Monday, 7 March 2016

JE KUKATAA KUPOKEA SUMMONS KUNA MADHARA GANI KISHERIA ?.NA  BASHIR  YAKUB -

Summons  ndio  wito  maalum  wa mahakama. Mara  zote  unapofuguliwa  mashtaka ( unaposhtakiwa) hasa  mashtaka  ya  madai  basi   ili  uweze  kufika  mahakamani  na  kujua  mashtaka  yanayokukabili yaipasa  mahakama  kutuma wito  maalum  ambao  kwa  jina  la kitaalam  ndio  huitwa  “summons”.

1.KWANINI  WATU  HUKATAA  KUPOKEA/KUSAINI   WITO   HUU.

Mara  nyingi wito  huu  unapotumwa baadhi  ya  watu  hukataa kabisa  kuupokea na wengine  huupokea  lakini  hukataa  kuusaini.  Zipo  sababu  ambazo  huwafanya  watu  wasipokee  wito  huu : 

( a ) Kwanza  ni  imani  kuwa  usipopokea  wito  basi  shauri  ulilofunguliwa  haliwezi  kuendelea.

( b ) Sababu  nyingine  ni   kuamini  kuwa  ukikataa  kupokea  wito  utakuwa  umejitoa  katika  hatia(liability)  ya  kutambua  chochote  kinachoendelea  hivyo   chochote  kilichopo  mahakamani  kitakuwa  hakikuhusu.             

( c ) Pia  wengine  hukataa  kupokea  wito  kwa  kuamini  kuwa kupokea  wito  ndio  kukubali  shitaka  na   hivyo  ni  bora  kuukataa  kwa  kuwa  kufanya  hivyo  itakuwa  ni  kukana  shitaka. Tutaona  hapa  chini  kama imani  hizo   zina  ukweli  wowote.

2. JE KESI  HAIWEZI  KUENDELEA KWASABABU  UMEKATAA  KUPOKEA WITO.?    

Jibu  ni  hapana  kukataa  kwako  kupokea  wito  hukuzuii  shauri  lililofunguliwa  kuendelea.  Na  hii  ni  athari  ya  kwanza  kabisa  anayoipata  mtu  aliyekataa  kupokea  wito.  Mtu  anapokataa  kupokea  wito  basi  yule  aliyetumwa  kupeleka  wito  huo atatakiwa  kuapa  kuwa  alimpelekea  fulani  wito  na  akakataa  kuupokea.

Baada  ya  kiapo  hicho  atarejesha  taarifa za  kukataa  kupokelewa  kwa  wito  huo  mbele  ya  hakimu/jaji  husika aliyepangiwa  kesi  hiyo.  Sambamba  na  hilo  ataambatanisha  kiapo  chake  kuonesha  kukataliwa  kupokelewa  wito huo.  Baada ya  hakimu/jaji  husika  kupokea  taarifa  hizo  basi  ataamuru  shauri  kuendelea  upande  mmoja(kama ataona inafaa).  

Shauri  kuendelea  upande  mmoja maana  yake  ni  kuwa  shauri  litaendelea  bila  uwepo  wa  yule aliyekataa  kupokea  wito.
Kwa  hiyo  jibu  la  swali  hili  ni kuwa  kukataa  kupokea  au  kusaini  wito  hakuzuii  kesi  kuendelea.

3. JE  KUPOKEA /KUSAINI  WITO  NI  KUKUBALI  SHITAKA ?.

Hapana  siyo  kweli  hata  kidogo. Unapokubali  kupokea  wito  au  kuusaini  haimaanishi  kwa  namna  yoyote  kuwa  umekubali  shitaka. Hakuna uhusiano  wowote  kati  ya  kupokea/kusaini  wito  na  kukubali  mashtaka. Kupokea/kusaini   wito  maana  yake  ni  kuthibitisha  tu  kuwa   umeona  kuwa unaitwa.

Masuala  ya  kukubali  kosa  au  kukataa  yapo  mahakamani .  Ni  pale  unapokuwa  mahakamani  au  wakati  wa  kujibu  mashtaka  kwa  maandishi  ndipo  unapoweza  kukubali au  kukataa  kosa. Kwahiyo  hakuna  haja  ya  kukataa  kupokea/kusaini   wito kwasababu hiyo.

4. MADHARA  YA  KUKATAA  KUPOKEA/KUSAINI  WITO.

(  a ) Athari  ya kwanza  kabisa  ni  kuendelea  kesi  bila  kuwepo  kwa  aliyekataa  kupokea  wito.  Kuendelea  kwa  kesi  upande  mmoja  ni kupatikana  kwa  hukumu  ya  upande  mmoja.

Na  mara  nyingi  hukumu  za  upande  mmoja  ni  lazima  tu  aliyekataa  kufika  mahakamani  awe  ameshindwa. Kwahiyo  madhara  makubwa  kabisa  yanayopatikana  ni kushindwa  kesi  na  kupoteza  kabisa  hata  kile  kidogo  ambacho  alitakiwa  kukipata.

Sio  rahisi  kesi  ikasikilizwa  upande  mmoja  halafu aliyesikilizwa  akashindwa. Bali  ambaye  hakufika  mahakamani  ndiye  atakayekuwa  ameshindwa.

( b ) Madhara  mengine  makubwa  ni  kukosa  kusikilizwa.  Unapokataa  kupokea  wito/kuusaini  maana yake  ni  kuwa  hautofika  mahakamani. Usipofika  mahakamani  maana  yake  ni  kuwa  umejinyima  haki  ya  kusikilizwa. Kumbuka  uzoefu  huonesha  kuwa  siku  zote  mpeleka  mashtaka  huwa  ana kawaida ya kusema  vitu  vingi  vya  uongo  na  uzushi  dhidi  ya  mshitakiwa.

Unaposhindwa  kupokea  wito  na  hivyo  kutofika  mahakamani  basi  hakuna  mtu  wa kufika na kukana  uongo  na  uzushi  kwa  niaba  yako. Utaifanya  mahakama  na umma kuamini  kila  kinachosemwa  na  utakuwa  umekosa  nafasi  ya kupinga na  kuonesha  kusingiziwa.

( c ) Pia upo  katika  hatari  ya  kupoteza  mali  ikiwa  mlalamikaji  aliyefungua  kesi  anadai  kitu  kutoka  kwako. Ikiwa  anadai  mali kama ardhi,nyumba, gari,  baiskeli, mifugo,  na  mali  nyingine  yoyote basi  upo  katika  hati hati  ya  kupoteza  hata  kama  ilikuwa  ni haki  yako.

Hii  ni  kwakuwa  haukufika  mahakamani  na  hivyo umetoa  nafasi  ya  ushindi  kwa  mlalamikaji  ambaye  katika  kukaza  hukumu(execution)  ataomba  kupatiwa  ile  mali  na  mahakama  itamteua  dalali  wa  kuhakikisha  unakunyanganya  ile  mali  na  atakabidhiwa  mlalamikaji/mshitaki.
MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA     SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.      0784482959,        0714047241              bashiryakub@ymail.com
1 comments:

  • Nsolo S. Stephen says:
    7 March 2016 at 03:28

    Je, aliyekataa kupokea au kusaini WITO huo hawezi kutiwa hatiani kwa kudharau mahakama?
    Je, asipopokea au kutosaini WITO lakini akafika shaurini, itakuwaje?

Post a Comment