Wednesday, 3 February 2016

JE KUTOWEZA TENDO LA NDOA KUNABATILISHA NDOA KISHERIA?.

Tokeo la picha la WAMEFUNGA  NDOA

NA  BASHIR   YAKUB - 

Ni  muhimu kujua tofauti  ya  kisheria  ya maneno  ubatili  na  ubatilifu  kabla  ya kujua  lolote  kuhusu  hadhi/nafasi  ya  kisheria  ya ndoa  pasi  na tendo  la  ndoa.  Ujuvi  wa  maneno  ubatili  na  ubatilifu ndio utakaopelekea kufahamika  vyema  kwa haya makala. Kisheria  kuna  tofauti  kati  ya ubatili  na  ubatilifu.

1.TOFAUTI  YA  KISHERIA  KATI  YA  UBATILI  NA  UBATILIFU.

( a ) UBATILI.

Maana  ya  ubatili  kisheria  ni  kuwa  jambo  hilo  haliruhusiwi  kabisa. Halitakiwi  kutendwa  kwa  namna  yoyote  ile . Kwa  lugha  ya kitaalam  matendo  haya  huitwa  “VOID  ACTS”. Ni  matendo  haramu  kabisa. Kwa  mfano  kwenye  ndoa   matendo  haramu  ni  pamoja  na  mtu  kutangaza  ndoa  na  mtoto  wake  wa  kuzaa,  au  mtu  na  mzazi  wake, au    kutangaza  ndoa  ya  jinsia  moja  au  kutangaza  ndoa  na  mtu  mwenye  umri  mdogo.  Kwa  namna  yoyote  matendo  haya  ni  batili( void),  haramu   na  hayaruhusiwi  kwa  namna  yoyote.

( b ) UBATILIFU.

Maana ya  ubatilifu  kisheria  ni  kuwa  tendo  linakuwa si  halali  wala  si  haramu  isipokuwa  ili  liwe  halali  au  haramu  litategemea  uamuzi  wa  upande  mmoja  kati  ya  pande  mbili  zilizokubaliana. Upande  mmoja unaweza  kuamua   jambo  liwe  halali  au  liwe  haramu ,  nitatoa  mfano.

Mtu  akikuuzia  gari  ambalo  liko  tofauti  na  ulivyokuwa  umemwagiza  katika  mkataba  wenu  tendo   hilo  sio  halali   wala  sio haramu/batili  ila ni  batilifu. Hii  ina  maana  kuwa  ukiamua  kulipokea  gari  hilo  na  kulikubali hivyohivyo  lilivyo  basi  umehalalisha  tendo  hilo  na  limekuwa  halali. Ukikataa  kulipokea  kwakuwa  linapingana  na  kile  kilicho  kwenye  makubaliano  basi  tendo  hilo la  kuletewa  gari  lililo tofauti  linakuwa  haramu/batili.  

Basi ifahamike  kuwa  katika  sheria  yapo  matendo  ambayo  si  halali   wala  si  haramu.  Na  haya  kwa  kitaalam  huitwa”voidable  acts”. Na hicho ndicho kitakachoelezwa  katika   kujibu  swali  la nafasi  ya kisheria  ya mtu  ambaye   hawezi  kutekeleza  tendo  la  ndoa.

2.   KUTOWEZA  KUTEKELEZA  TENDO  LA  NDOA.

Sheria  imesema  kushindwa  kutekeleza  tendo  la  ndoa”incapable  of  consummating”. Maana ya  hili  ni  kushindwa  kabisa  kutekeleza  tendo  la  ndoa   na  sio  uwezo  mdogo  katika  kutekeleza  tendo  la  ndoa. Tofauti  hii  ni  lazima  ipambanuliwe bayana.

3.   JE  KUTOKUWEZA  TENDO  LA  NDOA  KUNABATILISHA  NDOA.

Hapo  juu  imeelezwa  maana  ya  ubatili  na  ubatilifu.  Swali  ni  je  kutokuweza  tendo  la  ndoa  kunaingia  katika  ubatili  au  ubatilifu.  Jibu  ni  kuwa  kutokuweza  tendo  la  ndoa ( incapable  of  consummating) kunaingia  katika  ubatilifu.

Kwa  maana  hii  ni  kuwa   kama  mwanandoa  “A”  hawezi  kutenda  tendo  la  ndoa  basi  mwanandoa  “B”  anayo hiari  ya  kuamua  kuendelea  na  ndoa  hiyo  ikiwa  halali  au  kuachana  nayo  ili iwe  haramu/batili. Ni  kusema  kuwa  uhalali  na  uharamu  wa  ndoa  hiyo  uko  mikononi  mwa  mwanandoa  “B”. Kuendelea  nayo  ni  kuihalalisha  na  kuachana  nayo  ni  kuiharamisha. 

Ni  hiari  ya  kisheria  aliyonayo. Hivyo  basi  jibu  la  swali  katika  kichwa  cha  makala  ni  hilo  tu  kuwa kutokuweza tendo  la  ndoa   kunaweza  kubatilisha  ndoa  au  kusibatilishe  kutegemea   na  uamuzi  wa  mwanandoa.

Mwanandoa  akiona  atavumilia  hali  hiyo ataendelea  na  ndoa   na   akiona  hali  hiyo  haiwezi  basi  ataacha.Uamuzi  ni  mikononi  mwake  na  huo  ndio  ubatilifu( voidable).
Hii  yote  ni kwa  mujibu  wa  sheria  ya  ndoa  sura  ya  29  kifungu  cha 39( a ) ( I ).

4. UGONJWA WA AKILI, NA  MAGONJWA  YA  KUAMBUKIZA  NAYO  HUPELEKEA  UBATILIFU.

Kifungu  hichohicho  cha  39  cha  sheria  ya  ndoa  kinaeleza  zaidi  kuwa   inapotokea  mwanandoa  mmoja  ana  ugonjwa wa  akili  au  magonjwa  mengine  ya  kuambukiza,halafu  mwingine  hana  basi  uhalali  wa  kuendelea  kwa  ndoa  hiyo  au  kutokuendelea utakuwa  mikononi  mwa  yule  ambaye  hana. Akiamua  kuendelea   itakuwa  ndoa  halali  na  asipoamua    basi  ubatili  wa  ndoa  hiyo  utapatikana.

Zingatia  kuwa katika  kujitoa  katika  ndoa batilifu  taratibu  za  kimahakama  za  talaka  zitafuatwa.

           NYUMBA  HII  INAUZWA  GOBA.
1.Ina vyumba 2, kimoja master.
2. Iko  ndani  ya  fensi.
3. Ina  hati  full( title deed).
3. Umeme umo na maji,jiko na public toilet.
4. Ipo goba karibu  na  goba  secondary.
5. Km  tatu  na nusu  kutoka  masana.
7. Bei milioni  120 inapungua .
0784482959.

0 comments:

Post a Comment