Tuesday 5 January 2016

JE WAJUA KUMSHAURI MTU KUTENDA JINAI NAYO NI JINAI ?.



Image result for KUTENDa  kosa
NA  BASHIR  YAKUB - 

Usimshauri  mtu  kuhusika  katika  kitendo chochote  ambacho  kinakatazwa  na  sheria. Kufanya  hivyo  kutakufanya  nawe  kuhesabika  umehusika katika  kosa  hilo. Hii  ni  hata  katika  mambo  ya  kawaida  tuliyozea.  

Ukimsikia  mtu  anapanga  kwenda  kumkomesha  fulani kwa  kumpa  kipigo  usitie  neno  lako labda  kama  unamzuia. Usijaribu  hata  kusema  nenda  kamfanyie  amezidi.  Maneno  hayo  ni  machache  lakini  kisheria  yatachukuliwa  kama  ushauri  kwa mtenda  kosa.

Au  mtu  anakwambia  nakwenda  kumpa  vidonge  vyake  kwa  maana  ya  kumtukana na  kumdhalilisha  na  wewe  unasisitiza kwa  kumwambia  ndio kampe  maana  amezidi, utakuwa  nawe  umeingia  kwenye  kosa  bila  kujali  ulienda  huko  lilikotokea  tukio au  haukwenda . Hizi  ni  jinai  za  kila  siku  ambazo  watu  hujikuta  wameingia  bila  kujua  na  wakifikishwa  vituo vya polisi  huanza  kulaumu kuwa  wameonewa kwa kuamini hawakutenda. Jihadhari.

1.JINAI  KUBWA.

Hapo  juu   imezungumzwa  kushauri  katika  kutenda jinai  za  kudhalilisha,kutukana  na  kupiga . Lakini  ni  muhimu  ijulikane  kuwa  suala  la  kuingia  katika  kosa  la  kushauri  kutenda  jinai  haliishii  katika  jinai  hizo. Suala  hili  huenda  mpaka  kwenye  jinai kubwa  kama  kuiba,kuvunja, kuua, uhaini, kuteka, kuumiza, n.k.

Unapotoa  ushauri   wa  namna  yoyote  ile  kwa  mtu  ambaye  anakwenda  kutenda  moja  ya  makosa  niliyotaja  hapo juu na ambayo sikutaja  na  wewe  unakuwa  umeingia  katika  kosa  hilo. Hata  kumwambia  mtu  anayekwenda  kuiba  kuwa  mlango  ule huwa  hauwekwi  kufuli  au mle  ndani hukaa  watu  wawili  huku  ukijua  kuwa  lengo  la  yule  ni  kuiba au kutenda uhalifu mwingine unakuwa  umeingia  katika  kosa.  

Usije  ukasema  hivyo  halafu ukajipa  matumaini  kuwa  kwakuwa  haupo  kwenye  tukio  basi  ndio  uko  salama. Hapana  hauko  salama na  wewe  umehusika  katika  kosa  hilo.

Kifungu  cha  22( d ) cha  kanuni  za  adhabu  kinasema  kuwa  mtu  yeyote  ambaye anamshauri  mtu  mwingine  kutenda  kosa katika  mazingira  yoyote  anaweza  kushitakiwa   kwa  kutenda  kosa  au  kwa  kushauri  kutenda  kosa. 
Hapa  yapo  mambo  mawili  ambayo unaweza  kushitakiwa  nayo. Kwanza  waweza  kushitakiwa  kwa  kutenda  kosa  hilohilo  alilotenda uliyemshauri  au  kushitakiwa kwa  kosa  la  kushauri  kutendeka  kwa  jinai.

2. KUMUWEZESHA  MTU  KUTENDA  JINAI  NAYO  NI  JINAI.

Mbali  na  kushauri   kama  tulivyoona  hapo  juu  pia  kumuwezesha  mtu  kutenda  jinai  nayo  ni  jinai.  Kifungu  cha  22( b ) cha kanuni  za  adhabu  kinasema  kuwa  kila  mtu  ambaye  anafanya  kitendo  au  anaacha  kufanya  kitendo  kwa  dhumuni  la  kumwezesha  au  kumsaidia  mtu  mwingine  kutenda  kosa  naye  atakuwa  ameshiriki  katika  kosa.

Kumwezewsha  mtu  kutenda  kosa  ni  kama  kumkodisha  au  kumpa mtu kipando  chako( gari, pikipiki n.k.), huku  ukijua  kabisa  kuwa  anakwenda  kutenda  kosa.
Au kumwelekeza  eneo  la  tukio , au  kumsaidia  kwa  zana  nyingine  yoyote , au  kumsaidia  kipesa nauli, na  namna  nyingine  yoyote  ya  msaada  wa  hali, mali  au  mawazo  wakati  akienda  kutenda  kosa  kutahesabika  mbele  ya  macho ya sheria kama kumuwezesha  mtu  huyo  kutenda  jinai. Hilo linakuingiza  hata  wewe  muwezeshaji  katika kosa.  Tunaposema  unaingia  katika  kosa  ina  maana  kuwa  utashitakiwa  naye.  

Lakini  pia kuacha  kutenda  nako  kunahesabikla  kusaidia  kuwezesha  jinai. Kwa  mfano  unaacha  kufunga  mlango makusudi  huku  ukijua  kuwa  kuna  mtu  atakuja  kuingia  kutenda  uhalifu. Hii  nayo  ni  jinai  ya  kuwezesha.
Kushauri  na kuwezesha  kutenda  kosa kunakwenda  sambamba  na kushawishi  kutenda  kosa. Kushawishi  nako  kunaingia  katika  haya na hivyo  kwapaswa  kuepukwa.

Kubwa  la  kuzingatia  katika yote ni  kuwa  ukimuona  mtu  anaelekea  kutenda  tendo  lolote  ambalo  ni  kosa  iwe  kupiga,kutukana, kuharibu  mali, kufanya  fujo, maandamano  haramu  na  vitu  vingine  ambavyo  huonekana  ni  vya  kawaida  lakini  ni  makosa  kisheria usitie  neno  lako  kwa  kuchochea,kuhimiza, au kusaidia  kwa  namna  yoyote  ile. Kufanya  hivyo  kutapelekea  na  wewe  kuunganishwa  kwenye  kosa  hilo jambo  ambalo  unaweza  ukaona  umeonewa  kumbe  laa.
                       NYUMBA  HII  INAUZWA  BOKO.


1.Ina vyumba 3, kimoja master.
2. Uwanja  unabaki  mkubwa.
3. Umeme umo na maji,jiko na public toilet.
4. Ipo Boko kwa mpemba karibu na darajani.
5. Eneo zuri tulivu kwa makazi.
6. Mita 200 kutoka  barabara  kuu ya  Bagamoyo .
7. Bei milioni 57 inapungua  kidogo.
0784482959.





0 comments:

Post a Comment