Monday 18 January 2016

UNAJUA NINI KUHUSU BARAZA LA ARDHI LA KATA ?.


Image result for BARAZA LA  ARDHI  LA  KATA

NA  BASHIR  YAKUB - 

Tunapozungumzia mgogoro  wa ardhi  tunazungumzia mgogoro  katika  viwanja, mashamba, nyumba  na  majengo. Wengi  wetu  tunapokutwa  na  migogoro  ya  ardhi  hukimbilia  mahakama  za  wilaya  au  mahakama  kuu  ya  ardhi. Lakini  tunasahau  kuwa  lipo  baraza  la  ardhi  la kata  ambalo  baadhi  ya  migogoro  haifai  kwenda huko  wilayani  au  mahakama  kuu kabla  ya  kupitia  hatua  hiyo.  Makala  yataeleza  kuhusu  baraza  la  ardhi  la  kata  na  mashauri  yanayotakiwa  kuanzia  hapo.

1.NGUVU  YAKE  NI  KATIKA  KATA  TU.

Baraza la  ardhi  la  kata  ni  mahakama  ya  ardhi  katika  kata husika . Hii  ni  kwa  mujibu  wa kifungu  cha  10 ( 1 )  cha  sheria  ya  mahakama  za  usuluhishi  wa  migogoro  ya ardhi.   Baraza  hili mipaka  yake  ni  katika  kata  husika  kwa maana  ya kuwa  mipaka  ya  kata ndio  mamlaka  yake  kijiografia.

Kwa  maana hii  kila  kata   hutakiwa  kuwa na  baraza  lake  la  usuluhishi  wa  migogoro  ya  ardhi . Baraza la  ardhi  la  kata  fulani  haliwezi  kuvuka  mipaka  na  kwenda  kuamua  mgogoro  wa  ardhi  wa  kata  nyingine.

2.  JE  INATAKIWA  WAAMUZI  WANGAPI  KATIKA  BARAZA.

Unapokuwa  na mgogoro  katika  baraza  hili  ni  muhimu  kujua  ni  watu  wangapi  wanatakiwa  kuamua  mgogoro  wako. Mara    kadhaa  hasa  huko  vijijini  waamuzi  katika  mabaraza  haya  wamekuwa  wakijikalia  tu  na kutoa  maamuzi  pasi na  kuzingatia akidi. 

Unapaswa  kujua  kuwa  kuna  akidi  maalum  ya  kisheria na  hivyo  kabla  ya kuamuliwa  mgogoro  wako  ni  vyema    ukahoji  akidi  hasa  ikiwa  haijatimia.
Kifungu  cha 14( 1 ) kinasema  kuwa  vikao   vya  usuluhishi vya  baraza   vitakaliwa  na  wajumbe  wasiopungua  watatu  huku  mmoja  akitakwa  kuwa  mwanamke.  Hii  ni  akidi  ya  kisheria  na  hivyo  yafaa  ujue  kuwa  unayo  haki  ya  kuhoji  ikiwa  akidi  hii  haijatimia. 

Ni  muhimu  kutoruhusu  kikao  kuendelea  ikiwa  akidi  haijatimia  kwakuwa  maamuzi  yatakayotolewa  na akidi  pungufu  kisheria yatakuwa  batili. Kwahiyo  hata  kama  umeshinda  ushindi  wako  utakuwa  ni  kazi  bure.

3.  JUMLA  YA  WAJUMBE

Kifungu  cha  11  cha  sheria  ya  mahakama  za  usuluhishi  wa  migogoro  ya  ardhi  kinasema  kuwa  baraza  la  usuluhishi  litakuwa  na  wajumbe  wasiopungua  wanne  na  wasiozidi  nane . Kati  yao  watatu  inabidi  wawe  wanawake. Hawa  ni  wajumbe  wa  jumla  ambao  ndio  huunda  baraza zima. Zingatia  hii sio  akidi  ya  kila kikao ila  ni  wajumbe  kwa  ujumla  wao.

4.  KAZI   KUU   YA BARAZA.

Kazi  kubwa  ya  baraza  la  ardhi  la  kata  imeelezwa  vyema  katika  kifungu cha  13 ( 1 )  cha  sheria  ya  mahakama  za  usuluhishi  wa  migogoro  ya  ardhi.  Kifungu  kinasema  kuwa  kazi  ya  msingi  ya  baraza  ni  kutafuta  amani  na  utulivu  katika  eneo  husika  kupitia  kusuluhisha  na  kuwasaidia  wahusika  walio katika  migogoro  kufikia  suluhu  yenye  maelewano  katika  masuala  yanayohusu  ardhi.

5. KUZINGATIA  MILA  WAKATI  WA  USULUHISHI.

Kwakuwa  baraza  hili  linahusu  kata   sheria  imetoa  mwanya  kwa wasuluhishi  kuhusisha  taratibu  za  kimila  katika  kutafuta  suluhu.  Hii  ni  kwakuwa  masuala  ya  ardhi  na  usuluhishi kwa  kiasi  kikubwa  yameambatana  na  mila. Sheria inaamini  kuwa  kwakuwa  wasuluhishi  watakuwa  wanatoka  kata  husika  basi   pia  watakuwa  wanajua  taratibu  za  kimila  za  eneo  husika.

Hii  ni  kutokana na  kifungu  cha   13 ( 3 ) kinachosema  kuwa  baraza  katika  kufanya  kazi  zake  za  usuluhishi  litahusisha  kanuni  yoyote  ya  kimila  inayohusu  usuluhishi. 

