NA BASHIR YAKUB -
Hakimiliki katika masuala
ya ardhi huhusisha
umiliki wa ardhi zenye hati. Umiliki huu hutoa
wajibu na haki fulani
kwa mmiliki katika ardhi husika. Si rahisi
kudai una hakimiliki
katika ardhi kama hauna hati.
Aidha tumezoea kuona
hati zilizo na
jina la mtu mmoja
mmoja. Hii ni hata
kwa wanandoa ambao hudai
mali husika zinatokana na
jasho lao wote. Lakini je unajua
kuwa inawezekana hati miliki
ikawa na majina
ya wanandoa wote badala
ya kuwa na jina
la mmoja tu hasa baba ambao
ndio wengi hupenda
majina yao yaonekane
hapo ?. Jambo hili
linawezekana na linaruhusiwa.
1.HAKIMILIKI YA PAMOJA KUONDOA
MGOGORO.
Kutokuelewana ambako mara
kadhaa hutokea baada
ya kifo cha
mmoja wa wanandoa kwaweza
kuondolewa na umiliki
wa ardhi wa
pamoja. Ikiwa una wasiwasi juu
ya mustakabali wa
mali hasa ardhi
huko mbeleni ni
vema basi ukachukua
hatua hii ya
kusajili kwa umiliki wa
pamoja.
Kama kiwanja/ nyumba ina hati
yenye majina mawili la baba na mama halafu mmoja wao
akafariki itakuwa ni vigumu
ndugu au mwingine
yeyote mwenye nia
mbaya kudai umiliki wa kiwanja/nyumba hiyo.
Lakini hali
itakuwa tofauti iwapo hati
ina jina la mmoja na
huyohuyo mmoja ndiye aliyefariki. Pale pote
ambapo ndugu walidhulumu
mali za marehemu
hasa ardhi ni
pale ambapo kuna jina
la mmoja.
Mara nyingi fitina
huingia pale penye mwanya wa
kufanya hivyo. Si rahisi
fitina kuingia pasi na mwanya. Kuweka majina ya
wanandoa wote kwenye hati
za ardhi ni
hatua ya kuziba
mwanya wa fitina. Itawezekanaje ndugu au mwingine mwenye
nia ovu kudai umiliki wa ardhi ya marehemu
huku akijua kuwa
hati inalo jina
la mke pia.
Si rahisi hata kidogo.
Lakini pia umiliki
wa pamoja huondoa
mgogoro pale panapo
talaka. Swali la je
mwanandoa fulani amechangia
chochote katika kupatikana
kwa mali huwa
halipo ikiwa majina
yote mawili ya
wanandoa yameonekana kwenye
hati.
2. KUMILIKI ARDHI
PAMOJA KATIKA NDOA
YA MKE ZAIDI
YA MMOJA.
Suala la kuwa na
hati yenye majina ya wanandoa
wote ni pana.
Tunaposema wanandoa wote hatumaanisha
mme na mke mmoja tu.
Kinachomaanishwa hapa ni kuwa
inawezekana kuwa na hati yenye jina
la mme pamoja
wake zake wawe
wawili, watatu n,k.
Kifungu cha 161 ( 1 )
cha Sheria namba
4 ya ardhi
kinasema kuwa , pale
ambapo mwanandoa anapata
hakimiliki ya ardhi
iliyosajiliwa kwa jina
lake na mke
wake au wake
zake itajengwa dhana
ya kisheria kwamba
wanandoa hao wanamiliki
ardhi hiyo kwa
pamoja.
Kifungu
kinaonesha wazi kutambua hakimiliki
ya ardhi inayohusisha
mitala.
3. KILA
MWANANDOA ATAPEWA HATI YAKE.
Majina ya wanandoa
yanapokuwa yameingizwa yote kwenye hati basi ni
haki ya kila
mwanandoa ambaye jina
lake limeingia kupata nakala
yake ya hati.
Kwahiyo mwanaume atamiliki
hati yake halikadhalika
mwanamke au wanawake
nao watamiliki hati
yao kila mmoja
yake. Hii ni tofauti na
hati inapokuwa na
jina la mtu
mmoja tu ambapo
huyohuyo ndiye humiliki hati hiyo.
4. KUGAWANA ARDHI INAYOMILIKIWA
KWA PAMOJA.
Hati inapokuwa na majina ya wanandoa
wote sio lazima iwe
imeeleza nani anamiliki
wapi mpaka wapi.
Kutokana na hilo
mmoja wa wanandoa
anaweza kuomba iwekwe mipaka au
ijulikane nani anamiliki
nini japo hati
ni moja.
Katika kulifikia hilo
maombi maalum inabidi
yapelekwe kwa kamishna
wa ardhi kwa
ajili ya kutambulisha
nani anamiliki nini katika
ardhi hiyo, liwe
jengo,nyumba, shamba au vinginevyo.
Kifungu cha 162 ( 1 )
cha sheria ya
ardhi kinasema kuwa
maombi yaliyo katika
fomu maalum yatawasilishwa kwa
msajili kwa ajili
ya kugawa nani anamiliki nini.
Haki
ya maombi haya
ni ya mtu yoyote
kati ya wale
ambao majina yao
yanaonekana kwenye hati.
Hili litafanyika kwa
kuzingatia sheria nyingine kama
sheria ya ndoa( The law of marriage
Act).
MWANDISHI WA MAKALA
HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA
GAZETI LA SERIKALI LA HABARI
LEO KILA JUMANNE , GAZETI JAMHURI
KILA JUMANNE NA GAZETI NIPASHE KILA
JUMATANO. 0784482959,
0714047241
bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment