Tuesday 2 February 2016

ZIJUE AINA SABA ZA ADHABU ZINAZOTOLEWA NA MAHAKAMA.


Tokeo la picha la MAGEREZA
NA  BASHIR  YAKUB  -

Adhabu  hizi  zimeainishwa  kifungu  cha  25 cha  kanuni  za  adhabu  sura  ya 16. Ni  adhabu  zinazohusu  makosa  ya  jinai.

1.ADHABU  YA  KIFO ( DEATH PENALTY).

Adhabu  hii  hutolewa  kwa  wenye  makosa  makubwa  kama  kuua  kwa  kukusudia(murder).  Kifungu  cha  26  kanuni  za  adhabu  kinasema  kuwa,  mtu  atakapohukumiwa  adhabu  ya  kifo  basi  adhabu  hiyo itatekelezwa  kwa  kunyongwa  kwa  kitanzi  mpaka  mtu  huyo  atakapokufa.

Hata  hivyo  adhabu  hii  hutekelezwa  kwa  namna tofauti   katika nchi mbalimbali. Baadhi  ya nchi  adhabu  ya kifo  hutekelezwa  kwa  kupiga  risasi   na  nyingine  kudungwa  sindano  ya  sumu. Sisi  kwetu  ni  kitanzi/kamba  shingoni  kwa kuninginizwa mpaka roho  itoke. 

 Pamoja  na  hayo  adhabu  hii  inapingwa  sana  na  mashirika ya  haki  za  binadamu  pamoja  na  wanaharakati wengine duniani kote.

2. ADHABU YA  KIFUNGO ( IMPRISONMENT).

Adhabu  ya  kifungo  hutolewa  kwa  muda  tofauti  kutegemea  na aina  ya  kosa  alilotenda mtu.  Yapo  makosa  watu  hufungwa  miaka  saba,  mwaka  mmoja,  miezi, miaka  thelathini lakini  pia  kipo  kifungo  cha  maisha.  Kifungo  kimegawanyika  mara  mbili.

Kipo  kifungo  cha  ndani  na  kipo  cha  nje. Kifungo  cha  ndani  ni  kifungo  ambacho mtu anakuwa   ndani  ya  uzio  maalum  ambao  haruhusiwi  kutoka  huku  ukihudumiwa  na  askari  magereza.  Hii  huitwa  jela ( jail). Hataruhusiwa  kutoka  humo  mpaka  muda  maalum  utakapoisha. Aidha  kifungu  cha  nje wakati  mwingine  huitwa  kifungo  cha masharti.

Ni kifungo  ambacho  mtuhumiwa  hazuiliwi  katika  jela isipokuwa  atapewa  masharti  kadhaa  atakayotakiwa  kutekeleza akiwa  nje  ya  jela.  Anaweza  kuwa  anaishi  nyumbani  kwake   lakini  kwa  sharti la kuripoti  sehemu  fulani  kila  siku au  vinginevyo, anaweza  kuzuiwa  kusafiri  nje  ya  mkoa  wilaya  au  vinginevyo, anaweza  kupewa  sharti  la  kutotenda  kosa  ndani  ya  mwaka, miaka  au  vinginevyo  n.k. Kubwa  hapa ni  kuwa  kifungo hiki  mtu  anakuwa  nje  lakini  kwa  masharti maalum.

3.  ADHABU  YA  KUCHAPWA  VIBOKO ( CORPORAL  PUNISHMENT).

Hakimu  au  jaji  anaweza  kwa  mamlaka  aliyonayo  kuamuru  mtuhumiwa  kuchapwa  bakora.  Adhabu  hii  inaweza  kutolewa  ikiwa  kama  adhabu  inayojitegemea  au  kama  nyongeza  baada  ya  adhabu  nyingine. Maana  yake  ni  kuwa unaweza kuhukumiwa  kifungo  na  viboko  au  viboko pekee na  uachiwe  huru.

4.   ADHABU  YA  FAINI ( FINE).

Hii  nayo  inaweza  kuwa  adhabu  inayojitegemea  au  inayotumika  kama  adhabu  ya  nyongeza  baada  ya  kuwa  imetolewa  adhabu  nyingine. Faini  huhusisha  malipo  ya  fedha  ambayo  yatalipwa kwa  utaratibu  maalum  utakaowekwa  na  mahakama.

5.  ADHABU  YA KUNYANGANYWA  MALI ( FORFEITURE).

Mahakama  inaweza kuamuru  mali  ya  mtuhumiwa  kunyanganywa   baada  ya  kupatikana  na hatia.  Mali  kunyanganywa  ni sehemu  ya  adhabu. Mara  nyingi  mali  zinazonyanganywa  ni  zile  zilizotumika  katika  uhalifu. Gari  au  pikipiki  kutumika  katika  wizi  ambao  umethibitishwa  inaweza  kunyanganywa. Hii  ni pamoja  na  mali  nyingine  kama nyumba,  meli, n.k.

6.  ADHABU  YA  KULIPA  FIDIA ( COMPESATION).

Fidia  ni  tofauti  na  faini. Fidia  ni  kulipia  kile ulichoharibu,  kupoteza au  hasara  uliyosababisha. Fidia  ni  mpaka  kiwepo  kitu  kilichopelekea  hasara, upotevu, au  uharibifu. Pesa  inayolipwa  kufidia hasara,uharibifu ndio  huitwa  fidia. Aidha  faini  hulipwa  bila  kuhitaji kuwepo  kitu  kilichoharibika  au  kusababishiwa  hasara.

7.ADHABU  YA  KUTUNZA  AMANI  NA  KUWA  NA  TABIA NJEMA ( PEACE  KEEPING & BE OF GOOD  BEHAVIOUR).


Mara  nyingi  adhabu  hii hutolewa  kwa  wenye  makosa  madogo  madogo. Hatutarajii  mtu  aibe , auwe  au abake  halafu  adhabu  yake  iwe kuhakikisha  anatunza  amani na kuwa  na  tabia  njema  mtaani . Ifahamike  kuwa adhabu  hii hutekelezwa  mtu  akiwa  nje.  
Ni  sawa na  kifungo  cha  nje  kwa  sharti  la  kutunza  amani  na  kuwa  mtu mwema  mtaani. Endapo  mtu huyu  atatenda kosa  jingine  katika kipindi  hiki  cha  uangalizi  basi  atapewa  adhabu  nyingine  kubwa  zaidi .

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA     SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.      0784482959,        0714047241              bashiryakub@ymail.com

0 comments:

Post a Comment