Tuesday 8 March 2016

SHERIA HAIKATAZI KUFUNGA NDOA IWAPO MMOJA WA WANANDOA HAYUPO.

Image result for harusi

NA BASHIR  YAKUB - 

Mtu  mmoja  aliyeko  Zurich  alipiga  simu  akiuliza  swali  ambalo  ni  kichwa  cha  haya  makala .   Yeye  yuko  zurich  lakini  anataka  kufunga  ndoa  na  mwanamke  aliyeko  Tanzania  bila  kulazimika  kurudi  nchini. Anataka  afunge  ndoa  akiwa  hukohuko zurich  na  mwanamke  akiwa  Tanzania .

Alisema  huko  aliko  jambo hilo linaruhusiwa  kisheria  ila  wasiwasi  wake  ni  kama  hata  Tanzania  jambo  hilo linaruhusiwa.  Kabla  ya  kutizama jambo  hilo  kisheria upo  umuhimu  pia wa  kutizama  baadhi  ya  mambo  kuhusu  ndoa.

1.NINI  MAANA  YA  NDOA.

Kwa  mujibu  wa  kifungu  cha  9( 1 )  cha  sheria  ya  ndoa  sura  ya  29,  ndoa imetafsiriwa  kama  muungano  wa  hiari  kati  ya  mwanamke  na  mwanaume   wenye  lengo  la  kudumu  maisha  yao  yote.

2.  SHERIA  INASEMAJE  KUHUSU WAZAZI   KUCHAGUA  WACHUMBA.

Katika  maana  ya  ndoa  kuna  neno  hiari. Hili  ni  jambo  la  kwanza  katika  ndoa. Maana  yake  ni kuwa kusiwe  na  kulazimisha,  ulaghai,  udanganyifu n.k. Hata  kurubuni  kunakolenga  kuondoa  hiari  ya  mtu   nako  ni  kulazimishwa. Pia   wazazi  kuwachagulia  vijana  wao  wachumba  na  kuwashinikiza  kuwaoa  au  kuolewa  nao  nako  ni kuondoa  hiari  ya  wahusika.

Si  kosa  mzazi  kuona mchumba  kwa ajili  ya kijana  wake isipokuwa  ni  kosa akitumia  nafasi hiyo   kulazimisha/kushinikiza  kufungwa  ndoa. Haya  ni  kwa  mujibu  wa  kifungu  cha  16  cha  sheria  ya  ndoa.

3.  JE  NDOA  YA   MKATABA  INARUHUSIWA ?.

Lengo  la  ndoa  lazima  liwe  ni  kuishi  wote  katika  maisha  yao  wote.  Hii  ni  kwa  mujibu  wa  kifungu  cha 9( 1 ). Maana  ya  hili  ni kwamba kusiwe na  ndoa  za  mikataba.  Ndoa  za  mikataba  ni  kwamba  mnafunga   ndoa kwa  muda  maalum  mtakaoona  unafaa  yaweza  kuwa  miaka miwili, mitatu,  minne  au  zaidi  kadri  wahusika  watakavyokubaliana.  Hapa kwetu ndoa  lengo lake  ni  iwe  maisha  yote. 

Hata  hivyo  talaka  inaruhusiwa. Hivyo basi  haiwezekani  kufunga ndoa kwa  muda  maalum  hapa  Tanzania.

4.  JE SHERIA  INASEMAJE  KUHUSU  NDOA  ZA  JINSIA  MOJA.

Kifungu  cha  9 ( 1 )  kimesema  kuwa  ndoa  ni  muungano  kati  ya  mwanamke  na  mwanaume.  Maana  yake  ni  rahisi  tu kuwa  hakuna ndoa  kati  ya  mwanamke  na  mwanamke au  mwanaume na  mwanaume.  Uingereza,  marekani  na  baadhi  ya nchi  za  ulaya  sheria  zimeruhusu  ndoa  za  jinsia  moja.  Sisi  kwetu  hilo ni  haramu  kabisa.

5.  UMRI  WA  KUOA  NA  KUOLEWA  NI  UPI.

Kwa  ujumla  umri  wa kuoa  au  kuolewa  ni  miaka  18.  Hata  hivyo  mwanamke  mwenye  umri  chini  ya  miaka 18  anaweza  kuolewa  ikiwa  atapata  ridhaa kutoka  kwa  baba,  au  mama  na  kama  wote  wamefariki  basi  ridhaa hiyo  itatolewa  na  mlezi  wake. Hii  ni  kwa  mujibu  wa kifungu  cha  17)( 1 ) cha  sheria  ya  ndoa.

6. JE YAWEZEKANA KUFUNGA  NDOA  PASI  NA  KUWEPO  MWANAUME.

Ndio  inawezekana.  Na  si  mwanaume  tu  bali yoyote  anaweza  asiwepo  kati  ya mwanaume  au  mwanamke. Inaruhusiwa   siku  ya  ndoa  kuwapo  na  mmoja  tu  kati ya  wanaotarajiwa  kufunga  ndoa .Anaweza  kuwa  mwanaume    au  mwanamke.  Ndoa  haibatiliki( become  void) kwa  kutokuwepo  mmoja  wa   wahusika.  Hili  si  katika  mambo  yanayobatilisha  ndoa.

Kwahiyo  inawezekana  mwanaume  akawa  Zurich  na  mwanamke  yuko  Tanzania  na  ndoa  ikafun gwa  Tanzania.  Sharti  la  kisheria  la  hatua  hii  ni  kuwa  yule  asiyekuwepo  awakilishwe( represented) na  mashahidi/shahidi  aliyempa  ridhaa.

Anachotakiwa  kufanya  yule  asiyekuwepo  ni   kuwapa  ridhaa  mashahidi/shahidi  ambao  ndio  watakwenda  kusimama  badala yake. Ndoa  itafungwa  na  kila  kitu  kitakuwa  halali.  Lakini  izingatiwe  kuwa mamlaka  ya  uwakilishi  yanaishia  katika kufunga  ndoa. Uwakilishi  mwingine  baada  ya  ndoa  hautaruhusiwa. Haya  ni  kwa  mujibu  wa  kifungu  cha  38 ( 1 ) ( j )  sheria  ya ndoa  sura  ya  29.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA     SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.      0784482959,        0714047241              bashiryakub@ymail.com





0 comments:

Post a Comment