapita  bila  kulipa  basi  amevunja  mkataba.

Unapokubaliana  na  mtu  kuleta  bidhaa  ya  kiwango  fulani  halafu  akaleta  bidhaa  iliyo  chini  ya  kiwango  au  chini  ya  idadi  amevunja  mkataba. Kuvunjwa   kwa  mkataba  kunajitokeza   katika ngeli  nyingi. Kwa  mfano  muda  ni  sehemu  ya  mkataba na  hivyo  jambo  halitakiwi  tu  kutekelezwa  kama  lilivyoainishwa  ndani  ya  mkataba  bali  pia  linapaswa  kutekelezwa  katika  muda  uliokubaliwa.

1.NAMNA  MBILI  ZA  KUVUNJWA  KWA  MKATABA.
Mkataba  unaweza  kuvunjwa  kwa  namna  kuu  mbili,  kwa  matendo  au  maneno.

(  a )  Kuvunjwa  mkataba  kwa  maneno. Hii  ni  hatua  wakati  ambapo  mmoja  wa  wahusika  katika    mkataba  husema   wazi  kuwa   anaachana  na  mkataba  na  hataendelea  nao.  Kusema  kwa  maneno   hujumuisha  hata  maandishi  ambapo  mhusika  ataandika  na  kusema  hawezi  tena  kuendelea  na  mkataba.

( b ) Kuvunjwa  kwa  matendo.  Hii  ni  hatua  ambapo  mhusika  katika  mkataba   anavunja  mkataba  bila  kusema  wala  kuandika. Matendo  yake  tu  huashiria  kuwa  amevunja  mkataba.

Kwa  mfano  kutotekeleza  kile  kilichokubaliwa   huhesabika  kama  kuvunja  mkataba  kwa  matendo.  Umeahidi   kuleta  gunia  miamoja   za  mahindi  kwa  bei  fulani  na  sasa  muda  umeisha  na  gunia  ulizoleta  ni  40. Umevunja  mkataba  kwa  matendo.

Kwahiyo  kitendo cha kushindwa  kutekeleza  kilichokubaliwa   lakini  bila  kesema  kwa  maneno/maandishi  kuwa  umevunja  mkataba  ndiko  kuvunja  mkataba  kwa   matendo( implied breach).

2.  NANI  ANAWEZA  KUDAI  FIDIA  YA  KUVUNJWA  KWA  MKATABA.

Mkataba  mara  nyingi  huwa  na pande  mbili  au  zaidi. Si  kila  upande  katika  pande  hizi  hustahili  kudai  fidia  ya kuvunjwa  kwa  mkataba. Fidia  ni  haki  ya  yule aliyevunjiwa  mkataba. Aliyevunjiwa  mkataba  ni  yule  aliyeathirika  kutokana  na  kuvunjwa  kwa  mkataba.

3.  FIDIA HUTOLEWA PALIPO  NA  HASARA  TU.

Ili  mtu  aweze  kulipwa  fidia  kutokana  na  kuvunjwa  mkataba  ni  lazima  kuwe  kuna hasara  ya  moja  kwa  moja  aliyoipata  kutokana  na  kuvunjwa  huko. Yawezekana  mtu  akavunja  mkataba  lakini  pasiwe  na  hasara  yoyote  iliyopatikana. Kwa  hapo  ni  vigumu  kudai  fidia.  

Fidia  hutolewa  kwa  madhara.  Tena  madhara  yenyewe  ni  yale  ya  moja  kwa  moja.  Yasiwe  yale  madhara  yaliyo  mbali  na  athari  za  kuvunjwa  mkataba.
Mfano  wa madhara  yaliyo  mbali ni  pale utakapokubaliana  na  mtu  kuwa saa  7 kamili  za  mchana awe  ameleta  gunia 40 za mahindi na  muda  ukafika  akawa  hajaleta. 

Ukiamua  kumfuata huko aliko na  katika  kumfuata  ukapata ajali huwezi  kusema  akulipe  fidia  ya  ajali  kwa  kuwa alivunja  mkataba hakufika  kwa  wakati  hatua  iliyokufanya  umfuate. Hayo  ni madhara  yaliyo mbali.

Isipokuwa  atakulipa  fidia  ikiwa amefika baada  ya saba na  wewe  wateja  wako  wakawa  wameondoka  na  hivyo ukawa  huna  sehemu  nyingine  ya  kuuza  mzigo. Kwa hili madhara  yako  karibu  na  atatakiwa  kulipa  fidia  ya  hasara.

4.  ENDAPO MKATABA UNAELEZA  FIDIA.

Wapo  watu  makini  ambao  katika  mikataba  yao  hueleza nini  kitatokea  iwapo  upande  mmoja  utavunja  mkataba.  Hili  huwa  ni  jambo  zuri  sana  kwakuwa  hupunguza  utata  pale  mkataba  unapokuwa  umevunjwa  tayari. 

Huwa  inaandikwa  katika  mkataba  kuwa  endapo   upande  fulani  utashindwa  kutekeleza  hili  na  lile  basi  utatakiwa  kulipa  kiasi  fulani  kama  fidia, adhabu au hakutakuwa na malipo yoyote.

Ikiwa  mkataba  utakuwa  unaelekeza lolote kati ya haya  basi huwa  hakuna  jingine  isipokuwa  hicho  kilichoandikwa kitatakiwa  kufuatwa.

5.  USHAURI.

Ni vema  sana  kuzingatia  vipengele  vya  mkataba   wakati  mnaposainishana  ili  kuondoa  utata  pale  linapojitokeza  jambo. Ni vema  ukawasiliana  na  mwanasheria  katika  eneo  lako  nyakati  zote  mbili. 

Wakati  wa  kuandaa   vipengele  vya  mkataba(terms),   na  wakati  wa  kusaini  mkataba.  Hii  itakuwezesha   kuingiza  vipengele  vya  kitaalam vinavyolinda  maslahi  yako  katika  mkataba.


MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA     SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.      0784482959,        0714047241              bashiryakub@ymail.com

0 comments:

Post a Comment