Tuesday, 23 February 2016

KAMPUNI ILIYOSAJILIWA NJE KUFANYA BIASHARA TANZANIA.NA  BASHIR  YAKUB -

Mara  kadhaa  tumeeleza  namna  ya  kusajili  kampuni. Yumkini  tulipoeleza  hivyo  tulirejea usajili  wa  kampuni  zilizo  Tanzania.  Tulieleza  faida  za  kufanya  biashara  chini  ya  kampuni  na  tukaeleza  namna  ya  kisheria  ya  kusajili  kampuni  mwanzo  mpaka  mwisho  unapopata  cheti  cha  kuzaliwa  kwa  kampuni( certificate  of  incorporation). 

Hatujawahi  kueleza  usajili  wa  kampuni  ambayo  imeanzishwa  nje  ya  Tanzania inayohitaji  kufanya  biashara  Tanzania.

1.KAMPUNI  ILIYOSAJILIWA  NJE  YA  TANZANIA.

Tunaposema  kampuni  kusajiliwa  nje  ya  Tanzania  tunamaanisha  kampuni   imeanzishwa  nje  ya  Tanzania    na  cheti  chake  cha  usajili  imekipata  huko  nje  ya  

Tanzania  na  hivyo  inatambulika  kama  kampuni  ya  huko  ilikosajiliwa.  Kampuni  ya  namna  hii  inaweza  kuamua  kuja  Tanzania  kufanya  biashara  bila  kuhitaji  kuanzisha  kampuni  nyingine  mpya  isipokuwa   kuendeleza  ileile  na   kupafanya Tanzania kama  tawi  au  si  tawi   lakini sehemu  kuu  ya  biashara.

2.  WATANZANIA  WALIO  NJE  YA  NCHI  KUMILIKI  MAKAMPUNI  HAYA.

Baadhi  ya  Watanzania  walio  nje  ya  nchi  wamewahi  kuuliza  swali  hili  wakitaka  kujua  utaratibu  wa  kufuata  ili  kuifanya  kampuni  iliyoanzishwa nje  ya Tanzania kuweza kufanya  kazi  zake  Tanzania.

Kwa  waliouliza  swali  hili  watapata  majawabu  lakini  pia itafahamika  kwa  wengine  kuwa  unaweza  kuunda  kampuni  hukohuko  uliko  ikafanya  kazi  huko  lakini  pia  Tanzania  ambako  ni  nyumbani  kukawa  na  tawi  la  biashara  .

Lakini  pia  wapo  watu  ambao  huulizwa  swali  hili na  rafiki  zao  wa  kigeni  kuhusu  kuingiza  kampuni  Tanzania   kwa  ajili  ya  biashara.  Hawa  nao  sasa  watakuwa  na majawabu.

3. NAMNA  KUSAJILI  KAMPUNI  ILIYOANZISHWA  NJE  YA  NCHI.

( a ) Kwanza  kabisa  usajili  huu  utafanyika   kwa  msajili  wa  makampuni  na  biashara( BRELA) jengo  la  ushirika, ghorofa  ya  sita,  Mnazi  mmoja  Dar  es  salaam.

( b ) Mtatakiwa  kuwasilisha  nakala  halisi ( certified  true  copy)  za  waraka  na  katiba  ya  kampuni( memorandum & article  of  association).  Kwakuwa  nakala  hizi  zitakuwa katika  lugha  ya  nchi   ilikosajiliwa  kampuni  basi  nakala  hizo zinatakiwa  kuambatana  na  tafsiri  halisi  kutoka  kwa  mfasiri  aliyesajiliwa.

Zitafasiriwa  na  kuingizwa katika  lugha  ya  kiingereza.  Ikiwa  zipo  katika  lugha  ya  kiingereza  basi   mfasiri  hahitajiki  zitawasilishwa hivyohivyo.

( c ) Mtatakiwa  kuambatanisha   orodha ya  wakurugenzi  wa  kampuni  pamoja  na  katibu. Kutakuwa  na  majina  matatu  ya  kila  mkurugenzi  na  katibu,  utaifa  wake, anuani  yake  ya makazi   na  shughuli  anazojishughulisha  nazo  mbali  na hiyo  kampuni( kama  zipo).

( d )  Kama  kampuni  tayari  inafanya  biashara   itawasilisha  tamko   maalum  kuhusu  madeni  pamoja  mali  ilizoweka  rehani   kwa  ajili  ya  madeni  hayo. Itaeleza  mali ilizoweka  rehani  zilipo (nchi  husika itajwe).

( e ) Kuwasilisha  waraka  maalum  unaoeleza  jina  la  mtu  mmoja  au  zaidi  anayeishi  Tanzania ,  anuani  zake  za  makazi  na  kazi  yake.  Katika  waraka  huo  mtu  huyo atatajwa  kama  mtu  ambaye   atakuwa  muwakilishi   wa  kampuni  hiyo  hapa  Tanzania  na  kuwa  shughuli  zote   na  taarifa  za kampuni  zitapatikana  kwake.

( f ) Anuani  kamili  ya  ofisi  kwa  hapa  Tanzania  na  sehemu  ya  kufanyia  biashara  ni  lazima  vioneshwe  na  kuthibitishwa.

( g ) Kiapo  cha  katibu  na  mmoja wa  wakurugenzi  wa  kampuni  kuonesha  tarehe  rasmi  ya  kuanzisha  biashara  Tanzania  na  aina  ya  biashara  itakayofanywa  na  kampuni.

Pia  jina  la biashara  litakalotumika  litapaswa  kuoneshwa.  Jina la biashara  laweza  kuwa  tofauti  na  lile  ililosajiliwa   nalo  huko  ilikotoka.

( h ) Taarifa   za  akaunti  ya  kampuni.  Kama  taarifa hii itakuwa  katika lugha  nyingine  isiyo  kiingereza  basi  tafsiri  kutoka  kwa  mfasiri  aliyesajiliwa  itahitajika.

Nyaraka  hizi  zinatakiwa  kuwasilishwa  ndani  ya  siku  30  tangu  kampuni  hiyo  iombe  kusajiliwa  Tanzania. Kwa  ufupi  haya  ndiyo  ya  awali  yanayohitajika.  Na  haya yote  ni  kwa  mujibu  wa  sheria  ya  makampuni   sura  ya 212  hususani  vifungu  vya  433  Na  434.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA     SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.      0784482959,        0714047241              bashiryakub@ymail.com0 comments:

Post a Comment