Tuesday 15 March 2016

KUUZWA MALI ZA MAREHEMU KULIPIA DENI LAKE.

Image result for maLI ZAKE


NA  BASHIR  YAKUB -

Marehemu  atakapokuwa   ameacha  shauri  mahakamani  ambalo  alikuwa  anashtakiwa nalo  kabla  ya  kufa  kwake  basi  hukumu  itakapotoka  itatakiwa  kutekelezwa.  Hapa  tunaongelea  hukumu  itokanayo na mashauri  ya  madai. Sambamba na  hilo makala  yataangalia  pia mambo  kadhaa  yanayohusu  kifo  cha  mtu  ambaye  alikuwa  akishitakiwa/akilalamikiwa  mahakamani kabla  ya  kifo  chake. Amri  ya  xxii  kanuni  ya  1 – 12  ya  sheria  ya  mwenendo  wa  mashauri ya madai  ndiyo  itakayotuongoza.

1.JE MSHITAKIWA  AKIFA  NA  KESI  ITAKUFA.

Kanuni  za  jumla (general rule)   ni  kwamba  shauri  hutakiwa  kufunguliwa  na  mtu  aliye  hai  dhidi/akimshitaki  mtu  aliyehai. Hii  ni  kanuni  ya  jumla  yenye  kumaanisha kuwa  mtu  aliyekufa  hawezi  kushtaki  wala  kushtakiwa. Hata  hivyo  kwenye  kanuni  za  sheria  pale  penye  kanuni  ya  jumla( general rule)  huwa  kuna  vinginevyo( exception).  Hii  ina  maana  yapo  mazingira  ambapo  mshitakiwa  atakufa  lakini  kesi  yake  haitakufa  itaendelea.

2. KESI KUENDELEA HATA  BAADA  YA  KIFO  CHA  MSHITAKIWA/MLALAMIKIWA.

Ikiwa  marehemu  alikuwa  ameshtakiwa/amelalamikiwa   katika  kesi  ambazo  zinahusu  mali  kama  nyumba, gari, kiwanja  na  mali  nyinginezo   na  akafa kabla  ya  kesi  hiyo  kuisha  basi  kesi  hiyo  itaendela.  Pia  ikiwa  alishitakiwa  katika  mashtaka yanayohusu   masuala  ya  mikataba  pia  kesi  hiyo nayo  itaendelea.

3.KUTOENDELEA  KESI BAADA  YA  KIFO  CHA  MSHITAKIWA.

Ikiwa mashitaka  aliyoshitakiwa  nayo  marehemu  yalikuwa  ni  mashtaka  binafsi   basi  kesi  hiyo  haitaendelea. Mashtaka   binafsi (personal)  ni  kama mashtaka  ya  kudai  fidia  baada  ya  kudhalilishwa, kupigwa, kutukanwa n.k.,  Mashtaka  ya  namna  hii ni mashtaka  yenye  viashiria  vya  ubinafsi ( individuality)  na  hivyo hufa  pale  tu  mshitakiwa  anapokufa.

4.NDUGU  WA  MSHITAKIWA  KULAZIMIKA  KURITHI  MASHTAKA.

Ikiwa  mshitakiwa  amefariki  lakini  ikawa  kesi  yake bado  ina  hadhi  ya  kuendelea  kutokana  na  mashitaka  yaliyokuwa  yakimkabili  basi  ndugu  wa  marehemu    watalazimika  kusimama  kama  washitakiwa  na  kuendeleza  ile  kesi.

 Amri  ya xxii kanuni  ya 4 ( 1 )  ya sheria  ya  mwenendo  wa  madai  inasema  kuwa  mshitakiwa  anapokuwa  amefariki  na  shauri  likatakiwa  kuendelea  basi  mahakama  itawezesha   mwakilishi  wa  marehemu mshitakiwa  kusimanma  badala  ya  marehemu .

5. KUUZWA  MALI  ZA   MAREHEMU  KULIPIA  DENI .

Hapa  ni  deni  lile  litokanalo  na  hukumu.  Ikiwa  kesi  imeendelea  na  hatimaye  kutolewa  hukumu/maamuzi  basi  utaratibu  wa  kulipa  ikiwa  kesi  inahusu  kulipa  utafuata.  Lakini  pia  kama  kesi  inahusu  kurudisha  mali  fulani  kama  nyumba,kiwanja  basi  kitatakiwa  kurudishwa   hata  kama  marehemu  alikirithisha  katika  wosia.

6. ULAZIMA WA  NDUGU  KUCHUKUWA  KESI  YA  MAREHEMU  MSHITAKIWA.

Ulazima  wa ndugu   wa  marehemu kurithi mashtaka  yaliyokuwa  yakimkabili  ndugu  yao  unatokana  na ukweli  kuwa  ikiwa  watakataa  kutokea  na  kusimama  kama  washitakiwa  wapya na kuendelea  kutetea  kesi   iliyokuwa  ikimkabili  marehemu  basi kesi  itaendelea  na  upande  mmoja  uliopo  yaani  upande  wa  walalamikaji  na  hukumu  itatolewa.  

Hukumu  itakapotolewa  utafuata  utekelezaji  ambapo   mali  alizoacha marehemu  ndizo  zitakazotumika   kulipia  kile  kinachotakiwa.
Kama  ni  nyumba au  kiwanja  na  kinatakiwa  kurudishwa  basi  kitarudishwa  hata  kama  ndugu  wameishagawana.  Kwahiyo  ni  muhimu  basi  ndugu  kujitokeza  na  kusimama  kama  washitakiwa  wapya  katika  kesi  za  namna  hiyo. Kujitokeza  ni bora  kwakuwa  kunaweza  kubadili matokeo  tofauti  na  kutokujitokeza.  Kutokujitokeza maana yake ni  nyepesi tu kuwa mmempa  ushindi mlalamikaji  na  kwahiyo  muwe  tayari kunyanganywa  mali  za  marehemu  hata  kama  mmegawana  tayari.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA     SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.      0784482959,        0714047241              bashiryakub@ymail.com


0 comments:

Post a Comment