Wednesday, 13 January 2016

NAMNA YA KUDAI FIDIA ARDHI YA KIJIJI INAPOTWALIWA.

Image result for ARDHI  YA  KIJIJI

NA  BASHIR  YAKUB -

Suala  la  kudai  fidia  pindi  ardhi  ya kijiji  inapotwaliwa  linaongozwa  na sheria  ya  ardhi  ya  vijiji  ya  1999. Fidia  ni  haki  pale  ardhi  ya  kijiji  inapotwaliwa. Ziko  sababu  zinazoweza  kuifanya  serikali  kutwaa  ardhi  ya  kijiji  kwa  mfano   kupisha  miradi  ya  maendeleo,  kupisha  uwekezaji  kwa  manufaa  ya  kijiji  husika  na  taifa  zima,  halikadhalika   kuondoka  katika  eneo  ambalo  limetangazwa  kuwa  hatarishi  kwasababu  za  kijiografia  au  nyinginezo.  

Yumkini  kwasababu yoyote  katika    hizi  fidia  hubaki  haki  ya  msingi  kwa  mwananchi.

1.MTAPATAJE  TAARIFA  YA  KUDAI  FIDIA.

Sheria ya  ardhi  ya  kijiji  inamtaka  Kamishna  wa  ardhi  kutoa  taarifa  kuhusu  fidia   kwa  halmashauri ya  kijiji  pamoja  na  watu  wote  wanaokalia  ardhi  inayotakiwa  kutwaliwa.

Huu  ni  wajibu  kwa  kamishna  na kufanya  hivyo hakutegemei  hisani yake. Taarifa  hiyo  itatolewa  katika  fomu  maalum  na  itakuwa  ikieleza  eneo  rasmi  linalotakiwa  kutwaliwa  huku  ikiitaka  halmashauri  ya  kijiji  na  watu  wote  watakaoathirika kuleta  malalamiko  ya  fidia  pale fomu inapoelekeza.

Hii  ina  maana  hata  kama  mwanakijiji  haijui  haki  yake  ya  kudai  fidia  basi  fomu  hiyo  itatakiwa  imweleze  kuwa  una  haki  ya  kudai  fidia  na  madai  yako  yapelekwe sehemu  fulani.

2.  MUDA  WA  KUWASILISHA  MADAI  YA  FIDIA.

Baada  ya  halmashauri  ya  kijiji  pamoja  na wahanga   wanaotakiwa  kuondolewa  kujaza  fomu  ya  fidia  kwa  ukamilifu  basi  madai  yao  yatatakiwa  kuwasilishwa  sehemu  ambako  fomu  hiyo  imeelekeza. Maombi  yatatakiwa yawasilishwe ndani  ya  siku  sitini ( 60).  

Siku  hizo  sitini  zinaanza  kuhesabika  tangu  siku  mlipopokea  taarifa  ya   nia  ya kutwaliwa  ardhi  yenu.  Siku  ambayo   mnaletewa  taarifa  na  fomu  ya  fidia  ndiyo  siku  zinapoanza  kuhesabiwa.

Ni  muhimu  kuhakikisha  madai  yanapelekwa  ndani  ya  muda   kwasababu  muda  huo  ni  wa  kisheria  na  hivyo  kuwa  na athari mbaya  ukipita.

3.  MSAADA  WA  KUTAYARISHA  MADAI  YA  FIDIA.

Suala  la  kutayarisha  madai  ya  fidia  ni  la  kisheria zaidi. Sheria  ya  ardhi  ya  vijiji  inasema kuwa  afisa  mteule  kwa  maana  ya  afisa  aliyeteuliwa  na  serikali  kushughulikia  suala  la  ardhi   yenu  inayotwaliwa   ndiye  atakayetoa  msaada\mwongozo  kwa  halmashauri  ya kijiji  pamoja na  wahanga  wanaoondolewa  katika maeneo  ili  kuandaaa  madai  ya  fidia. 

Madai  ya  fidia  ni  nyaraka  maalum  na  ya  kisheria  hivyo  si  jambo  ambalo  kila mtu  anaweza  kuandaa. Kwahiyo  suala  la msaada  wa  kuandaa   madai  ya  fidia  ni    jukumu  la kisheria  alilonalo   afisa  anayeshughulikia   kutwaliwa  eneo  lenu.

4.  KUKUBALI   KULIPWA  FIDIA.

Kwa  mujibu  wa  sheria  kamishna  wa  ardhi  ndiye  mwenye  mamlaka  ya  kukubali  malipo  ya  fidia   baada  ya  madai  kuwasilishwa  kwake. Hata  hivyo  pamoja  na  kuwa  mtakuwa  mmeelezwa  haki  yenu  ya  kudai  fidia  bado  kamishna  anaweza  kukataa  madai  yenu  na  kuamuru  kuwa  hakutakuwa  na  malipo  ya  fidia.

Hii  hutokana  na  sababu  mbalimbali  za  kisheria  mojawapo  ikiwa  ni wananchi  kuwa  wameingia  katika  ardhi  ambayo  imezuiwa. Ikiwa waliingia  baada  ya ardhi  hiyo  kuwa  imezuiwa   kukaliwa basi  uwezekano  wa  maombi  yao  ya  fidia  kukataliwa  ni  mkubwa.

Aidha, Kamishna  atatakiwa  kutoa  majibu  ya  kukubali  au  kukataa  fidia  ndani  ya  tisini ( 90) toka  siku  alipopokea  maombi  ya  madai  yenu  ya  fidia. Hivyo  ni  muhimu  kujua  kuwa  mnapokuwa  mmepeleka  madai   ya  fidia  kama  ilivyoelekezwa  hapo  juu  basi  hesabuni  mpaka  siku  tisini  halafu  kama  hamjajibiwa  ni  wajibu  wenu  kufuatilia  na  kujua  kulikoni. 

Zisipite  siku  tisini  pasi  na  majibu  yoyote   halafu  mkakaa  kimya  bila  kufuatilia. Hii  ni  kutokana  na  athari  za  kisheria  zinazoweza  kuwakuta  iwapo  muda  utapita.

5.   KULIPWA  FIDIA  BAADA  YA  SIKU  21.

Ikiwa maombi  ya  fidia  yatakubaliwa  basi  kamishna  atatoa  taarifa  kwa  Waziri  mwenye  dhamana  akimueleza  kukubali   kulipwa  kwenu  fidia  na  ndani  ya  siku  ishirini  na  moja ( 21) tangu  waziri  apokee  taarifa,  malipo  ya  fidia  kwa  wahanga inabidi yatoke.

Kwa  ufupi  huo  ndio  utaratibu  wa  fidia  kwa  ardhi  ya kijiji.
                            NYUMBA  HII  INAUZWA  BUNJU "B".



1. Ina vyumba 3, kimoja master na fremu ya duka mbele.
2. Ipo ndani  ya  fensi  kubwa sana.
3. Umeme, maji vimo ndani, jiko na public toilet.
4. Ipo Bunju B  mkono  wa kulia ukitokea mjini.
5. Eneo zuri tulivu kwa makazi.
6.Ni nyumba yenye eneo kubwa.
7. Mita chache kutoka  barabara  kuu ya  Bagamoyo .
8. Bei milioni  90 inapungua .

0784482959.

0 comments:

Post a Comment