Thursday 21 January 2016

SIFA ZA KUMILIKISHWA ARDHI TANZANIA.

Image result for ARDHI  YA  KIJIJI

NA  BASHIR  YAKUB -

Ili  uweze  kupewa ardhi  na kutambuliwa  kama  mmiliki Tanzania zipo  sifa  ambazo  unatakiwa  kuwa nazo. Si  kila  mtu  anaweza  kupewa  ardhi  ya  kumiliki.  Sifa  hizo  zinatofautiana  na  wakati  mwingine  kufanana  kutokana  na aina  ya  ardhi  inayoombwa  na  mtu husika.  

Kuomba  kumilikishwa  ardhi  ni  hatua  ambayo  huchukuliwa  na  mtu   anapohitaji  kupata  hati.  Nasema  hivi   kwa  maana  ya  kuwa    kuna  watu  wana  ardhi  lakini  hawana  hati  za  umiliki.  Hawa  kisheria  hatuwezi kusema  wamemilikishwa  ardhi.  Aliyemilikishwa  ardhi  ni  yule  aliye  na  hati  ya  umiliki. 

1.AINA  ZA  ARDHI  TANZANIA.

Sifa  za  umilikishwaji   ardhi  zinategemea  sana  na aina  ya  ardhi inayoombwa  na mtu.  Hapa  kwetu  Tanzania  ardhi  yoote  imegawanywa  katika  makundi  makuu  matatu  kama  tutakavyoona.

( a ) ARDHI  YA  VIJIJI.

Ardhi  ya  vijiji hujumuisha  ardhi  yote  ya   maeneo yaliyotengwa  kama  vijiji.  Ardhi  hii  ni  lazima  iwe  ndani ya  mipaka  ya  kijiji na  iwe nje  ya  hifadhi.  Pia  ardhi  yote  iliyokuwa haitambuliki  kama kijiji lakini ikatumika  kama  kijiji  kwa  kipindi  kisichopungua  miaka  12  kabla  ya  kuanza  kutumika  kwa  sheria  namba 5 ya  ardhi  ya  vijiji  nayo  itahesabika  kama  ardhi  ya  kijiji.

( b ) ARDHI  YA JUMLA.

Ardhi  hii  huwa  ni  ile  ardhi  yote  isiyokuwa  ya kijiji  na isiyokuwa  ya  hifadhi. Kuielewa  zaidi  ardhi  hii   twaweza  kusema   kuwa  ni  ile  ardhi  ya  mijini   na  maeneo  yanayozunguka  miji  hiyo.  Ardhi  yote  ya  mijini  kama  si  ardhi  iliyohifadhiwa  itakuwa  ni  ardhi  ya  jumla.

( c ) ARDHI  YA  HIFADHI.

Hii  ni  ardhi  iliyohifadhiwa  kama  jina  lenyewe  lilivyo.  Ardhi  ya  hifadhi  hupatikana  kote  mjini  na  vijijini. Ardhi  hii  hujumuisha maeneo  ya  hifadhi  za  wanyama kama  mbuga, milima  iliyohifadhiwa  kama  Kilimanjaro, misitu  ya    hifadhi, mabonde  ya  hifadhi, viwanja  vyote vya wazi vya  mijini  na  vijijini, maeneo  maalum  ya  hifadhi  ya  bahari, mito  na  maziwa,  viwanja  vya  michezo, maeneo  yote  yaliyotangazwa  kuwa  hatari  kwa  watu  kuishi,   na  hifadhi  zote  za  barabara.

Kwa  kuangalia  aina  hizo  tatu  za  ardhi  unakuwa  umeongelea  ardhi  yote  ya  Tanzania.

2.   SIFA  ZA  KUMILIKISHWA  ARDHI.

( a ) Hapo  juu  makala  yameeleza  kuwa  kumilikishwa  ardhi  kunategemea  na  aina  ya  ardhi  unayotaka. Kwa  upande  wa  umilikishwaji  wa  ardhi  ya  kijiji  sifa  zifuatazo  zinahitajika.

Kwanza  awe  yeyote  kati  ya mwanamke  au  mwanaume.  Vijijini  wanawake  wengi  hunyimwa  haki  hii.  Hata hivyo  ni  haki  ya  kisheria  kwamba, kuwa   mwanamke  ni  sifa  ya  kumiliki  ardhi  ya  kijiji.

Pili, awe  na  umri   unaofika  miaka  kumi  na  nane.  Akiwa  mwanamke  au  mwanaume  basi  awe  ametimiza  umri  wa  miaka  kumi  na  nane.  Asiwe  chini  ya  umri  huo.

Tatu, anaweza  kuwa  mtu  mmoja  wawili  au  kikundi  cha  watu. Ardhi  ya  kijiji  sio  lazima  imilikiwe  na  mtu  mmoja mmoja. Hata  kikundi  cha  watu  kinaweza  kumiliki  chini  ya  hati  moja.

Nne si  lazima  awe  raia  wa  Tanzania.  Hata  mgeni  anaweza  kupewa  ardhi. Hata  hivyo  atapewa  kwa  hakimiliki  isiyo  ya  asili ( derivative right).  Atapewa  kwa  matumizi  na taratibu  zake  za  kupatiwa  ardhi  zitakuwa  tofauti  na  za  Mtanzania.

( b ) Kumilikishwa  ardhi  ya  jumla/ya  mjini.  Sifa  za kumilikishwa  ardhi  ya  jumla  ya  mijini  hazitofautiana  na  zile  za  ardhi  ya  kijijini zilizoelezwa  hapa  juu. Kubwa  ni umri  wa  miaka  kumi  na  nane, mwanamke  au  mwanaume anaruhusiwa  kumiliki, mgeni  atapatiwa  kwa  matumizi  maalum, na  vikundi  vitaruhusiwa  kumiliki.

Maelezo  haya  yote yamechambuliwa  kutoka  sheria  namba  4  ya  ardhi  ya  mwaka  1999 na  namba 5  za  ardhi  ya  vijiji.
MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA     SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.      0784482959,        0714047241              bashiryakub@ymail.com


1 comments:

  • Unknown says:
    26 January 2016 at 20:24

    mimi naomba masaada nina kiwanja mabacho nalipia kodi ya ardhi kila mwaka tokea mwaka 90 ila ilikuja kutokea kuna mtu mwengine kamilikisha tokea mwaka 93 namaanisha kiwanja kina dable alocation nifanyeje a japo huyu mwenzangu aliamua kusarenda akiona kuwa amezulumiwa ila wizara inanizungusha kupata hati nifanyeje

Post a Comment