Wednesday, 16 March 2016

JE NI KOSA MKOPAJI KUTOSEMA KAMA ANA MKE/MME WAKATI AKICHUKUA MKOPO.

Image result for MKOPO


NA  BASHIR   YAKUB -

Mara  kadhaa  tumeeleza  mambo  mbalimbali  ya kisheria kuhusu  mikopo , waomba mikopo  na  watoa  mikopo.  Haki  na  wajibu  ni  vitu  ambavyo  mara  nyingi  vimeguswa. Hii  ni  kwasababu  eneo  hili  ni  katika  maeneo  tata.

Ni tata kwa  pande  zote  yaani taasisi  za  fedha halikadhalika  wachukua  mikopo.  Iko  sintofahamu  nyingi  hasa  kwa  wachukua  mikopo. Mara  nyingi  hawa  hujikuta  katika  matatizo   na  wakati  huo  eti  ndio  hufahamu  haki   na  wajibu  wao.

Baada  ya  tatizo  kutokea  ndipo  hujua  walitakiwa  kufanya nini  huko  nyuma. Bahati  mbaya muda  huo huwa  wamechelewa  tayari.

1.SUALA  NA  KUWA  NA  MKE/MME WAKATI  WA  KUCHUKUA  MKOPO.

Wakati  wa  kuchukua  mkopo  ni  wakati  ambao  taasisi  inayotoa  mkopo  humtahini ( interview)  mchukua  mkopo. Kila  taasisi  yaweza  kuwa  na  maswali  ambayo  yana tofauti  na  taasisi  nyingine. Maswali hutokana na   na taarifa ambazo  taasisi ingependa  kujua  kutoka  kwa  mchukua  mkopo.

Hata  hivyo  pamoja  na  utofauti  huo bado   yapo  maswali  ya  msingi ambayo  kila  taasisi  utakayoenda  kuchukua  mkopo  ni  lazima  utaulizwa.  Haya  ni  yale  yatokanayo  na  sheria zinazohusu  masuala  ya  mikopo.  Ni maswali  yanayofanana( common  questions).

Moja  ya  maswali  haya  ni  swali  hili   la  kutaka  kujua  kama  muomba  mkopo  ana  mwenza kwa  maana  ya  mke  au  mme.  Hili  ni  swali  la  kisheria  ambalo   lina  athari  na  matokeo  ya  kisheria  kama  tutakavyoona  hapa .

2.UPI  UMUHIMU  WA  KUJUA IWAPO MWOMBA  MKOPO  ANA  MME/MKE.

Hii  ni  kwasababu  unapochukua  mkopo   mara  nyingi  hutakiwa  kuweka  rehani.  Na  rehani  inayokubalika  huwa  ni  mali  isiyohamishika  ambayo  ni  nyumba au  kiwanja. Na  mara  nyingi nyumba  au  kiwanja  ni  mali  ambazo  huhesabika  zinamilikiwa  kwa pamoja kati ya  mme  na  mke  ikiwa  wameoana.

Kwa  maana  si  ruhusa  kwa  mmoja  wa wanandoa  hao  kuweka  rehani  mali  hizo  bila  mwingine kuridhia. Na  ikitokea  kuwa mmoja  hakuridhia  basi  hupata  haki  ya kusitisha  mali  hiyo  kuhusishwa  katika  mkopo.

Hatua  hiyo  inaweza  kuwa  hasara  kwa  mtoa  mkopo. Basi  kutokana  na  hilo huibuka  umuhimu mkubwa  wa  kujua  iwapo  mwomba  mkopo   ana  mke/mme.

3.NI  WAJIBU  WA  NANI  KUTAFITI  KAMA  MWOMBA  MKOPO  ANA  MKE/MME.

Hapo  awali ilikuwa  ni  wajibu  wa  taasisi  inayotoa  mkopo  kufanya  utafiti  na  kupeleleza  ikiwa  kama  mwomba  mkopo  ana  mke au  mme. Hili  lilikuwa   ni  sharti  kutoka  sura  ya  113  sheria  ya  ardhi  kifungu 114.

Hata  hivyo  baadae  kifungu  hiki  kilibadilishwa  na  kifungu  cha  8 cha  sheria  ya  rehani  ya  mikopo ya mwaka 2008 ambacho  sasa  kinatoa  wajibu  huo  kwa  mwomba  mkopo  kueleza  ikiwa  ana  mke/mme  kabla  ya  kuweka  ardhi  rehani.
Taasisi  inayotoa  mkopo  imepewa  wajibu  mwepesi  tu  wa  kujiridhisha  na  taarifa  hiyo.

Katika  kujiridhisha  kifungu kidogo  (3) kinasema  kuwa taasisi  ya  mikopo  itatakiwa  kumuapisha  mwomba  mkopo  kwa  kile  anachosema. Ikiwa  ataapa  uongo  kwa  kusema  hana  mke/mme  wakati anaye basi  tutaona  sheria  imesemaje.

4.KUTOA  TAARIFA  YA  UONGO KUWA  HUNA MKE/MME WAKATI WA KUCHUKUA  MKOPO.

Kifungu  kidogo  cha  ( 4 )  cha sheria  ya  rehani za  mikopo kinasema  kuwa  iwapo  mwomba  mkopo  atasema  mathalani  kuwa  hana  mke/mme  na  akapewa  mkopo  basi  atakuwa  ametenda  kosa  ambalo  linastahili  adhabu. Adhabu  yake  ikiwa  itathibitika  ni  kulipa  faini  ambayo  thamani  yake  sio  chini  ya  nusu  ya  pesa  ya  mkopo  iliyochukuliwa. 

Ikiwa  zilichukuliwa  milioni  mia  basi  faini  yake  itaanzia  milioni  khamsini  kwenda  mbele.

Mbali  na  adhabu  hiyo  pia  mahakama  inaweza  kuamuru  mchukua  mkopo  kwenda  jela  kwa  kifungo  kisichopungua  miezi  kumi  na  mbili. Maana  yake  anaweza  hukumiwa  miezi  12  au  zaidi  kutegemea  na  uzito  wa  mazingira  ya kilichotendwa.
MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA     SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.      0784482959,        0714047241              bashiryakub@ymail.com



1 comments:

Post a Comment