Kifungu  kinasema kuwa  ikiwa taratibu  za  kimila hazitatumika  basi  kanuni  za  maamuzi  ya  asili ( principle  of  natural  justice) zaweza  kutumika.

6.  BARAZA  HALISULUHISHI  MGOGORO  UNAOZIDI  MILIONI  TATU.

Kifungu  cha  15  cha  sheria  ya  mahakama  za  usuluhishi  wa  migogoro  ya ardhi  kinasema  kuwa  baraza la  kata  halitakuwa  na  uwezo  wa  kusuluhisha  mgogoro  ambao  thamani  yake  ni  zaidi  ya  milioni  tatu. Thamani  ya mgogoro  huangaliwa  kwa  kutizama   thamani  ya  ardhi  inayogombaniwa. Thamani  ya  ardhi  inayogombaniwa  ikizidi  milioni  tatu  basi mgogoro  huo  hauwezi  kuanzia  baraza  la  ardhi  la  kata.
MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE.      0784482959,        0714047241              bashiryakub@ymail.com


1 comments:

  • baptcmwanza says:
    6 April 2020 at 09:44

    Habari nimebahatika kusoma kwa ufasaha eneo hili ,Ila Nina swali langu naomba ushauri
    1-Ikiwa Mwenye ardhi in mgonjwa akakubaliana na familia yake kuuza eneo dogo la ardhi kutoka kwenye ardhi yao
    1.a .Mnunuzi akapatikana wakaonyeshana kipande cha ardhi kinacho tangazwa kuuzwa akaridhika wakakubaliana bei Tsh 500,000/-
    Mnunuzi akaomba kutanguliza Tsh 300,000/- na kiasi kilicho baki akaahidi kulipa kwa mda Fulani,
    Kwa kuwa anatanguliza wakakubaliana wauzaji na mnunuzi waweke mkataba wao mdogo wa maandishi wao wenyewe mkataba ukashuhudiwa na mashahidi wa pande zote mbili na wakakubaliana siku mnunuzi alioahidi kulipa fedha iliobaki ndipo watahusisha Selikali ya mtaa au kijiji(sentence hii ingawa hawajaiandika kwenye mkataba wao)
    Kwa kuwa wauzaji wana mgonjwa na waliuza kwa ajili ya gharama za kutibisha mgonjwa wao wakaitumia ile advance kwa shughuli hiyo na wao kutanguliza kwenye tuba ili mnunuzi atakapo malizia fedha iliobaki na familia itaiongezea kukamilisha ghalama za tiba kwa mgonjwa wao.
    Mnunuzi ajashindwa kutimiza makubaliano yao na hakuwahi kuja kuomba kuongeza mda wa kulipa labda kutokana na shida iliomsibu akashindwa kutimiza makubaliano ya awali ya ununuzi wa ardhi husika
    Akaja nje ya mda na bila fedha iliobaki anadaiwa .
    Kwa kuwa mda umeishaenda sana wauzaji wakamwambia awaongeze fedha zaidi ya alizokuwa anadaiwa kwa msingi ya mda waliokubaliana umeisha pitiliza zaidi Je hapo sana makosa?
    1 .b. Mnunuzi huyo akiondoka na kupeleka madai baraza LA ardhi LA kata itakua halali?
    1.c.Wauzaji bada ya wito wa baraza wakaekwa chamber iliwajadriane
    Wahusika mnunuzi na wawauzaji ili kuondoa mgogoro wakaona eneo husika liuzwe kwa kutafuta mnunuzi mpya ili mnunuzi wa awali aludishiwe advance aliokuwa amelipa na wakafikiria Wenda ndani ya siku 90 eneo husika litakuwa limepata mteja mpya ili wauzaji walejeshe ile advance ya mnunuzi wa awali,Baraza likaandika in short kuwa wahusika wamekubaliana kulejesheana advance ndani ya siku 90 bila kuandika kuwa eneo husika hadi liuzwe kwa mteja mpya ,siku zikapita bila eneo hill kupata kuuzwa wauzaji wakalitaarifu baraza hill kwa maandishi nakala kwa aliekuwa mnunuzi wa awali alieshindwa kumalizia fedha za mauziano ya awali bada ya mnunuzi wa awali alieshindwa kumalizia alipopokea nakala hiyo yeye akaenda kulalamika kwa Afisa mtendaji wa kata kwa niaba yake malalamiko yakapokelewa na mtendaji wa mtaa anakoishi huyo aliekuwa mnunuzi ,Ofisi husika ikawaita na katika kuwasikiliza likatolewa tamko kuwa nanukuu
    Eneo husika libaki lilivyo ikiwa mmoja wa wahusika akipata mnunuzi apitie ofisi ya kata ili wasimamie mauziano na mnunuzi wa awali ndipo alejeshewe fedha alizolipa kama advance .
    Ukapita Mnunuzi huyo wa awali akapata mteja akapitia ofisi ya kata wakaenda kwa kwenye ardhi ili eneo lilokuwa linauzwa liuzwe bahati mbaya mnunuzi alieletwa eneo akaona ni ndogo kwake akashindwa kununua wakaishia hapo ili waendelee kutafuta wateja wengine
    Ghafla mnunuzi yule wa awali kwa kukosa wateja akaenda tens baraza LA ardhi LA kata kwa Mara ya pili kwa malalamiko tena je wenye ardhi waliokuwa wanauza kwa ajili ya ugonjwa makosa yao ni yapi?na watajibu nini hali hali wao sio waliokiuka makubaliano na kusababisha sura ya mgogoro?

Post a Comment